KAMANDA KOVA AJIPANGA KUPAMBANA NA WAHARIFU SIKU YA MKESHA WA MWAKA MPYA,SOMA HAPO KUJUA
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NDANI
JESHI LA POLISI TANZANIA
28/12/2015
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
JESHI
LA POLISI KANDA MAALUM LIMEJIPANGA UPYA KUHAKIKISHA USALAMA KATIKA MKESHA WA
MWAKA MPYA BAADA YA SHEREHE ZA MAULID NA KRISMAS KUMALIZIKA SALAMA
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es
Salaam limeweka mikakati ya hali ya juu kuhakikisha kwamba wakati wa mkesha wa
Mwaka Mpya hali ya usalama inakuwa shwari. Katika mkakati huo vikosi vyote vya
Polisi ikiwa ni pamoja na askari unifomu (GD), FFU, wanamaji, kikosi cha Mbwa
na Farasi, askari kanzu, na wengine. Aidha, kikosi cha Polisi Anga kitafanya
doria kwa kutumia helkopta ya Polisi. askari wa doria ya pikipiki watakuwepo
barabarani wakifanya doria.
Pia tumekusudia kushirikisha wadau wengine wa ulinzi na usalama
ikiwa ni pamoja na Jeshi la Zimamoto, kampuni binafsi za ulinzi, wadau
wanaohusika na uokoaji wakati wa majanga,
vikundi vya ulinzi shirikishi pamoja na kamati za ulinzi na usalama ngazi zote jijini Dar es
Salaam. Aidha, wakaguzi wa Tarafa na askari Kata watashiriki kikamilifu kuhakikisha maeneo
yote yanalindwa masaa 24.
Sambamba na hatua hizo, vikosi vyote vya Polisi vitakuwa barabarani
masaa sita kabla ya mwaka Mpya vikifanya doria.
Fukwe zote za bahari na maeneo yote yenye mikusanyiko yatalindwa kwa
kuweka vituo vya polisi vya muda vinavyohamishika (Mobile Police Station). Pia
askari wa kutosha watakuwepo kuhakikisha wananchi wanasherehekea kwa
amani.
Wakati wa mkesha huo nyumba zote za ibada zitalindwa hivyo wananchi
wasiwe na hofu yoyote juu ya usalama wao kwa kuwa Jeshi la Polisi lipo imara.
Hata hivyo wananchi wanatakiwa kuchukua tahadhari za kiusalama kwa kutoa
taarifa kwa hali yoyote inayotia shaka.
Wananchi wanashauriwa kusherehekea siku ya Mwaka Mpya katika ngazi
ya familia au kukusanyika katika mitaa kwa amani wakisherehekea.
Aidha, wafanyabiashara mbalimbali hasa wa
maduka ya kubadilishia fedha (Bureau De Change), na wale wenye maduka makubwa
wanatakiwa kuchukua tahadhari kwa kutosafirisha pesa nyingi kwa njia za
kawaida. Wanashauriwa kusafirisha pesa hizo kwa njia za kietroniki na nyingine
kama hizo. Pia wanashauriwa kuomba ulinzi wa Polisi kama kuna ulazima wa
kufanya hivyo ili kuepuka kuvamiwa na watu wenye nia mbaya.
Madereva wanatakiwa kuzingatia sheria za usalama barabarani ikiwa ni
pamoja na kutoendesha vyombo vya moto kwa mwendo kasi, na kutokuwa walevi.
Wananchi wanapoona dalili zozote au maandalizi ya uvunjifu wa amani
watoe taarifa haraka na mapema iwezekanavyo katika vituo vya Polisi vya karibu
ili hatua zichukuliwe kwa haraka.
Watu wajiepushe ma ulevi wa kupindukia au kupiga risasi za moto kama
sehemu ya sherehe hiyo.
Upigaji wa fataki na flash flash haziruhusiwi katika usiku wa mkesha
wa Mwaka Mpya.
Atakayekaidi atakachukuliwa hatua pao kwa papo kutokana na mtandao
madhubuti wa vyombo vya usalama ikiwa ni pamoja na askari makachero watakaokuwa
doria kila mahali.
TATHMINI YA
UHALIFU WAKATI WA SIKUKUU YA MAULID NA KRISMAS
Kwa ujumla hali ya ulinzi na usalama katika jiji la Dar es Salaam wakati
wa sikukuu za Maulid na Krismas ilikuwa shwari. Hapakuwa na matukio makubwa ya
uhalifu katika siku hizo mbili licha ya makosa madogo yaliyoripotiwa kati ya
tarehe 25/12/2015 hadi 27/12/2015.
Aidha, Jeshi la
Polisi limefanikiwa kukamata Bastola moja aina ya RIVOLVER yenye namba 801340
rangi nyeusi iliyotengenezwa nchini Brazil ikiwa na risasi mbili. Tukio hili
limetokea tarehe 24/12/2015 maeneo ya Ubungo Kibo wakati askari wa upelelezi
wakiwa wanafuatilia matukio ya uhalifu waliwatilia shaka watu watatu na
kuwafuatilia kisha kuwakamata.
Baada ya
mahojiano walikiri kumiliki bastola hiyo ambayo ilikuwa imefichwa dukani kwa
PETER S/O MASSAWE, Miaka 25, mkazi wa Rombo Kibo jijini Dar es Salaam. Wengine
waliokamatwa ni kama ifuatavyo:
·
MATOLA S/O RASHIDI
@ Carlos, Miaka 30, Mkazi wa Kimara Baruti
·
ISMAIL
S/O OMAR, Miaka 29, Mkazi wa Kimara Baruti
Jumla ya watuhumiwa 71
wamekamatwa kwa tuhuma za makosa mbalimbali yakiwemo ya kubugudhi abiria,
kupika na kuuza pombe haramu ya moshi (gongo), kuuza na kuvuta bhangi, kupiga
debe, na makosa mengine. Aidha umekamatwa mtambo mmoja wa kutengeneza gongo, kete 236 na misokoto 174 za bhangi pamoja na lita 50 za gongo.
Tunawaomba wananchi waendelee kulisaidia Jeshi la Polisi katika
kukabiliana na uhalifu katika jiji la hasa tunapouaga mwaka 2015 na
kuukaribisha mwaka 2016
SULEIMAN
H. KOVA – CP
KAMISHNA
WA POLISI KANDA MAALUM
DAR
ES SALAAM.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni