Zinazobamba

Mavazi ya mama Samia: Waislam wamjibu Muimbaji wa Muziki wa Injili, Faustin Munishi,



TAMKO LA WAISLAM  KUHUSU UDHALILISHAJI ULIOKUSUDIWA KWA RAIS WA TANZANIA, MAMA SAMIA SULUHU HASSAN

 

 

UMOJA WA WANAZUONI WA KIISLAMU TANZANIA

 

Kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, Mhe. Spika Wa Bunge,

Mhe. Jaji Mkuu,

Mhe. Spika Baraza la Wawakilishi,

Mhe. Mufti-Baraza Kuu la Waislamu Tz (Bakwata), Mhe. Mufti wa Zanzibar

Mkiti-Baraza la Maaskofu (Tec), Mkiti Baraza la Maaskofu (Kkkt) Kamanda wa Polisi (IGP) Vyombo Vyote vya Habari, Mitandao Yote ya Kijamii,

Kwa Watanzania Wote

 

As-salaam alaykum Warahmatullahi Wabarakatuhu.

 

YAH: TAMKO LA WAZI KWA UDHALILISHAJI ULIOKUSUDIWA KWA RAIS WA TANZANIA, MAMA SAMIA SULUHU HASSAN

 

“Rais Samia Si Rais wa Waslamu Lakini ni Rais Muislamu”

 

Mnamo siku chache zilizopita, ujumbe mfupi wa maandishi kutoka kwa Muimbaji wa Muziki wa Injili, Faustin Munishi, ulisambaa katika mitandao ya kijamii ukizungumzia uvaaji wa Rais wetu mpendwa Mama Samia Suluhu Hassan.

 

Mwandishi alituhumu uvaaji wa Rais wetu hususani uvaaji wake  wa  ushungi  (Hijab), yaani kufunika kichwa, nywele zake zisionekane kama ilivyo agizo la Mwenyezi Mungu, “Ewe Nabii waambie wake zako na binti zako na wake wa Waumini Waislamu wateremshe shungi zao hadi vifuani mwao…” (Qur’an 33:59).

 


Bwana huyu mtovu wa adabu na heshima kwa Rais aliandika, “Tanzania siyo Islamic Republic. Kule Afghanistan mama Samia akivaa hivyo ni sawa. Wao wametangaza Afghanistan kuwa nchi ya Kiislamu inayoongozwa na sharia. Tanzania tuna dini nyingi hivyo Rais avae kiraia kama  marais waliomtangulia.  Yeye Samia siyo  Rais  wa Waislamu ni Rais wa watanzania wote. Hivyo watanzania tungependa kumuona Rais wetu sote  siyo  tukimuona  Rais  image  inakuwa  mama  muislamu mswahili  wa uswahilini. Kwa maoni yangu Samia anashusha hadhi ya taasisi ya urais na kuifanya ionekane kama mama wa kiswahili mpika vitumbua. Wasaidizi wa Rais "President hundlers" hawajaliona  hilo?  Wamshauri  rais  avae  suti  za kike za heshima  ili kudumisha Mamlaka ya taasisi ya  urais.  Tuwe  wakweli,   rais  Samia  akihutubia unayaona Mamlaka  ya  taasisi  ya  Urais  au  unamuona  mama  wa  Kiswahili Muislamu?”

 

Ukiyasoma maneno hayo ya msanii wa Muziki wa Injili, Mchungaji Munishi, unaiona wazi dhamira ya mwandishi akidhihirika kwa sura ya chuki binafsi ya kidini”. Tunasema chuki binafsi ya kidini kwa sababu tarehe 25 Juni 2021, Rais wetu Mama Samia alikutana na Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini (TEC) jijini Dar es Salaam akiwa amevaa uvaaji wake huo huo unaolaaniwa na Munishi na hawakumtaka avae suti ya kike ili aongee nao.

 

Tukirejea katika maandishi yake anadai mambo kadhaa yasiyo na msingi ambayo kama si mafundisho ya Dini yetu, kutuamrisha kulinda heshima za watu zisivunjwe na hususani wanawake, tungenyamaza tu kama wengine walivyonyamaza.

 

Munishi anadai kwamba: -

 

i)                  Tanzania si Islamic State

ii)                Rais Samia si Rais wa Waislamu ni Rais wa Watanzania wote

iii)              Rais Samia anaonekana na image (taswira) ya mama Muislamu Mswahili wa Uswahilini

iv)              Rais Samia anashusha hadhi ya taasisi ya urais na kuifanya ionekane kama (ya) mama wa kiswahili mpika vitumbua

v)                Washauri wa Rais wamshauri avae sutiza kike za heshimaili kudumisha Mamlaka yataasisi ya uraisi

 

Dondoo ya (i) na (ii) hatuna mushkeli nazo kwani kweli Tanzania si Islamic State (Dola ya Kiislamu) na Rais Samia Suluhu Hasan si Rais wa Waislamu bali ni Rais wa Watanzania wote. Kwa hayo mawili hakuna mwenye tatizo nayo, kwani yako kwa  mujibu  wa  Katiba ya Tanzania ibara ya 3. (1) inayoelezea Tanzania ni nchi ya namna gani na ibara ya 19.(1) na 20.(1) zinazozungumzia uhuru wa mtu juu ya imani, kuabudu na kujiunga na dini anayotaka.

