Mkurugenzi aviburuza mahakamani vikundi vilivyoshindwa kurejesha mkopo
Mwandishi wetu
HALMASHAURI
ya wilaya Tunduru mkoani Ruvuma kupitia bajeti ya mapato ya ndani
imetenga Sh. milioni 264,570,167.88 sawa na asilimia 10 kama mikopo kwa
ajili ya kuviwezesha vikundi 20 vya kimkakati vya vijana,wanawake na watu wenye
ulemavu.
Fedha
hizo ni utekelezaji wa sera,miongozo na maagizo mbalimbali yanayohusu
uwezeshaji wa mikopo isiyo na riba kwa vikundi hivyo katika mwaka
wa fedha 2021/2022.
Hayo
yamesemwa na Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wilaya ya Tunduru Jacelyne
Mganga wakati wa utoaji mikopo ya Sh. milioni 103 kwa makundi hayo
maalum.
Alisema, fedha hizo ni kwa ajili ya kuendeleza viwanda vidogo vinavyojishughulisha
na ushonaji, usindikaji, useremala, uchomeaji, Bodaboda na kilimo cha kimkakati
cha mazao ya chakula na biashara.
Alisema,
vikundi vilivyopata mikopo ni vyenye sifa ambapo Sh.milioni 50 fedha
zilizotokana na asilimia 10 ya robo ya kwanza ya mwaka 2021/2022 na Sh.milioni
53 ni fedha zilizotokana na marejesho kutoka kwa makundi hayo.
Aidha alisema, kwa siku za usoni Halmashauri inakusudia kufanya maamuzi magumu
ya kupeleka fedha za mikopo kwa vikundi vilivyo na miradi endelevu inayofanya
kazi, badala ya fedha hizo kupeleka kwa vikundi vilivyobuni mradi.
Kwa mujibu wa Mganga,hatua hiyo ni baada ya kubaini miongoni kuwa changamoto za
marejesho ya mikopo imevikumba vikundi vingi vilivyobuni miradi kushindwa
kutekeleza na hatimaye kushindwa kurejesha mikopo kwa wakati.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Tunduru Chiza
Malando alisema katika utekelezaji wa mpango wa kutoa mikopo changamoto kubwa
ni urejeshaji wa mikopo hiyo kwa baadhi ya vikundi jambo lililoifanya
Halmashauri kuchukua hatua ya kuwapeleka mahakamani wana vikundi walioshindwa
au kuchelewa kurudisha mikopo.
Malando amewaomba wana vikundi waliopata fedha hizo, kuhakikisha wanakwenda
kuzifanyia kazi iliyokusudiwa na wanarejesha kwa wakati ili ziweze
kukopeshwa kwa vikundi vingine vyenye mahitaji.
Mkuu wa wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro amewaasa wana vikundi kuupokea mkopo
huo na kurejesha kwa wakati ili vikundi vingine viweze kunufaika.
Mtatiro, amepiga marufuku tabia ya baadhi wana vikundi kugawana
fedha hizo na kutekeleza mradi wa mtu mmoja mmoja kwani ni hatari kwa kuwa
vikundi vingi vinashindwa kurejesha kwa taratibu zilizotumika awali.
Aidha alisema, kumekuwa na malalamiko mbalimbali kutoka katika wana kikundi
hususani baadhi ya watu kuitaji fedha za mkopo na kutumia bila ya utaratibu
hivyo kusababisha vikundi vingi kusambaratika
Hakuna maoni
Chapisha Maoni