SAKATA LA KURUDIWA UCHAGUZI ZANZIBAR,CUF KUKUTANA KUJIBU MAPIGO,SOMA HAPO KUJUA
CHAMA cha
Wananchi CUF kinatarajia kimeitisha vikao vya juu vya kitaifa vya Chama ili
kujadili marudio ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar uliotangazwa kurudiwa Machi 20,
2016 na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar.
Katika taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi
wa Habari na Mawasiliano wa CUF, Ismail Jussa, imesema kuwa vikao hivyo
vitafanyika Januari 27 na 28 mwaka huu, na ndiyo vitakavyotoa msimamo rasmi wa
CUF.
Ifuatayo ni
taarifa kamili ya Jussa.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Kufuatia tangazo jengine la kihuni lisilozingatia Katiba wala
Sheria la Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) Jecha Salim Jecha
kutangaza tarehe 20 Machi, 2016 kwamba ni siku ya kile anachokiita uchaguzi wa
marudio Zanzibar, Chama Cha Wananchi (CUF) kimeitisha vikao vya juu vya kitaifa
vya Chama ili kujadili suala hilo na kutoa msimamo rasmi wa Chama.
Kamati ya Utendaji ya Taifa itakutana Jumatano, tarehe 27
Januari, 2016 na kufuatiwa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa litakalokutana
Alhamis, tarehe 28 Januari, 2016. Vikao hivyo vitafanyika Ofisi Kuu ya Chama,
mjini Dar es Salaam.
Chama kinatoa wito na kuwanasihi Wazanzibari wote waliochoshwa
na utawala wa kibabe na wa kidikteta wa CCM na ambao walikikataa chama hicho
kwa kishindo tarehe 25 Oktoba, 2015 kuendelea kutunza amani na kuwa watulivu
katika kipindi hiki kigumu na kusubiri maamuzi ya chama chao wanachokiamini.
HAKI SAWA KWA WOTE
ISMAIL JUSSA
KAIMU MKURUGENZI WA HABARI NA
MAWASILIANO
Hakuna maoni
Chapisha Maoni