 

Lakini kwa mujibu wa dondoo ya (iii) hadi ya (v) hapo juu zinazotokana na maneno ya Bwana Munishi, sisi Umoja wa Wanawazuoni wa Kiislamu Tanzania (Hay-atul Ulamaa),


tunapinga kwa nguvu zote kashfa na kukosa adabu kwa bwana Munishi na wengineo wenye matamshi ya aina hii na fikra potofu za aina hii kwa Rais wa Tanzania mama Samia Suluhu Hassan.

 

Mosi, madai kwamba “Rais Samia anaonekana na image (taswira) ya mama Muislamu Mswahili wa Uswahilini” tunasema si kosa wala dhambi kwa mama Samia kuonekana hivyo. Tena tunampongeza na kumheshimu kwa kulinda na kudumisha utamaduni wa mama Muislamu wa Kiswahili hata akiwa Rais wa nchi.

 

Hakuna ibara yoyote ile ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayombagua mama Muislamu wa Kiswahili, au Mkiristu wa Kiswahili au wa Kichagga au wa Kisukuma au wa Kigogo kuwa Rais wa Tanzania.

 

Ibara ya 39 (1) (a)-(e) inazitaja sifa za Rais wa Tanzania kwamba, “Mtu hatastahili kuchaguliwa kushika kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano isipokuwa tu kama:

 

(a)   ni raia wa kuzaliwa wa Jamhuri ya Muungano kwa mujibu wa Sheria ya Uraia.

(b)  ametimiza umri wa miaka arobaini;

(c)  ni mwanachama, na mgombea aliyependekezwa na chama cha siasa;

(d)   anazo sifa za kumwezesha kuwa Mbunge au Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi;

(e)  katika kipindi cha miaka mitano kabla ya tarehe ya Uchaguzi Mkuu hajawahi kutiwa hatiani katika Mahakama yoyote kwa kosa lolote la kukwepa kulipa kodi yoyote ya serikali.

 

Rais wetu mama Samia, anakidhi sifa zote hizo ndiyo maana akashika wadhifa wa makamu wa Rais na hatimaye sasa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Suala la kuwa kwake mama Muislamu wa Kiswahili halina nafasi katika mamlaka ya Urais na mtu akiingiza mambo hayo bila shaka anakuwa amekusudia kuvunja tu na kudharau hadhi ya Raisi.

 

Pili, bwana Munishi kudai kwamba “Rais Samia anashusha hadhi ya taasisi ya urais na kuifanya ionekane kama “(ya) mama wa kiswahili mpika vitumbua”, maneno haya yanakusudia tu kumtukana, kumdharau na kumvunjia heshima na hadhi Raisi wetu na watanzania wote.

 

Uvaaji wa Rais Samia Suluhu Hassan haujakiuka “Mwongozo wa mavazi kwa  watumishi  wa umma kwa mujibu wa Waraka wa utumishi wa umma Na. 3 wa mwaka 2007” maarufu kwa Kiingereza kama, Dress Code for Public Servants.

 

Rais ni mtumishi wa umma nambari moja na analazimika kuvaa kwa mujibu wa waraka huo uliotolewa na “Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi” mwaka 2007 wakati wa utawala wa Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete na Makamu wake akiwa Mheshimiwa Ali Mohamed Shein. Wakati huo hata Mama Samia hajawa makamu wa Rais.


Ndiyo maana tunawaona waheshimiwa wabunge katika bunge la Jamhuri ya Muungano na wawakilishi katika Baraza la Wawakilishi Zanzibar wanawake wakivaa kama avaavyo mama Samia na wanaume wakivaa hata kanzu wakiwa bungeni au katika Baraza la Wawakilishi.

 

Mbona hatujawahi kumsikia Mchungaji mwenye chuki na Uislamu, Faustin Munishi, akisema waheshimiwa wabunge na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wanaovaa ushungi kama mama Samia wameshusha hadhi ya bunge au Baraza la Wawakilishi?

 

Ni mara ngapi Rais aliyemtangulia Rais Samia, Rais mwendazake John Joseph Magufuli, ambaye ni Mkatoliki alionekana amevaa kanzu na kofia kama wavaavyo Waislamu tena akiwa katika majukumu yake ya Kirais?

