CHADEMA WAJILIPUA TENA LISSU AIENYESHA SERIKALI,SOMA HAPO KUJUA
TUMECHOKA kuvumilia! Ni kauli ya viongozi wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema) baada ya kudai kusakamwa na Serikali ya Rais
John Magufuli, anaandika
Pendo Omary.
Chama hicho kimetoa kauli hiyo
leo mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, baada ya Jaji Mstaafu,
Salome Kaganda ambaye ni Kamishna wa Maadili na Mtendaji Mkuu wa Sekretarieti
ya Maadili ya Viongozi wa Umma kuwaandikia barua viongozi wa chama hicho
akiwatuhumu “kukiuka masharti ya Hati ya Ahadi ya Uadilifu wa Viongozi wa
Umma.”
Jaji Kaganda aliwaandikia barua viongozi hao tarehe
4 mwezi huu ambapo Chadema wameitaka sekretarieti ya maadili ya viongozi wa
umma kuacha vitisho kwa viongozi wa chama hicho.
Walioandikiwa barua hiyo ni Freeman Mbowe Mwenyekiti
wa Chadema na Tundu Lissu, Mwanasheria Mkuu wa chama hicho.
Vincent Mashinji, Katibu Mkuu wa Chadema amesema,
kwa mujibu wa barua ya Jaji Kaganda, katika tarehe, muda na siku ambayo
haijulikani, viongozi hao wa Chadema walitoa matamshi ambayo yanachochea
wananchi kutotii sheria, kufanya vurugu, kudharau misingi ya demokrasia iliyopo
nchini na kutishia usalama wa nchi.
“Hata hivyo, Jaji Kaganda hakuyataja matamshi hayo
wala kuyafafanua. Aidha, alidai kwamba matamshi hayo yanatokana na maazimio
yaliyofikiwa na kikundi cha watu wachache nje ya Bunge,” amesema Dk. Mashinji.
Licha ya kudai kwamba, maazimio ya kikundi
hicho yanapuuza utangamano, utulivu na usalama wa wananchi wengine kinyume na
dhana ya maslahi mapana ya umma, Jaji Kaganda hakukitaja kikundi hicho cha watu
wachache nje ya bunge huku pia akidai matamshi ya viongozi hao yalilenga
‘kushamirisha ‘ maslahi yao binafsi na maslahi ya Chadema.
“Mheshimiwa Mbowe ni Mwenyekiti wa Taifa wa chama
kikuu cha upinzani hapa nchini. Ni kiongozi wa chama ambacho mgombea urais wake
alipata zaidi ya kura milioni sita kati ya kura 15 milioni zilizopigwa kwenye
uchaguzi mkuu wa urais mwaka jana.
“Ni mbunge wa kuchaguliwa na kiongozi wa Kambi Rasmi
ya Upinzani Katika Bunge. Ni mtu na kiongozi anayejulikana na kuheshimika ndani
na nje ya Tanzania. Kusema kuwa kiongozi huyo anaongoza kikundi cha watu
wachache nje ya Bunge kwenyewe ni kuonesha maadili yenye mashaka kwa mwandishi
wa barua hiyo,” amesema Dk. Mashinji.
Tundu Lissu, Mbunge wa Singida
Mashariki ameeleza kushangazwa na barua ya Jaji Kaganda akisema;
“Ni vigumu kuamini kwamba, barua hii imeandikwa na
mwanasheria na mtu ambaye amewahi kushikilia madaraka ya Jaji wa Mahakama Kuu
ya Tanzania.
“Barua ambayo haina maelezo yoyote ya kile
kinachodaiwa kuwa kosa; haitaji tarehe, siku, muda au mahali kosa hilo
lilipotendeka.
“Haitaji vifungu vya sheria yoyote iliyokiukwa na
wala kuonyesha kama sekretarieti ya maadili ya Viongozi wa Umma ina mamlaka
kisheria ya kushughulikia kosa hilo, in onyesha mapungufu makubwa ya kitaaluma
na kiuandishi ya kamishna wa maadili na katika mazingira ya kawaida,
ingestahili kupuuzwa,” amesema Lissu.
Kwa mujibu wa Lissu ambaye ni mwanasheria wa chama
hicho, Chadema haiwezi kuipuuza barua hiyo na kwamba, inaashiria kuwepo kwa
njama za kuwafungulia mashtaka katika Mahakama ya Maadili Viongozi hao ambao ni
wabunge kwa lengo la kuwavua ubunge.
Aidha, mojawapo ya vigezo vya kikatiba vya mtu
kukosa sifa ya kuwa mbunge ni pamoja na kuhukumiwa na kupewa adhabu ya kifungo
kwa kosa linaloambatana na utovu wa uaminifu au kwa kuvunja sheria ya maadili
ya viongozi wa umma.
Kwa mujibu wa sheria hiyo, kamishna wa maadili ana
mamlaka ya kuchunguza tuhuma za ukiukwaji wa maadili ya viongozi wa umma na
kuunda mahakama (Tribunal) ya kusikiliza tuhuma hizo na kupeleka taarifa ya
mashauri hayo kwa kamishna ambaye atapaswa kuwasilisha nakala za taarifa hiyo
kwa rais na spika wa Bunge.
“Rais Magufuli na washauri wake wanafahamu ugumu wa
kutumia mahakama za kawaida kwa lengo la kukandamiza wapinzani.
“Licha ya matatizo yake mengi, Mahakama ya Tanzania
imedhihirisha mara nyingi uwezo wa kulinda uhuru wake na kutokuwa tayari
kutumika kwa malengo ya kisiasa ya watawala.
“Sasa Magufuli (Rais John Magufuli) na washauri wake
wanaandaa mazingira ya kuitisha Mahakama ya Kangaroo watakayoidhibiti wao ili
kuhakikisha wanawakandamiza viongozi wakuu wa chama chetu.
“Kama ambavyo tumethibitisha mara kwa mara chama
chetu hakitakuwa tayari kuona viongozi wake wakikandamizwa kwa kutumia kivuli
cha maadili ya viongozi wa umma. Tutapambana na njama hizo. Kwa uthabiti na kwa
weledi ule ule ambao tumepambana na njama nyingine za aina hiyo katika siku za
nyuma,” ameeleza Lissu.
Aidha Jaji Kaganda amenukuliwa na gazeti la
Mwananchi la leo akikana kujua kuhusu barua hiyo huku akisema “mimi sifahamu
kuhusu suala hilo, sina taarifa.”