MATAIFA YA ULAYA YAMCHAKAZA MAGUFULI,WASOMI WAMTABILIA MABAYA UTAWALA WAKE,KIBAMBA ASEMA UROHO WA MADARAKA WA CCM KUWALAZA NJAA WATANZANIA,SOMA HAPO KUJUA
![]() |
| Balozi Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa |
UAMUZI wa mataifa 11 yenye uanachama wa Jumuiya ya
Ulaya (EU) kusitisha kuchangia Bajeti Kuu ya Tanzania,sasa uamuzi
huo unatajwa kuliweka Taifa
pabaya.Mtandao huu umeelezwa.Anaandika KAROLI VINSENT endelea nayo.
Hali hiyo imekolezwa zaidi na
uamuzi huo wa sasa wa mataifa hayo 11 ambao ulitanguliwa na ule wa Serikali ya Marekani
kupitia Shirika lake Changamoto za Milenia (MCC) kusitisha msaada wa zaidi ya
shilingi trilioni moja zilizokuwa ziende kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo.
Akizunguma na Mtandao huu kwa sharti la kutotaja
jina lake mtandaoni,Kigogo mmoja mwandamizi aliyoko ndani ya wizara ya
Fedha,amesema kwa sasa Taifa linapitia kipindi kigumu ambacho anakifananisha na
kipindi cha miaka 1980 ambapo nchi ilikuwa kwenye hali mbaya ya kiuchumi.
“Sikiliza ndugu mimi mtaalamu wa haya masuala ya
uchumi,wanaokwambia kwamba watajiendesha nchi bila kutegemea misaada
wanajidanganya nafsi zao,huwezi ukaendesha taifa kubwa kama hili ukategemea
mapato ya Pombe na Sigara,huu ni uwongo wa mchana kweupe”amesema mtoa taarifa
wetu huyu.
Kuhusu mapato ya kodi ya mwezi ambayo serikali ya
Chama cha Mapinduzi CCM wamekuwa wakitumia hoja hiyo kudai kuwa kwa sasa
wanaweza kujiendesha wenyewe,
Kigogo huyu amepinga hoja hiyo kwa kusema kinachoitwa
makusanyo makubwa ya serikali,kwa kudai kuwa asilimia kubwa ya mapato hayo yanaishia kwenye
kujilipa mishahara.
“Nakuapia kabisa ndugu,mapato yanayokusanywa na
serikali asilimia kubwa yanaishia kwenye kujilipa mishahara ambapo kiasi
kinachobakia kidogo kinalipa madeni ya ndani na ya nje ambayo ni mkubwa harafu wanachokilipa hakiwezi kufua
dafu deni ni kubwa mno, harafu kingine kinaelekezwa kwenye elimu bure na kiasi
kidogo ndio kinakwenda kwenye hiyo miradi ya maendeleo tena hakifiki hata
bilioni 100,sasa utajiendesha vipi bila wahisani,waulizeni hao wanaowadanganya”amefafanua
“Ninachokwambia sasa watanzania wategemee hali mbaya
sana ya nchi,yaani kama mtu uliokuwa unakula milo mitatu basi sahivi utakula
milo miwili,kama ni mmoja basi upo katika hali mbaya ya kutokula kabisa,yote
haya yanatoka na ulafi tu wa madaraka unaofanywa na viongozi wa CCM”
WACHUMI NAO
WANENA.
Wakizungumza na Chanzo changu yaani (Gazeti la Mtanzania )wachumi mbalimbali
wametoa yamoyoni huku wakitoa tahadhari kubwa kwa Rais John Magufuli.
wabobezi wa masuala ya uchumi wanabashiri hatua hiyo
huenda ikasababisha mtikisiko wa uchumi katika siku chache zijazo ambao pamoja
na mambo mengine utailazimisha Serikali au Taifa kwa ujumla kufunga mkanda.
Wachumi hao wanasema endapo Serikali haitaamua
kuchukua hatua ya kukabiliana na hali hiyo matokeo ya uamuzi huo yataonekana
katika bajeti kuu ya mwaka 2016/17 na watakaoathirika zaidi ni Watanzania wa
kawaida.
Mtaalamu wa uchumi na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha
Mzumbe, Profesa Honest Ngowi, amesema uamuzi wa MCC na ule wa mataifa 11
kuondoa msaada wao kwenye Bajeti Kuu ya Serikali utaathiri kwa kiasi kikubwa
mipango ya maendeleo ya nchi.
Prof. Ngowi amesema athari za kukosekana kwa misaada
hiyo zinaweza zikawagusa na zisiwaumize watawala lakini zikawaumiza zaidi
wananchi wa kawaida wenye uhitaji wa kujinasua kwenye umasikini na kujiendeleza
kiuchumi.
Kwa mujibu wa Prof. Ngowi, ingawa fedha za msaada wa
MCC zinatafsiriwa na baadhi ya wanasiasa kwamba ni ndogo, lakini malengo ya
ufadhili wake yangesaidia kuinua uchumi wa wananchi wengi.
