TMA wajichimbia Morogoro kufanya tathmini, M’kiti awataka wakusanye mapato
TMA wajichimbia Morogoro kufanya tathmini, M’kiti
awataka wakusanye mapato
Na Suleimani Magali
Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Hali ya Hewa
Tanzania (TMA), Dkt. Buruhani Nyenzi amewapongeza watendaji wa mamlaka hiyo kwa
kukamilisha zoezi la kuandaa kanuni za kutekeleza sheria namba 2 iliyotungwa
mwaka 2019 ikiwemo kanuni ya tozo. Pia Dkt Nyenzi ameiagiza TMA kusimamia
sheria kikamilifu.
Akizungumza katika semina ya ufunguzi wa Baraza la Wafanyakazi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), lililofanyika katika Ukumbi wa Magadu, Morogoro, Dkt Nyenzi amesifu utendaji kazi wa mamlaka huku akiwasisitiza wajitahidi katika suala la kukusanya mapato.
“Nawaagiza mkasimamie Sheria hii kikamilifu ikiwa ni
pamoja na ukusanyaji wa mapato katika maeneo yaliyoainishwa. Hii itasaidia
kuwezesha utekelezaji wa majukumu yenu kwa ufanisi mkubwa pamoja na kutatua
changamoto mbali mbali zilizo katika uwezo wenu”.Alisema Dkt. Nyenzi
“Nimejulishwa pia kuwa ili kutekeleza sheria
iliyoanzisha taasisi hii mmefanikiwa kuandaa kanuni zitakazowezesha utekelezaji
wa sheria hiyo. Katika eneo hili, niwapongeze kwa kukamilika kwa Kanuni saba za
Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Na. 2 ya mwaka 2019 ikiwemo Kanuni
ya Tozo, natambua kuwa kanuni hizi zimeshasainiwa, kilichobaki ni utekelezaji
wake”.Alizungumza Dkt. Nyenzi.
Aidha, Dkt. Nyenzi aliipongeza TMA kwa kazi nzuri
inayofanya na kuwataka kuchapa kazi kwa bidii na kuendelea kutoa taarifa kwa
watoa maamuzi ili kusaidia ufanyaji wa maamuzi na kuwezesha Serikali
kukabiliana na changamoto zinazosababishwa na matukio ya hali mbaya ya hewa
ambayo yanazidi kuongezeka kutokana na mabadiliko ya tabianchi.
Akizungumzia ushiriki wa TMA katika Mkutano mkubwa
wa mabadiliko ya tabia nchi maarufu COP26 ambao Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alishiriki na kuhutubia mkutano, Dkt Nyenzi
alisema anatambua katika maazimio ya mkutano huo TMA inajukumu la kufanya ili
kufanikisha jitihada za kuhimili athari za mabadiliko ya tabia nchi.
Amesema anaamini jukumu hilo litatimizwa vyema kwani
TMA ina wataalamu wanaokubalika kimataifa wakiwemo wajumbe katika kamati mbali
mbali za Shirika la Hali ya Hewa Duniani akiwemo Mwenyekiti wa Baraza anayeshika nafasi ya Makamu wa tatu wa Rais wa
Shirika la Hali ya Hewa Duniani
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa
Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) Dkt. Agnes Kijazi
aliishukuru Serikali na kueleza madhumuni maalum ya Baraza hilo ni kufanya tathmini
ya utendaji wa Mamlaka.
Amesema wanaamini
tathmini itasaidia kuongeza ubora na ufanisi katika utoaji wa huduma kwa
umma kwa lengo la kupunguza athari za mabadiliko ya hali ya hewa na tabia nchi.
“Hivi karibuni tumeshuhudia athari mbalimbali zitokanazo
na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi ikiwa ni pamoja na kuwa na vipindi
vya ongezeko la joto hadi kufikia nyuzi joto 35.6 kwa maeneo ya ukanda wa
Pwani.
Aidha, nichukuwe fursa hii kuendelea kutoa wito kwa
watanzania wenzangu kuendelea kufuatilia taarifa za hali ya hewa zinazotolewa
na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania kila mara ili kupunguza madhara yatokanayo
na hali mbaya ya hewa”.Alifafanua Dkt. Kijazi.
Vile vile, Dkt. Kijazi alieleza baadhi ya changamoto
zinazoikabili mamlaka hiyo ni pamoja na ni mishahara midogo hali inayopelekea
wataalamu kuhamia katika Taasisi zingine.
Hata hivyo amesema jambo hilo litafika mwisho mara
tu ‘Job Evaluation’ itakapofanyiwa kazi,
Hakuna maoni
Chapisha Maoni