RAIS MAGUFULI ATOA NENO TENA VITA DHIDI YA MADAWA YA KULEVYA,SOMA HAPO KUJUA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.
John Pombe Magufuli, ameviagiza vyombo vyote vya ulinzi na usalama kuongeza
nguvu katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwa kuhakikisha vinasimamia
sheria ipasavyo ili kukabiliana na tatizo hilo hapa nchini.
Mhe. Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo tarehe 12
Februari, 2017 Ikulu Jijini Dar es Salaam, muda mfupi baada ya kuwaapisha
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya Bw. Rogers
William Siyanga, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Peter Makakala, Balozi
wa Tanzania nchini Ubelgiji Mhe. Joseph Edward Sokoine, Balozi wa Tanzania
nchini Algeria Mhe. Omar Yusuf Mzee na Balozi wa Tanzania nchini Uganda Mhe.
Grace Aaron Mgovano.
Mhe. Dkt. Magufuli amewataka viongozi wote wa
Serikali kuungana na vyombo vya dola katika mapambano dhidi ya watu
wanaojihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya na ametaka mapambano hayo
yasifanywe kwa mzaha wala kwa kuangalia majina ya watu, vyeo vyao na taasisi
wanazoongoza.
Mhe. Rais Magufuli amewapongeza viongozi wote wa
mikoa walioanza kukamata watu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya na
amewaomba Watanzania wote waunge mkono juhudi za kukabiliana na wanaofanya
biashara na kutumia dawa za kulevya ambazo zinazidi kuangamiza nguvukazi ya
Taifa.
“Niwaombe ndugu zangu tuungane katika vita hii dhidi
ya dawa za kulevya, waandishi wa habari na wana mitandao tuweke mbele Utanzania
wetu, akitokea mtu anapambana na dawa za kulevya tumuunge mkono badala ya
kumchafua.
“Vita hii ni kubwa hatuwezi kwenda nayo kwa mzaha na
Serikali itahakikisha inasimamia sheria namba 5 ya mwaka 2015 iliyohusu kuzuia
na kupambana na dawa za kulevya ambayo ilitungwa na Bunge la 10 lililoongozwa
na Spika Anna Makinda na sheria hiyo ikatiwa saini na Rais Mstaafu wa Awamu ya
Nne Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, nawapongeza sana kwa kutunga sheria hii.”
Amesisitiza Mhe. Rais Magufuli
Pia, Mhe. Dkt. Magufuli amesema takwimu zinaonesha
kuna watanzania 1,007 wamekamatwa na kufungwa gerezani katika nchi mbalimbali
baada ya kupatikana na makosa ya kujihusisha na dawa za kulevya, na
amemuagiza Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na
Mabalozi wote wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi hizo kutojihusisha kuwatetea
waliofungwa kwa makosa hayo na badala yake waache sheria za nchi husika
zichukue mkondo wake.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amemtaka Kamishna
Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Peter Makakala kufanya mabadiliko makubwa ndani
ya Idara ya Uhamiaji nchini kutokana na utendaji wake kutoridhisha.
“Nataka ukafanye mabadiliko makubwa (Total Reform),
nataka Uhamiaji izalishe fedha kwa ajili ya nchi hii, nataka ukadhibiti utoaji
hati za kusafiria (Passports) maana zimekuwa zikitolewa hovyohovyo” amesisitiza
Mhe. Rais Magufuli.
Hafla ya kuapishwa kwa viongozi hao pamoja na kula
kiapo cha uadilifu kwa viongozi wa umma kilichoongozwa na Kamishna wa Maadili
Mhe. Jaji Mstaafu Harold Nsekela, imehudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia
Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, Kaimu Jaji Mkuu Mhe. Prof.
Ibrahim Juma, Mawaziri, Makatibu Wakuu wa Wizara mbalimbali na Wakuu wa vyombo
vya Ulinzi na Usalama.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
12 Februari, 2017