“Nadhani hili jambo litaakisi ama kuonekana katika
bajeti kuu ijayo, mataifa haya 11 kuondoa ufadhili wao katika Bajeti Kuu ya
Serikali, itailazimu Serikali itafute fedha za kufidia pengo,” alisema Profesa
Ngowi.
Alisema ili Serikali ifidie pengo hilo itahitaji
mambo matatu ambayo ni kukopa, kupandisha kodi au kuongeza vyanzo vingine vya
mapato.
“Maswali ya kujiuliza, kama Serikali itakopa ina
maana lazima itafute fedha za kurejesha mkopo, kama Serikali itapandisha kodi
ina maana itawaumiza tena wananchi wake ambao wanakabiliwa na utitiri wa kodi
na kama itaongeza vyanzo vipya vya mapato, je, ina muda wa kutosha wa kupata
fedha ya kuziba pengo la wafadhili katika bajeti kuu? alihoji Profesa Ngowi.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti ya
Kupunguza Umasikini (REPOA), Profesa Samweli Wangwe, amesema wafadhili kuondoa
misaada yao katika Bajeti Kuu ya Serikali na miradi ya maendeleo ni pigo kwa
uchumi wa nchi.
Alisema pamoja na pigo kutokea Serikali inabidi
iweke mpango mkakati wa kukabiliana na pigo hilo kwa kupunguza matumizi yake
yasiyokuwa na ulazima.
“Si vyema sana kusifu ukubwa wa kiasi walichokuwa
watufadhili… Ingawa ni kweli walikuwa wanachangia fedha nyingi kwa ajili ya
maendeleo ya nchi. Inabidi kufanyike utafiti wa kufahamu ni kiasi gani
walifadhili nchini na kiasi gani wamekirejesha kwao kupitia taasisi na kampuni
zao zinazofanya kazi hapa nchini,” alisema Profesa Wangwe.
Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba (Jukata), Deus
Kibamba, alisema kuondolewa kwa misaada hiyo ni mtihani mkubwa kwa Taifa.
Alisema kabla ya wahisani kuondoa misaada yao
kulikuwapo dalili zilizoashiria mwenendo wa Serikali katika kusimamia
demokrasia hauwapendezi na walionya mara kwa mara lakini Serikali haikusikia.
Kibamba aliongeza kuwa kitendo cha wafadhili kuondoa
misaada yao kinamaanisha kuwa miradi ya maendeleo itakwama na matokeo yake
kuwaumiza wananchi.
Alisema kuondolewa kwa misaada hiyo kunaiumiza nchi
hususani wananchi masikini, kwamba watawala wanaweza wasiugulie maumivu kwa
sababu wao wana akiba tofauti na mwananchi wa kawaida.
“Nawashangaa wanaosema eti tutajitegemea na hatuwezi
kuwapigia magoti wafadhili, kweli ni hoja lakini Tanzania imefikia kiwango
hicho wanachokifikiria? Kwanza hapa si kwamba tunawapigia magoti wafadhili bali
itabidi tupigiane magoti wenyewe kwa sababu tumekoseana kwa kukiuka misingi ya
demokrasia, huko Zanzibar jamii imepasuka vipande viwili….Sawa wafadhili
hawatakiwi kuingilia mambo ya ndani ya nchi lakini je, wataendelea kufadhili
watu waliokosana kutokana na kukiukwa kwa misingi ya demokrasia?
“Hata hili la kukosa msaada wa fedha za MCC huo ni
mradi mmoja tu miongoni mwa miradi mingi inayofadhiliwa na Serikali ya Marekani
hapa nchini, tujiulize itakuwaje kama ikifunga na hiyo miradi mingine?,”
alisema Kibamba.
Katika hatua nyingine gazeti hili lilimtafuta Rais
wa Mahakama ya Afrika, Jaji Mkuu mstaafu, Augustino Ramadhani, ili kufahamu
mtazamo kuhusiana na uamuzi huo wa baadhi ya nchi za Magharibi ambapo alikataa
kuzungumza chochote kwa hofu ya kugombana na wanasiasa.
“Siwezi kuzungumza lolote kuhusu jambo hilo,
niulizeni mambo ya kisheria katika Mahakama ya Afrika, lakini hayo mambo
siwezi kabisa kuyasemea, nitajikuta nagombana bure na wanasiasa,” alisema Jaji
Ramadhani.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya
Mwalimu Nyerere (MNF), Joseph Butiku, alisema jambo hilo ni kubwa na kutaka
liachwe kwa Serikali yenyewe.
“Hapana haya mambo ya dunia ni makubwa na unaweza
kuzungumza chochote ukajikuta unachonganisha mataifa, unajua mambo haya yana
siasa nyingi nadhani ni bora tukaiachia Serikali ikatafuta ufumbuzi wa jambo
hili,” alisema Butiku.
Ikumbukwe wakati wa sakata la kashfa ya Escrow,
Serikali ya Uingereza ilipunguza msaada wake wa kuchangia bajeti kuu ya
Serikali kwa asilimia 12.

No comments
Post a Comment