Maandalizi sensa yafikia pazuri, sasa kufanyika kidigitari kwa asilimia 100
Na Suleimani Magali
Imeelezwa kuwa maandalizi ya sense ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika Agost, 2022 yamefikia
asilimia 50, ambapo kwa sasa wanaendelea na zoezi la kutenga maeneo ya kuhesabu
watu pamoja na kuhamasisha watu kujitokeza kushiriki katika zoezi hilo la
kuhesabiwa.
Hayo yamebainisha na Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu
Dkt. Albina Chuwa, wakati wa makabidhiano ya kompyuta kutoka Serikali ya
Uingereza.
Aidha ameongeza kusema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania imepanga kufanya Sensa hiyo kidigitali kwa asilimia mia (100%) kwa
nchi nzima.
“Tanzania inatarajia
kufanya sensa ya Sita Agosti, 2022, sensa hiyo tutaifanya kidigitali kwa
asilimia mia ili kurahisisha zoezi la kuhesabu watu na makazi. Tumeshafanya
majaribio kama ambavyo Umoja wa Mataifa unavyotuelekeza kufanya,” alisema Dkt. Chuwa.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Benki ya Dunia hapa nchini,
Rob Swinkels, amesema kuwa, wametoa compyuta hizo kwa Ofisi ya Takwimu Bara na
Zanzibar ili kuboresha zoezi la sensa na kupata data sahihi, pia
kurahisisha zoezi la ukusanyaji data kwa haraka ili Serikali na Taasisi
nyingine ziweze kufanyia kazi data hizo kwa ajili ya maendeleo ya nchi.
Naye Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu
(UNFPA), Jacqueline Mahon amesema kuwa, wametoa kompyuta hizo ili kuhakikisha
kila Mtanzania anahesabiwa ili kupata takwimu ambazo ni sahihi katika sensa
hiyo itakayofanyika Agosti, 2022.
Aidha, Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, Anne
Makinda amesema kuwa, kompyuta hizo sio msaada sababu data zitakazopatikana
hazitatumika Tanzania peke yake bali zitahitajika pia katika takwimu za
dunia na hata mashirika ya kimataifa kama vile UNFPA na Benki ya Dunia.
Serikali ya Uingereza imetoa kompyuta mpakato 28 na kompyuta za
mezani 20 ambazo zitatumika katika sensa ya watu na makazi Agosti, 2022 hapa
nchini.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni