MAKONDA AANZA 'KUVIMBA KICHWA" AWATOLEA MANENO YA MIPASHO UKAWA,SOMA HAPO KUJUA

PAUL Makonda,
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ameanza kutoa kauli za mipasho dhidi ya vyama
vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), anaandika Regina Mkonde.
Akizungumza na Umoja wa Vijana Waendesha
Bodaboda wa Mkoa wa Dar es Salaam katika Viwanja vya Leaders Club jijini humo
leo, Makonda amesema wapinzani wataishia kuchongwa, na kwamba, mamlaka ya jiji
hilo yapo mikononi mwake.
Kauli yake inafanana na iliyotolewa na Said Meck Sadick,
aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam wakati akikabidhi ofisi hiyo siku
chache zilizopita.
Makonda ametoa kauli hiyo siku tatu baada ya Isaya Mwita, Meya
wa Jiji la Dar es Salaam, kutangazia umma kwamba licha ya uanachama wake wa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), atafanya kazi bila kujali itikadi
za vyama vya siasa.
“Mamlaka ya uamuzi ya utendaji kazi Mkoa wa Dar es Salaam yako
mikononi mwangu. Wengine wataishia kusema wee, lakini mwenye mamlaka ya mwisho
katika uamuzi ni mimi,” alitamba Makonda.
Kauli hiyo ya Makonda ni muendelezo wa mikogo yake dhidi ya
UKAWA ambao tayari wameonesha dhamira ya kuachana na migogoro ya kisiasa ili
kuhudumia wananchi.
“Msiwe kama baadhi ya viongozi wa waendesha bodaboda wanaofuata
wanasiasa na kuwatajia idadi ya wanachama wanaowamiliki ili wapate hela na
kutumikishwa kisiasa ili wafanye fujo halafu waanze kusema, serikali haifanyi
kitu, haithamini wananchi wake na mambo mengine ya kisiasa,” Makonda aliwaambia
bodaboda hao.
Aidha, ametoa maagizo kwa Simon Sirro, Kamanda Mkuu wa Polisi
Kanda Maalumu ya Dar es Salaam akimtaka ashughulikie matatizo ya waendesha
bodaboda.
“Ndani ya siku 90 kabla ya kupatikana kwa Kamati ya Kudumu ya
Umoja wa Waendesha Bodaboda, nakuagiza Sirro ukawaambie polisi wako waache
kuingilia matatizo ya waendesha bodaboda, bali polisi wawe washauri wa shughuli
zinazofanywa nao,” amesema.
Makonda ametaja takwimu za ajali na vifo vilivyosababishwa na
bodaboda katika Mkoa wa Dar es Salaam mwaka 2015. Takwimu hiyo inaonesha kutokea
kwa ajali zaidi ya 1000 na vifo 100.
“Katika Wilaya ya Ilala, ajali zilizotokea ni 486, vifo 34,
Temeke 542, vifo 31 na Kinondoni ajali 170 na vifo 36,” amesema.
Daud Laurian, Katibu wa Kamati iliyomaliza muda wake, wakati
akisoma risala, amemtaka Makonda kushughulikia baadhi ya wajumbe wa Saccos ya
umoja huo (DABOSA) kwa kosa la kufanya ubadhilifu wa fedha zao kiasi cha Sh 50
milioni.
“Tunakuomba Mkuu wa Mkoa Paul Makonda, uwatumbue baadhi ya
viongozi wa Saccos yetu ambao wamefuja fedha zetu shilingi milioni 50 kwa
manufaa yao binafsi,” amesema Laurian.
No comments
Post a Comment