MABASI ZAIDI YA 150 YA MOFAT YAMEPAKIWA
Mabasi zaidi ya 150 ya mwendokasi ya kampuni ya Mofat tangu yamenunuliwa yamepakiwa kutokana na kukosa nafasi ya utoaji wa huduma ya usafiri katika baadhi ya maeneo.
Taarifa hiyo imetolewa leo Mei 6, 2026 na Mkurugenzi Mtendaji wa kituo cha ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi (PPC), David Kafulila, alipofanya ziara ya kutembelea kampuni ya mabasi ya mwendokasi ya Mofat ili kujionea changamoto mbalimbali inazokumbana nazo.
Kafulila amesema kuwa kampuni hiyo kwa sasa inatumia mabasi 50 pekee kwa njia ya Mbagala, lakini mabasi mengine ambayo ni mapya na yamelipiwa bima yamepakiwa, hali ambayo inasababisha hasara kwa kampuni hiyo ya kizalendo.
"Huu ni uwekezaji unaohusisha mabenki. Kampuni imepaki mabasi mapya takribani nusu mwaka sasa. Hivyo binafsi kama Mkurugenzi ambaye wajibu wangu ni kuhakikisha miradi hii inakuwa endelevu, tumekubaliana kwamba waandae ripoti ya tathmini ya nusu mwaka ili kusudi iweze kutumiwa na Serikali kwenye vikao vya ngazi ya juu,
hususan kamati ya uendeshaji wa masuala ya ubia, kutathmini na kuona namna gani marekebisho kadhaa yanaweza kufanyika ili mradi huu uweze kuwa endelevu na uwekezaji huu uwe wa mfano na usilete changamoto kwa mwekezaji mwenyewe na wawekezaji wengine watakaopenda kuuona kama mfano," amesema.
Aidha, Kafulila amemaliza kwa kusema kuwa kwa sasa Dar es Salaam ina ziada ya mabasi ya mwendokasi tofauti na hapo awali ambapo kulikuwa hakuna mabasi ya ziada.
Kwa upande wake, msemaji wa kampuni hiyo ya Mofat, Philip Changala, amesema kwamba kwa sasa kampuni hiyo itaendelea kutoa huduma kwa manufaa ya wananchi katika eneo wanalotoa huduma la Mbagala, Kivukoni, Gerezani na Ilala Boma.
Aidha, amesema kwamba huduma zinazotolewa na kampuni ya Mofat zinasimamiwa na DART.
"Ziara ya PPC kutembelea mradi huu inaonesha ushirikiano mzuri kati ya Serikali na wawekezaji binafsi, na namna gani Serikali ipo tayari kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji binafsi pamoja na kusikiliza changamoto wanazozipata katika utoaji wa huduma za usafirishaji," amesema Changala.

No comments
Post a Comment