Zinazobamba

CHANGAMOTO YA MAKAZI UGHAIBUNI, IMEKUA FURSA.


Kutana na Heather Ngoda, mwenyekiti wa watanzania Diasporas nchini Mauritius, mjasiriamali wa Kitanzania na mwanzilishi wa kampuni ya Homefront Realty, inayojihusisha na biashara ya mali zisizohamishika yenye makao yake makuu nchini Mauritius.

Homefront imejipa jukumu la kuwahudumia wanafunzi wa Kiafrika na wageni kutoka nje ya Mauritius wanaohitaji makazi. 

Kampuni hiyo ilianza Aprili 2024, ambapo Heather amesaidia wageni tofauti ikiwemo wanafunzi wa kimataifa kutatua changamoto za kupata makazi katika kipindi chote wanachoishi kisiwani humo. 

Ndani ya kisiwa cha Mauritius Heather anadumisha uaminifu kwa dhamana aliyopewa na wageni kisiwani humo, kuhakikisha wanajisikia nyumbani katika nchi ya ugeni,kwa kuwapa makazi,kuwapa mbinu za kuishi kisiwani humo na kuwafungulia fursa mbalimbali wateja wake pale wanapohitaji msaada.

 Kupitia Homefront Realty, inawaweka Pamoja watanzania wanaoishi nchini Mauritius na raia wa mataifa mengine hususan mataifa ya Afrika.

Ndoto zake utotoni;

Ni kawaida kwa Watoto kutamani kazi ya kufanya atakapokuwa mkubwa. 

Wapo wanaotimiza ndoto zao na wapo ambao hukutana na matokeo tofauti na ndoto walizokuwa wakitamani kuwa. 

Kama ilivyo kwa Watoto wengine Heather akiwa binti mdogo alikuwa na ndoto tofauti tofauti mbali na biashara ya mali zisizohamishik
Kadri siku zilivyosonga fursa ya real estate ikaanza kujitokeza baada ya kupata nafasi ya kusoma ughaibuni.

‘‘Kusema kweli sikuwahi kufikiria biashara ya real estate tangu utotoni,nilikua na ndoto nyingi kama mtoto ila sio kwenye real estate, hata hivyo kila hatua ya maisha yangu ilikua inaniandaa kwenye hii nafasi,’’alisema Heather.

Safari yake katika sekta hii imekuwa mkombozi na mtatuzi wa changamoto, kuleta usawa na kufungua fursa kwa wageni wakiwemo watanzania wanaohamia nchini Mauritius. 

Kazi hii inafanyika kwa upendo na utu zaidi, jambo linalowapa furaha na faraja, wazazi wa watoto wanaokwenda masomoni nchini Mauritius,kwakuwa mwenyeji wa uhakika Homefront Realty yupo tayari kutoa huduma.

Alianzaje?!.

Heather ni miongoni mwa mabinti waliotumia changamoto walizopitia ugenini kuwa fursa binafsi na kuwanufaisha wengine pia. 

Alipokuwa masomoni nchini Mauritius, Heather aliiona changamoto ya upatikanaji wa makazi kwa wageni hasa waafrika.

 Akiwa miongoni mwa waliokabiliwa na changamoto hiyo,aliiona fursa ya kutatua changamoto ya upatikanaji wa makazi kwa wageni na kuichangamkia,na sasa ni mmiliki wa kampuni ya Homefront Realty akitendelea kutoa huduma za mali zisizohamishika,baada ya kuhitimu elimu ya chuo kikuu nchini Mauritius.

Heather ni msomi aliyehitimu shahada ya kwanza ya sheria kutoka Middlesex University nchini Mauritius.

Kitaaluma ni mwanasheria anaeitumia taaluma yake vizuri kuendesha biashara ya makazi kwa kuandaa mikataba rafiki na sheria za ardhi kimataifa.

‘‘Kuhitimu shahada ya sheria kumenipa msingi imara wa kuelewa sheria za ardhi, taratibu za mikataba na mahitaji ya kisheria katika sekta ya real estate na ujenzi kimataifa’’, alibainisha Heather.

Kupitia Homefront realty wanasaidia wawekezaji kupata ardhi na kuwapa muongozo wa kisheria, kuhakikisha uwekezaji wao unazingatia sheria zote za Mauritius na unalindwa ipasavyo.

