Zinazobamba

Wanafunzi waliomaliza la saba 2021 wahimizwa tabia njema mtaani

 




Mwandishi wetu

Wanafunzi waliomaliza darasa la saba jana wameaswa kuendeleza utamaduni wa maadili mema waliyopata shuleni husan katika shule za dini.

 

Kwa upande wa mabinti wametakiwa kuendelea kuvaa hijabu zao za kisheria kama ambavyo walivyokuwa shule ya msingi na kujisimamia na kuyasoma masomo ya elimu ya dini huko wanakoenda katika shule za sekondari.

Wito huo umetolewa na Mzee Khalifan Mikidadi, ambaye kwa muda mrefu amekuwa mlezi wa wanafunzi hususan katika shule za jiji la Dar es Salaam, wakati wa dua maalum ya kumuomba Allah (SW), ili kuwakurubisha wanafunzi hao kwa Mola wao na kuamini Allah ndio kila kitu katika maisha yao.

Hafla hiyo ya kuwaombea  dua wanafunzi wa darasa la saba ilifanyika mwishoni mwa wiki iliyopita katika Msikiti wa Buza.

 

Katika dua hiyo, wanafunzi wametakiwa kujiandaa na maisha baada ya kumaliza mitihani yao ya darasa la saba, huku wakitakiwa kuwa na tabia njema popote walipo kwani hiyo ndio sifa kuu ya Muislamu.

 

Dua hiyo iliambatana na semina kutoka kwa wataalamu mbalimbali kwa lengo la kuwaandaa na kuwapa moyo wanafunzi hao kufanya juhudi katika kusoma,  huku wakimuomba Mola wao kwani kwa kufanya hivyo mitihani yao inakuwa mepesi.

 

Aidha Mzee Mikidadi, ametoa wito kwa wazazi kuwa makini na tabia za watoto na kuwachunguza mara kwa mara ili kubaini mapema athari zinazotokana na marafiki wenye maadili mabaya, kwakuwa wanahama kutoka shule ya msingi  na kuelekea katika masomo ya sekondari.

Alisema wanafunzi waliomaliza darasa la saba wakiwa sekondari, wana tabia ya kujiona wamekuwa na wametoka kwenye utoto na kuanza kuwa watu wazima, hivyo hata tabia na mienendo yao inabadilika.

“Kipindi hiki watoto hawa wanakuwa katika kipindi kigumu kipindi cha mpito kwakuwa ndio wakati mgumu katika malezi, ukifanikiwa hapa ndio umefanikiwa kwa mtoto huyo na ukimuacha aende ovyo, utakuwa umempoteza mtoto huyo”. Alifafanua Mzee Mikidani wakati wa hafla hiyo ya dua.

Alisisitiza wazazi kuwafuatilia watoto hawa na kuwa nao karibu kwa kipindi ambacho  wanasubiria matokeo ya mitihani, wasiawaache kuzagaa na kuzurura hovyo hovyo mitaani.

Sheikh Taufiq Ibrahim, Afisa Mahusiano  Ofisi ya Mufti ambae alikuwa mgeni rasmi katika dua hiyo, aliwataka wanafunzi kuyatumia maneno ya Allah (SW) katika kitabu kitakatifu Qur’an, kama ambavyo amesema Allah (SW):

 “Niombeeni nami nitakujibu. Hayo ni maneno ya Mwenyezi Mungu na hakuna budi kutekelezwa.  

Sheikh Taufiq amewataka wazazi na walezi kuwaanda watoto wao katika maisha ya kumfurahisha Allah (SW) kila hatua wanayoiendea.

Amewataka wazazi kuwaombea dua  kwa Allah watoto, kuwaondolea wasiwasi wakati wa Mitihani kwa kusoma jina la Allah Assalamu  na jina  Al Basitu.

Alisema majina hayo matukufu ya Mwenyezi Mungu  yana miujiza mikubwa wakati wa kukabiliana na mitihani na kusubiri matokeo.

Akasisitiza wazazi kukithirisha dua kwa watoto wao, ili wapate mafanikio katika maisha yao.

Naye Ust. Salimu Bakiri, aliwataka watoto hao kufanya maandalizi katika kuyaendea masomo yao ya kidato cha kwanza kwa kujisomea ili watakapofika kidato cha kwanza, watakuwa wamepata mwanga katika masomo yao hayo.

 

Hakuna maoni