BAADA YA GAZETI LA MAWIO,WINGU LATANDA GAZETI LA MWANANCHI,POLISI YAINGILIA KATI,SOMA HAPO KUJUA
Jeshi la Polisi jana liliwahoji Mhariri Mtendaji wa
Mwananchi, Frank Sanga na mwandishi wa habari, Elias Msuya kuhusu makala
iliyochapishwa juzi kuhusu utendaji wa jeshi hilo.
Baada ya mahojiano yaliyofanyika kwa muda tofauti,
waliachiwa kwa dhamana na kutakiwa kuripoti kituoni hapo leo asubuhi.
Msuya ndiye aliyeanza kuhojiwa baada ya juzi jioni
kupigiwa simu na maofisa wa polisi akitakiwa kufika Kituo Kikuu cha Polisi
jijini Dar es Salaam kuhojiwa kutokana na makala yake ya uchambuzi yenye kichwa
cha habari “Polisi na hofu ya watawala kuondoka madarakani.”
Makala hayo yalichapishwa katika gazeti hilo toleo
la Julai 13 na mwandishi huyo alieleza mambo mbalimbali yanayohusu utendaji wa
jumla wa jeshi hilo kwa wananchi.
Baada ya kutoa maelezo kwa saa mbili, maofisa hao
walimpigia simu Sanga na kumtaka afike kituoni hapo kwa ajili ya kuhojiwa
kuhusu makala hiyo.
“Wamenihoji maswali mbalimbali kuhusiana
na makala niliyoandika. Nimewajibu kulingana na jinsi walivyokuwa wakiniuliza,” alisema
Msuya.
Msuya alifika katika kituo hicho saa moja asubuhi na
kukaa kwa saa mbili kabla ya kuanza kuhojiwa na kisha Sanga ambaye alifika
kituoni hapo mchana na kuhojiwa kwa dakika 90.
Akizungumzia suala hilo, Mhariri Mtendaji Mkuu wa
Mwananchi Communications Ltd (MCL), Bakari Machumu alisema baada ya wito huo wa
polisi, kampuni imetoa ushirikiano wa kutosha kwa kuwaruhusu Sanga na Msuya
kwenda kutoa maelezo polisi.
Alisema ni vyema masuala yanayohusu habari ambazo
zinatakiwa kutolewa ufafanuzi yakaihusisha Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa
na Michezo na Baraza la Habari Tanzania (MCT).
“Nadhani jambo kama hili kuchukuliwa
moja kwa moja na polisi ni kama kuingilia uhuru wa habari. Vipo vyombo
vinavyoweza kutoa ufafanuzi wa habari iliyoripotiwa na vyombo vya habari,” alisema
Machumu.
Baada ya mahojiano hayo, Sanga na Msuya waliachiwa
kwa kila mmoja kudhaminiwa na mtu mmoja.