 Katika kipindi cha mwaka mmoja, wamewezesha wawekezaji kutoka mataifa mbalimbali ikiwemo Afrika Mashariki na kuendelea kuimarisha ushirikiano wa Homefront Realty, Economic Development Board (EDB) na Mamlaka nyingine, kuhakikisha wateja wanaowahudumia wanapata huduma bora na salama za uwekezaji.

Heather alianza kazi hii ya mali zisizohamishika kupitia kampuni nyingine ya wazawa. 

Hapo alipata uzoefu wa kazi na kuona fursa ilipo hususan kuziba pengo la kutoa kipaumbele cha huduma ya makazi kwa wageni hasa waafrika.

Ushindani ugeninImemchukua miaka zaidi ya miwili kuaminiwa na wazawa wanaomiliki nyumba ambapo Heather huwatumia kuunganisha wateja wake wanapohitaji.

 Heather anaona uaminifu wake ni mtaji mkubwa wa kumpa nafasi ya kusonga mbele kutoa huduma ya makazi kwa wageni anaowapokea kisiwani humo. 

Wageni wengi kutoka mataifa mbalimbali sasa wanauhakika wa kuishi ugenini kama wapo nyumbani kupitia Homefront Realty.

‘‘Ushindani upo ila ni ushindani wa kawaida nikijilinganisha na real estates za wazawa yaan wenyeji wa Mauritius,kikubwa ninachojivunia nimejenga uaminifu kwa wenye nyumba na ninaendelea na mapambano,’’alisema Heather.

Kutokana na uaminifu huo Homefront Realty inahudumuia wageni,wazawa katika makundi mbalimbali ikiwemo wanafunzi. 

Kisiwa cha Mauritius kinapokea watalii wengi hivyo ni fursa pia ya kupokea wageni wengi zaidi kimataifa kwa kukodisha nyumba kwa wageni na kuuza nyumba kwa rai awa Mauritius.

Mafanikio katika kazi

Heather amepata mafanikio kadhaa ikiwemo kusaidia wanafunzi na wageni wakazi zaidi ya 200 ndani ya mwaka mmoja 2024-2025. 

Homefront Realty ni real estate pekee nchini Mauritius yenye mtazamo wa kiutu, ikisaidia waafrika wanaohamia kisiwani humo. 

‘‘Kwangu mimi kuwasaidia wageni kupata makazi ni fanikio kubwa sana hasa waafrika wenzangu ambao mara nyingi wanakutana na changamoto ya kupata makazi bora kwasababu kampuni nyingi zinatoa kipaumbele cha makazi kwa raia kutoka mataifa nje ya Afrika,kwahyo wazazi wengi wanafarijika kuona kuna mwafrika anaewapokea waafrika na kuwapa huduma kama wapo nyumbani,’’alisema Heather

Mafanikio mengine ni kuapata uaminifu kutoka kwa wenye nyumba ambao anashirikiana nao kuhakikisha wateja wake wanapata nyumba nzuri. Pamoja na hilo Heather anashirikiana na kampuni za wazawa katika biashara hiyo, jambo ambalo kwake ni mafanikio.

Pia Heather amepnua wigo wa huduma kupitia mitandao ya kijamii na kufanya wanaohitaji makazi kuwafikia kwa urahisi hususan wageni wanaoingia nchini Mauritius.

Matarajio yake

Heather anatarajia kuwa na jukwaa la kimataifa la kusaidia wanafunzi na wahamiaji waafrika kupata makazi kabla ya kuhamia kupitia mtandao, kwamaana ya kuwa na mtandao au ukurasa maalumu wa kutafuta nyumba.

‘‘Matarajio yangu hayako tuu kwenye kukuza biashara bali kwenye kuendeleza maisha ya watu, natamani kuona Homefront Realty ikiwa jukwaa la kimataifa la kusaidia wanafunzi na wahamiaji wa kiafrika kupata makazi,’’alisema Heather.

Umewahi kukutana na changamoto yoyote ile na ukaibadilisha kuwa fursa inayoacha alama kwa wengine?Au unapopitia changamoto unakosa mwelekeo na kuanza kulalamika! Badili mtazamo sasa. 

Huyu ndiye Heather Stephenson Ngoda, binti wa kitanzania aliyebadilisha changamoto kuwa fursa. Binti mwenye ndoto na maono makubwa ya ulimwengu wa real estate kimataifa,akiipeperusha vema bendera ya Tanzania katika visiwa vya Mauritius.

No comments