MIRADI YA MAENDELEO IMETEKELEZWA KWA ASILIMIA 89 ILALA:DC MPOGOLO.
*Amshukuru Dkt Samia kwa kutekeleza miradi ya maendeleo yenye tija kwa Wananchi.*
Na Mussa Augustine.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mh.Edward Mpogolo,amesema kuwa Wilaya yake imekamilisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa zaidi ya asilimia 89,hatua inayoakisi kasi kubwa ya utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilayani humo.
DC Mpogolo amesema hayo leo Februari 25,2026 Jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na Waandishi wa habari mara baada ya kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa kipindi cha Julai hadi Desemba 2025,huku akimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuunga mkono na kusukuma mbele miradi ya maendeleo yenye tija kwa wananchi.
Ameeleza kwamba Wilaya ya Ilala ina zaidi ya watoto laki nne(400,000)wanaosoma katika shule za msingi na sekondari,hali inayosababisha changamoto ya upungufu wa vyumba vya madarasa na madawati.
Amesema kuwa Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam imejikita kuongeza miundombinu ya elimu ili kuhakikisha watoto wanapata mazingira bora ya kujifunzia ili kuongeza ufaulu.
Mkuu huyo wa Wilaya ya Ilala amesema kuwa Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam imetenga Shilingi milioni 400 kwa elimu ya msingi na Shilingi milioni 400 kwa shule za sekondari kwa ajili ya utengenezaji wa madawati nakwamba wakandarasi wameanza kutengeneza madawati hayo ili kupunguza uhaba uliopo mashuleni.
"Katika bajeti ya mwaka 2026/2027, Halmashauri imetenga Shilingi bilioni moja kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarsa,hatua inayolenga kukabiliana na ongezeko la wanafunzi na kuboresha ubora wa elimu." amesema DC Mpogolo
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Jiji la Ilala, Nurdin Bilal(SHETTA),amewaomba wajumbe wa Halmashauri kuu ya CCM Wilayani humo kushiriki mafunzo ya pamoja ya maadili na uongozi bora,ili kuongeza ufanisi katika kuwatumikia wananchi na kusimamia vyema miradi ya maendeleo.
Amesema kuwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam pia inatarajia ifikapo mwaka 2028 idadi ya watoto wanaoanza Kidato cha Kwanza itaongezeka kwa kiasi kikubwa, huku makadirio yakionyesha zaidi ya watoto 65,000 watajiunga na ngazi hiyo,hali inayohitaji maandalizi ya mapema ya miundombinu ya elimu.






No comments
Post a Comment