Zinazobamba

UMMY MWALIMU AIKABA KOO MSD, AMEWATAKLA KUJENGA DUKA LA DAWA KILA HOSPITALI YA MKOA HAPA NCHINI




WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummi Mwalimu ameiagiza Bohari Kuu ya Dawa nchini (MSD) kujenga maduka ya dawa katika kila Hospitali ya mkoa hapa nchini kabla ya Mei na Juni mwaka huu.

Kauli ameitoa jana wakati wa ufunguzi wa duka la dawa katika Hospitali ya Mkoa wa Mwanza ya Sekou Toure, ambako amesema MSD wanapaswa kujenga maduka ya dawa katika kila hospitali ya mkoa nchini ili kukabiliana na uhaba wa dawa.

Amesema MSD wanapaswa kutambua kwamba suala la afya ndio kipaumbele kikubwa katika wizara ya afya hivyo lazima juhudi za upatikanaji wa dawa zifanyike kwa nguvu zote, kwani tatizo la dawa limekuwa ni sugu nchini.

Waziri Ummy amesema kuwa hata kama hawashindwa kujenga kila mkoa angalau wanapaswa kufikisha asilimia 50 ya ujenzi wa maduka katika baadhi ya mikoa ili kabla ya bunge la bajeti la Juni awe amepata cha kuzungumza bungeni.

Hata hivyo amesema wizara ya afya imejiwekea malengo ya upatikanaji wa dawa nchini kutoka asilimia 70 ya sasa hadi 95 na kwamba kama hatatatua tatizo la dawa katika hospitali za Serikali yupo tayari kuwajibishwa.

“Nilishajihukumu mwenyewe kwamba kama sitaweza kutatua suala la dawa hospitalini nipo tayari kuwajibishwa na hilo sikusubiri Rais (John Magufuli) aniambie nilijihukumu mimi mwenyewe na sasa nipo tayari kuwajibika.

“Pia unakuta mgonjwa anakaa saa sita hospitalini kumsubiri daktari akishamuona daktari na unapofika muda wa anakuta dawa hakuna, ni bora akae saa sita kumsubiri mganga alafu akapata dawa na hilo ndilo lengo letu,” amesema Ummy.

Mkurugenzi wa MSD, Laulean Kunu, amesema kuwa agizo la waziri huyo litafanyiwa kazi kwani mpaka sasa tayari wameishajenga maduka mengine mawili katika mikoa ya Mbeya na Arusha na katika kila duka la MSD dawa aina zote zitapatikana.

“Mikoa mingine iliyobaki sasa hivi tupo katika mazungumzo na viongozi wa mikoa hiyo na MSD tupo tayari kupeleka dawa aina zote katika maduka ili kuondokana na tatizo la uhaba wa dawa katika hospitali za Serikali,” amesema Kunu.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo, amesema kujengwa kwa duka hilo litahudumia zaidi ya asilimia 30 ya vituo vya afya 373 na zahanati 321 na hivyo kujengwa kwake kutapunguza tatizo la upatikanaji wa dawa.

Hakuna maoni