Serikali yaombwa kuifuta sheria ya ugaidi, wadau wasema imejaa uonevu
Na. Heavenlight
Bomani
Ofisi ya habari ya
Hizb Ut Tanzania, imeitaka serikali kufutilia mbali sheria ya ugaidi kwani
inapinga misingi mingi ya haki ikiwemo kumnyima mtuhumiwa dhamana, pamoja na
fidia baada ya kumuweka mahabusu kwa miaka mingi.
Akizungumza na
waandishi wa habari, katika ukumbi wa Hotel ya Travertine jijini Dar es salaam,
Mwakilishi kwa vyombo vya habari Hizb Ut Tahrir Tanzania Masoud Msellem,
amesema matumizi ya sheria hiyo yanaharibu mahusiano mema ya kijamii.
Ameongeza kuwa,
sheria hiyo ni ya kibaguzi inayolenga kuwakamata na kuwatuhumu kundi fulani
ndani ya jamii yaani waislamu.
"Kubwa zaidi
sheria hii inatoa mwanya kwa watendaji waovu kudhulumu na kuleta uonevu na
kutumika vibaya, hivyo katika kuepusha madhara zaidi ya sheria hiyo tunataka
sheria hiyo ifutwe kabisa ili kujenga jamii yenye utengamano, mshikamano isiyo
na chuki" alisema Masoud Msellem.
Aidha, alisema
kuachiwa huru kwa masheikh wa uamsho kuwe mwanzo wa kutendewa haki kwa mahabusu
wengi walio baki, kwani kuna mahabusu wengi wa mashtaka kama hayo ya ugaidi
bado wanasota magerezani.
Alisema ndani ya
mkoa wa Dar es salaam pekee kabla ya kuachiwa masheikh wa uamsho kulikuwa na
mahabusu wa aina hiyo 140, Arusha wakiwa 60, pamoja na Mtwara ambako
wanaharakati watatu wa Hizb Ut Tanzania wamekuwa wakishikiliwa kwa mashtaka ya
ugaidi karibu miaka minne(4).
"Tunaendelea tena
kusisitiza msimamo wetu kwa Taasisi za kusimamia haki kama uliokuwa katika
kampeni yetu ya Juni 2020, kwamba mahabusu wote katika mikoa mbalimbali
waachiwe huru, wapewe dhamana au kesi zao zisikilizwe kwa haraka" alisema
Masoud.
Pia, alitoa wito kwa
Mamlaka husika kutoburuzwa na propaganda za magharibi kwa jina la ugaidi, na
kueleza kuwa tarumbeta ya vita vya ugaidi ni chuki ya madola ya Magharibi dhidi
ya uislamu na waislamu, na badala yake watafiti uislamu kupitia vyanzo vyake
sahihi.
Hata hivyo,
tamko hilo la Hisb Ut Tahrir Tanzania, limekuja siku chache mara baada ya
Mkurugenzi wa Mashtaka(DPP) Sylvester Mwakitalu kuwafutia mashtaka masheikh
wote 36 wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar(JUMIKI),ambao
wamesota magerezani kwa zaidi ya miaka 7.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni