Embe zikiwa nyingi mwaka huo ni wa njaa? wakulima waanza kujikatia tamaa na mvua za vuri
Kwa desturi maeneo ya pwani na maeneo yaliyo jirani na maziwa na bahari huwa yanapata mvua za vuri-Mvua za Kivuli kama ambazo hunyesha katika maeneo haya kabla ya kunyesha kwa mvua za masika huku maeneo ambayo hayako jirani na vyanzo hivyo hunyesha mvua za masika tu.
Maeneo haya yaliyo jirani na bahari na maziwa hupata bahati hiyo
ya mvua mara mbili ambapo kwa hakika hali hiyo hufanya maeneo hayo kuwa na
rangi ya kijani mwaka mzima (chanikiwiti). Lakini maeneo mengine hupata mvua ya
mara moja kwa mwaka na kukumbwa na kiangazi kirefu.
Katika maeneo haya ya pwani mara nyingi mvua hizo za vuri huitwa
mvua za korosho, mvua za embe na majina mengine kulingana na wapendavyo
wakulima na wakaazi wa maeneo hayo.
Mvua hizo huitwa hivyo kwa kuwa kipindi zinanyesha tayari maua ya
embe, kprosho na matunda mengine huchanua na mvua huja kuweka mambo sawa na maua
haya huwa vizuri sana kuzaa matunda.
Wale wanaoita mvua za vuri kama mvua za kivuli wanamaanisha kuwa
mvua hizo huja na kuongeza majani katika mmea na kuongeza kivuri katika mmea
huo.
Mwaka huu katika maeneo mengi ya pwani mvua hiyo haijanyesha
kabisa au imepiga rasharsha tu huku
wakulima waliokuwa wakitegemea mvua za vuri kulima mahindi,kunde na
mazao mengine ya muda mfupi wamekuwa wakisubiri na hakuna mvua iliyonyesha
kabisa
Baadhi ya wakulima hao mathalani kwa mkoa wa Tanga, Pwani , Morogoro,
Mtwara na Lindi walikuwa tayari wametayarisha mashamba yao kwa ajiri ya kulima
mazao haya na kupanda mbegu za muda mfupi, mbegu zao zimebaki katika hifadhi
zao yaani kwenye ndoo, mitungi na mifuko yao wakikata tamaa kwa kuwa mvua hizo
hazioneshi dalili ya kunyesha kabisa.
“Mvua ya vuri mwaka huu haipo na hata kama mvua itanyesha iwe mwezi
wa kumi na moja au kumi na mbili nadhani mvua hiyo haitokuwa mvua ya vuri tena
bali hiyo itakuwa mvua ya mwaka na mimi nimeshatayarisha shamba langu kwa ajili
ya kupanda mbegu za mwaka .” Anasema kijana Ramia Hassani Mkaazi wa Handeni
Tanga.
Japokuwa wakulima hao wamekata tamaa lakini wana matumaini makubwa
ya kunyesha mvua ya masika mapema kama alivyosema kijana Ramia kwa hiyo kutokunyesha
huko kwa vuri kunawapa matumaini mengine wakulima hao, binafsi hilo naliona
kuwa ni jambo jema sana kwa mkulima wa jembe la mkono.
Je mvua itanyesha au la? Dada yangu Agness Kijazi Mkurungezi wa mamlaka
ya hali ya hewa Tanzania ameendelea na kufanya tabiri mbalimbali juu ya mvua
hizo tayari alishatoa tahadhari ya uhaba wa mvua za kutosha mwaka huu. Utabiri
huo unamaanisha kuwa kama mkulima anayo mazao katika hifadhi yake ana wajibu wa
kuyahifadhi vizuri ili yaweze kutunzwa na kumsaidia muda hali ikiwa tete zaidi.
Wale wanaotaka kuuza mazao lakini wana hifadhi ndogo wanawajibu wa
kutambua kuwa uuzaji huo unaweza kuwapa mashaka zaidi kwani mvua za vuri ndiyo
zimeshapita sasa tuangalia hayo matokeo ya mvua za mwaka (mvua za masika).
Jambo hili si geni kwa mikoa kama Singida, Dodoma, Tabora, Shinyanga
kwa kuwa wao matarajio yao makubwa ya mvua ni mwaka hadi mwaka tu. Wakulima wanawajibu
kufanya maandalizi ya mashamba huku utunzaji wa chakula kilichopo kuwa
maradufu.
Kwa wakaazi wa Mikoa ya Morogoro Tanga, Pwani na Dar es Salaam wamekuwa
na misemo mingi juu ya mvua, utaambiwa kuwa ukiona mwaka huu embe nyingi tambua
mwaka huo ni mwaka wa njaa.
Wanasema hivyo kwa hoja moja kubwa kuwa mvua ikinyesha kidogo tambua
maua ya embe huwa mengi na mvua kidogo
haiwezi kuyatikisa sana matawi ya miti ya matunda ikiwamo miembe kwa
hiyo embe hukua vizuri na kuwa nyingi mwaka huo.
“Mwaka huu hapa kwetu embe ni nyingi nimefika nyumbani na shambani
kwangu nimekuta embe zimezaa sana matawi yamefungana hadi chini kwa hiyo nasema
kuwa mwaka huu ni mwaka njaa kwa kuwa mvua zimenyesha kidogo, hili lipo tangu
enzi.” Anasema Mzee Michael Mbena mkaazi wa Mboga Chalinze ambaye ni mzee wa
miaka 80.
Hayo ni ndiyo wasemavyo wakulima na hali ya mvua ya mwaka huu
lakini kubwa ni kuomba Mungu mvua hizo zikinyesha zinyeshe kulingana mahitaji
ya jamii ya Watanzania ili kuondokana balaa la njaa ambalo linaweza kutokea
kama hzio mvua za mwaka hazitonyesha, Nakutakia siku njema.
0717649257
Hakuna maoni
Chapisha Maoni