 

Tatu, kudai kwake kwamba “Washauri wa Rais wamshauri rais avae suti za kike za heshima ili kudumisha Mamlaka ya Taasisi ya urais”, huu ni ujinga uliobobea kwa sababu mamlaka ya Taasisi ya Urais imeelezwa katika ibara za  katiba  Sura ya pili ibara ya 33. (1) mpaka 46 (B).

 

Hakuna mahali katika katiba yetu mamlaka ya Taasisi ya urais yamefungamanishwa na uvaaji wa Raisi. Bwana Munishi kwa ujinga wake ameandika “Tanzania tuna dini nyingi hivyo Rais avae kiraia kama marais waliomtangulia”. Kwani mavazi ya Rais Samia ni mavazi ya kijeshi na siyo ya kiraia? Kwa akili zake finyu Munishi anataka kutuaminisha uvaaji wa mama Samia si wa kiraia. Kwa maneno mengine Munishi hatambui uvaaji wa Waswahili, kwa hivyo kwake si uvaaji wa kiraia. Huu mtazamo ni mgeni mno kwa Watanzania.

 

Ni wazi kwamba Munishi ana chuki binafsi tena za kidini dhidi ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan na ametaka tu kuficha chuki yake hiyo katika kivuli cha kutetea mamlaka ya Taasisi ya urais.

 

Kutokana na maelezo hayo hapo juu, sisi viongozi wa Umoja wa Wanawazuoni wa Kiislamu Tanzania (Hay-atul Ulamaa) tunatoa kauli ifuatayo dhidi ya maandishi ya Mchungaji muimbaji wa nyimbo za Injili Faustin Munishi:-

 

Mosi, tunalaani na kupinga kwa nguvu zote kauli za kumdhalilisha Rais wetu mpendwa wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan kwa uvaaji wake wa heshima wa Kiislamu ambao uko kwa mujibu wa Dini yake na pia Waraka wa Tume ya Utumishi juu yamavazi wa mwaka 2007.

 

Pili, tunalaani na kupinga kwa nguvu zote juhudi za kutenganisha dini ya mtanzania yeyote na mamlaka aliyonayo katika serikali au taasisi za umma kwa mujibu wa uvaaji wake au kujihusisha kwake na ibada za Msikitini au Kanisani kwa mujibu wa dini yake.


Tatu, tunamtaka bwana Munishi aache mara moja kutoa maneno ya kashfa, matusi na udhalilishaji kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;  na  asipoacha  kufanya  hivyo tunaviomba vyombo vya dola kutekeleza wajibu wao wa kulinda  katiba  ya  nchi ikiwa ni pamoja na kuilinda hadhi na heshima ya  Taasisi ya  urais Tanzania, bila  kujali  dini, jinsia, kabila wala rangi ya mtu.

 

Nne, tunampongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kulinda imani na utamaduni wake katika mavazi hata akiwa Rais na kumtaka aendelee kuvaa kama avaavyo. Kwani hadhi na heshima ya Taasisi ya urais ambayo yeye ndiye mkuu wake itatokana na utendaji kazi wake na wala si mavazi yake ya suti za kike.

 

Raisi Samia Suluhu Hassan ni Rais wa Watanzania wote lakini pia ni Raisi mwenye Dini ya Uislamu kama ilivyokuwa kwa Baba wa Taifa Julius Nyerere alikuwa ni Mkristo. Raisi Ali Hassan Mwinyi alikuwa ni Muislamu, Raisi Benjamin William Mkapa alikuwa ni Mkristo, Raisi Jakaya Mrisho Kikwete alikuwa ni Muislamu, na Raisi John Joseph Magufuli alikuwa ni Mkristo. Na sasa Raisi Samia Suluhu Hassan ni Raisi mwenye Dini ya Uislamu, tena mwanamke Mswahili kutoka Visiwa vya Karafuu, Zanzibar. Hii ndio katika tamaduni zetu hapa Tanzania.

 

Chuki za namna hii hazipaswi kupewa nafasi zikakomaa katika nchi yetu. Tunaviomba vyombo vya dola kutokupuuza maneno kama haya kwa sababu moto huanza na cheche moja tu.

 



Tunawaasa Watanzania kuweka mbele utaifa wao na kushikamana kwa misingi ya amani, haki na uadilifu ili kuendeleza utangamano wa kipekee wa taifa letu barani Afrika. Mwenyezi Mungu Anatuambia: “Enyi watu, hakika Mimi Nimekuumbeni kutokamana na mwanamme mmoja (Adam) na mwanamke mmoja (Hawaa), na Nimekufanyeni mataifa na makabila ili mpate kujuana, hakika mbora wenu mbele ya Allah ni yule aliye MchaMungu Zaidi yenu.” (Qu’an 49:13)

 

 

 


Hakuna maoni