Zinazobamba

NEEC YASAINI MAKUBALIANO YA USHIRIKIANO NA KAMPUNI YA SANLAM KATIKA UTOAJI WA BIMA KWA VIKUNDI TANZANIA

 



Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi limesaini hati ya Makubaliano ya Ushirikiano na kampuni ya Bima ya Sanlam katika utoaji wa Bima kwa vikundi Tanzania.

Tukio hili limefanyika Leo katika ukumbi uliopo ofisi za Baraza Kivukoni Daresalaam.

Tukio hilo limeshuhudiwa na wawakilishi wa Taasisi tofauti kama TIRA, TIMAP, IR-VICOBA pamoja na VICOBA FETA.

Kabla ya kusaini makubaliano hayo, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Bibi. Beng'i Issa alisema kuwa kuna faida kubwa ambayo vikundi vitaenda kunufaika kutokana na Bima hii.

Alisema kuwa SANLAM imeandaa bidhaa ya Bima ambayo itakuwa suluhisho na mkombozi kwa vikundi kwa kusudi la kutoa fidia/dhamana ya kifedha kwa wanachama na wanufaika wao.

Bima hii itahusisha utoaji wa kiasi cha Fedha kwa familia kama faraja baada ya kufariki kwa mshiriki wa kikundi au wanufaika wao. Aliongeza kuwa itasaidia kuleta ufanisi kwa wanakikundi ili waweze kufikia malengo waliyojiwekea.

Nae Afisa Mwendeshaji Mkuu wa Kampuni ya Sanlam Geofray Masige alimshukuru sana Katibu wa Baraza na jopo lake kwa kuwezesha pande zote mbili kufikia makubaliano hayo.

"Bima hii ya vikundi gharama yake itakuwa Shilingi elfu saba tuu kwa kila mwanakikundi kwa mwaka mzima. Gharama hii ni ndogo sana na imezingatia hali halisi ya kipato Cha Wajasiriamali wadogo katika ngazi ya vikundi." Aliongeza ndugu Masige.

Baada ya kusaini hati ya makubaliano, Katibu aliushukuru sana uongozi wa Sanlam kwa kuonesha nia ya dhati ya kuwagusa na kuwainua Watanzania wa chini.

"Nitoe wito kwa vikundi popote vilipo vichangamkie fursa hii kwani Bima ni dhamana bora na ya kisasa na inasaidia sana pale ambapo shida hutokea." Alisisitiza Katibu Mtendaji.

No comments