Na Mussa Augustine.
Balozi wa Tanzania
Nchini Ujerumani Dr. Ally Poss amezindua maonyesho ya awamu ya kumi ambayo yanahusu
Sanaa ya Uchoraji huku akiwataka waandaaji wa maonyesho hayo East Africa Art
Biennale Association ( EASTAFAB) kuyafanya yawe na tija zaidi kwa kuhakikisha Sanaa
ya Uchoraji iwe fursa ya uchumi kwa Taifa.
Balozi Dr. Poss
amezindua maonyesho hayo katika Kituo Cha Nafasi Arts Space Jijini Dar es
Salaam huku akisema kwamba Sanaa ya Uchoraji ni muhimu kwa Jamii kwani
inatoa elimu ,kuburudisha kupitia picha ambazo zinachorwa na wasanii wa
Uchoraji ambapo pia ni muhimu kwa wanafunzi wa shule za msingi,sekondari
na elimu ya juu ambao wanajifunza Mambo mbalimbali kupitia picha.
" Sisi Kama
serikali Sanaa ya Uchoraji na Sanaa zingine tutaendelea kuziboreshea mazingira
ili wasanii wetu waweze kunufaika na vipaji vyao,serikali imeanzisha mfuko
rasmi wa sanaa ambao utazinduliwa Novemba 15 mwaka huu, ambapo utasaidia kutoa
mikopo ya riba nafuu ili kuwainua wasanii wetu ambao wanavipaji ili
wajiendeleze" amesema Dr. Poss ambaye alikua mgeni rasmi katika uzinduzi
wa maonyesho hayo.
Kwa upande wake
Mwenyekiti na Mwanzilishi wa maonyesho hayo ya East Africa Art Biennale
Association ( EASTAFAB) Prof.Elias Jengo amesema kwamba maonyesho hayo
yatafanyika kwa muda wa siku 20 ,ambapo mwaka huu yamekua ya awamu ya kumi
tangu kuanzishwa kwake mwaka 2003 ikiwa lengo ni kuinua na kuendeleza Sanaa ya
uchoraji. " Tunakushukuru
mheshimiwa mgeni rasmi Balozi Dr. Ally Poss umetoka Dodoma na kushiriki nasi
katika uzinduzi wa maonyesho haya ,tutakua pia na kongamano ambalo
litawashirikisha wasanii wote ili watoe mawazo yao yatakayosaidia kuinua Sanaa
zetu,tutakua na maazimio ambayo tutayawasilisha kwenu serikali muweze
kuyafanyia kazi" amesema Prof. Jengo.
Awali Mkurugenzi
wa kituo Cha Nafasi Arts Space Rebecca Yeing Ae Mzengi Corey
amesema kwamba kituo hicho kitaendelea kuibua vipaji na kuviendeleza ili vijana
wengi waweze kujiajiri kupitia vipaji vyao.Mkurugenzi wa Bodi ya
Filam Dr Kilonzo kutoka Wizara ya Habari,Sanaa ,Michezo na Utamadunj
amesema kwamba wizara hiyo itaendelea kushirikiana na wadau mbalimba katika
kuhakikisha Sanaa inakua na kuwafanya wawe na kipato Cha uhakika ambacho
kitawasaidia kuendeleza shughuli zao mbalimbali za Sanaa ikiwemo maonyesho.
Mwakilishi wa Balozi
wa Norwey Annete Otilie pamoja na Mambo mengine amepongeza kuwepo kwa usawa wa
kijinsia ambapo wanawake wengi wamekuwa wakipewa nafasi ya kushiriki katika
mambo mbalimbali ya Sanaa huku akisisitiza kuwa Norwey itaendelea kusaidia
kituo hicho katika kukuza Sanaa.
Wasanii mbalimbali
kutoka Tanzania ,Kenya,Uganda na mataifa mengine wameshiriki katika maonyesho
hayo huku baadhi yao wamesema kwamba wanaipongeza serikali na wandaaji wa
maonyesho hayo katika kuendelea kukuza vipaji vyao.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni