RC MAKONDA AONYESHA KIBURI,AWAGOMEA WABUNGE,SOMA HAPO KUJUA

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema
hawezi kufika mbele ya Kamati ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge kuhojiwa kwa
kuwa hajapokea barua ya kuitwa.
Makonda jana alisema hatoweza kwenda mbele ya kamati
hiyo bila barua rasmi iliyomtaka kufanya hivyo.
Bunge lililokuwa likiendelea na vikao vyake Dodoma
kabla ya kuahirishwa juzi, lilipitisha uamuzi wa kuwataka Makonda na Mkuu wa
Wilaya ya Arumeru, Alaxander Mnyeti, kufika mbele ya kamati hiyo na kuhojiwa
kutokana na kauli walizozitoa, zinazodaiwa kuudharau mhimili huo wa dola.
Lakini Makonda alisema jana “hilo suala la mimi
kuitwa kwenye kamati nalisikia na kulisoma kwenye magazeti."
"Sina uhakika ni lini wamefikia
uamuzi huu wa kuniita na hata kama wamefikia uamuzi huo, sijaletewa barua
rasmi.”
Baada ya Bunge kupitisha uamuzi huo wa kuitaka Ofisi
ya Bunge iwaandikie barua viongozi hao, juzi baadhi ya wabunge walihoji kauli
ya Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, kwamba azimio la chombo hicho cha
kutunga sheria kumtaka Makonda kufika mbele ya kamati kujieleza kuhusu tuhuma
za kuudharau mhimili huo, halikufuata utaratibu.
Hatua hiyo iliamsha hasira kwa baadhi ya Wabunge na
kuomba mwongozo kuhoji kwa nini Katibu wa Bunge ametoa kauli ambayo inakinzana
na makubaliano ya Bunge.
Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara na mwezake wa Iringa
Mjini Mchungaji Peter Msigwa (wote Chadema) walihoji kuhusu kauli ya Dk.
Kashililah.
Waitara alisema, “Asubuhi ya leo ( juzi)
nimetumiwa ‘clip’ ya sauti ya Katibu wa Bunge akikosoa uamuzi wetu hapa na pia
gazeti la Habari Leo, Ukurasa wa 25, kuna habari imeandikwa.
"Katika taarifa hii, Katibu wa
Bunge anasema maazimio ya Bunge yalikosewa na hayakufuata utaratibu,” alisema
na kuongeza kuwa: “ Kwa maana nyingine, hatatekeleza kile tulichokubaliana.”
Mchungaji Msigwa wakati akichangia taarifa ya Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, alieleza kuwa
hajafurahishwa na kauli ya Katibu wa Bunge.
Alisema Katibu wa Bunge amekosea kwenda katika
vyombo vya habari na kudai chombo hicho cha kutunga sheria kimekosea kwa kuwa
anafanya kazi ya Bunge na kwamba hajaajiri wabunge na anapaswa kufuata maagizo
yao.
Hoja ya kutaka kina Makonda washughulikiwe
iliwasilishwa na Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema) katikati ya wiki na
ilijadiliwa na kuungwa mkono na wabunge wote, wakiwamo mawaziri kwa kusema
‘ndiyo’.
Akiwasilisha hoja hiyo kipindi cha usiku baada ya
kipindi cha asubuhi kutoruhusiwa na Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge, Waitara
alisema: “Haya mambo ndiyo yamejirudia wakati nikiangalia televisheni ya
Clouds, Makonda akionekana akisema sisi humu bungeni tunasinzia.”
Alibainisha kuwa kwa mujibu wa Katiba ibara ya 63
(2), Bunge ndicho chombo kikuu kwa niaba ya wananchi katika kuisimamia na
kuishauri Serikali na linapitisha bajeti inayotumiwa na wateule hao wa Rais.
Alisema si sawa kwa wakuu wa mikoa na wilaya
kuwaweka rumande wabunge, madiwani na watumishi wa serikali.
“Bunge linaingia katika majaribu makubwa
ya kudharauliwa. Tunakula kiapo humu, tunaamua kwa niaba ya Watanzania, lakini
Mkuu wa Wilaya anasema hawa ni wapuuzi na Mkuu wa Mkoa anasema hawa wanalala
tu.”
Baada ya hoja hiyo, Waitara alitaka ijadiliwe na
Bunge na kutoa maazimio ili kurejesha heshima ya chombo hicho, hoja ambayo
Chenge aliipokea na kutoa nafasi kwa wabunge wanne kujadili kutokana na muda
kuwa mfupi.
Mbunge wa Ulyankulu (CCM), John Kadutu, alisema: “Nimehuzunika
sana wabunge tunafika mahali tunadharauliwa, halafu watu tunaangalia tu. Haya
ambayo yametokea kwa Makonda na Arumeru, pia yametokea Manispaa ya
Dodoma.Mkurugenzi anaongea na wabunge kama watoto.
“Nadhani hata ile sheria ya Marekani
wenzetu wanaoteuliwa kwa ngazi za juu lazima wapelekwe bungeni hapa kwetu
ingefaa kuletwa ili watu wa aina hii tuweze kuwamaliza hapa hapa.
"Wapo wanaodhani wako juu yetu.”
Alisema ni jambo la hatari kujenga serikali yenye
kiburi na kusisitiza “unapotaka kutoa pepo halibembelezwi. Unataka kupunga
majini huwezi kubembeleza.Lazima ukazane kupunga jini litoke. Hatuwezi kutoa
pepo kwa lugha nyepesi nyepesi (akipunguza sauti) pepo toka, haiwezekani. Kama
ni pepo tulikemee litoke.”
Ester Bulaya (Bunda Mjini–Chadema) alieleza Makonda
alivyompigia simu na kutamba kushughulikia wabunge kwa kuwa yuko karibu na
‘Bwana mkubwa’, huku akisisitiza kuwa Mkuu huyo wa Mkoa hakutengenezwa kuwa
kiongozi.
“Makonda alinipigia simu na kunitisha
kwamba yeye yuko karibu na Bwana mkubwa, atatushughulikia wabunge.
Alisema ataanza na (Joseph Kasheku)
Msukuma (Geita-CCM), Halima Mdee (Kawe-Chadema), Esther Matiko (Tarime
Mjini-Chadema), Sugu (Joseph Mbilinyi-Chadema Mbeya Mjini) na (Mchungaji Peter)
Msigwa (Iringa Mjini-Chadema),” alisema.
Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea alisema “Ni
lazima heshima ya Bunge ilindwe kwa gharama yoyote. Makonda anawapigia simu
wabunge akitaja mmoja wa mawaziri kuwa ndiye anatuma wabunge wamtukane.”
Naye Msukuma alisema haiwezekani Makonda afanye kazi
ya polisi na kuhoji aliko Mkuu wa Jeshi la Polisi, makamanda na makamishna
wake.
“Makonda ni nani katika hii nchi? Kama
(David) Jairo (aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini) alitoka
kwa azimio la Bunge, Makonda ni nani? Mimi niko tayari kupambana na Makonda,”
alisema Msukuma.
Hoja hiyo pia ilitolewa ufafanuzi na Mwanasheria
Mkuu wa Serikali, George Masaju na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera,
Uratibu na Bunge, Kazi, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, wakitaka
wahusika hao wasikilizwe kwanza na kuachia ngazi zingine iwapo watabainika
kutenda kosa.
Baada ya wabunge kuchangia, Chenge alitoa nafasi kwa
Waitara ambaye alihitimisha hoja hiyo na kutoa maazimio manne ambayo Mwenyekiti
huyo wa Bunge aliyafafanua na kupitishwa.
Maazimio hayo ni pamoja na Makonda na Mnyeti kuitwa
mbele ya Kamati ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge ili kuhojiwa juu ya kauli
zao zenye mwonekano wa udhalilishaji kwa Bunge, ambalo ni mhimili pacha na ule
wa utawala wanaoutumikia.
Lingine ni kumtaka Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene, kutoa
maelekezo kwa wakuu wa mikoa na wilaya kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na
kutoingilia majukumu yasiyowahusu.