Zinazobamba

WABUNGE WAMNANGA KIKWETE,NI KUHUSU RIPOTI YA TOKOMEZA,SOMA HAPO KUJUA

Baadhi ya athari za Operesheni Tokomeza, askari wakiwadhibu raia
Baadhi ya athari za Operesheni Tokomeza, askari wakiwadhibu raia

BUNGE limeitaka Serikali iweke hadharani ripoti ya Tume ya kimahakama iliyoundwa na Rais Jakaya Kikwete kuchunguza kilichojiri wakati wa Operesheni Tokomeza. Anaandika Dany Tibason …(endelea).
       Akiwasilisha maoni na mapendekezo ya Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira kwa mwaka wa fedha wa 2015/16, Mwenyekiti wa kamati hiyo, James Lembeli, amesema “ripoti hiyo tayari imekabidhiwa kwa Rais na baadhi ya matokeo yake yametangazwa ikiwa ni pamoja na kuwasafisha mawaziri waliojiuzulu kwa kashfa hiyo.”
       Amesema kuwa taarifa hiyo imewapa maswali makubwa wananchi kwa kuwa ripoti ya kamati ya Bunge iliyochunguza sakata hilo haikuwatia hatiani mawaziri hao bali waliwajibika kwa makosa yaliyofanywa na maofisa waliokuwa wanawasimamia.
       “Serikali iweke hadharani ili ripoti iseme ni nini kuhusu wananchi waliuawa, kuteswa, kuporwa mifugo yao au mifugo hiyo kupigwa risasi. Ni busara kwa serikali kuweka hadharani ripoti hiyo ili Watanzania waamini kama haki imetendeka,” amesema.
      Lembeli amefafanua kuwa, kamati yake ilikutana mara mbili na kushindwa kujadili taarifa ya Wizara ya Maliasili na Utalii baada ya kubaini kuwa wizara haikuwa imetekeleza ushauri wa kamati kuhusu masuala yenye manufaa kwa taifa na haikuweza kutoa sababu za msingi za kutokutekeleza ushauri huo.
         Pia, amemlalamikia Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu kuwa amekuwa akikiuka ushauri wao, kwamba kamati ilishauri na Bunge likaridhia kwamba mfumo wa ungiaji wa wageni hifadhini wa mara moja (Single Entry) uendelee kutumika katika hifadhi za Taifa na Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro.
            “Kinyume chake, wizara iliagiza kutumika kwa mfumo wa uingiaji wa wageni hifadhini zaidi ya mara moja (Double Entry), hivyo basi hizo taasisi mbili kupoteza mapato makubwa. Kamati inajiuliza uamuzi huo wa wizara ni kwa manufaa ya nani,” amehoji.
        Amesema kutokana na hali hiyo, takwimu zinaonesha kwa kipindi cha miezi kumi yaani Julai 2014 hadi Machi 2015, hifadhi ya Serengeti na hifadhi ya Ziwa Manyara zilipoteza zaidi ya Sh.1.4 biloni.
        Lembeli ameongeza kuwa wizara kulazimisha mfumo wa uingiaji wa wageni hifadhini zaidi ya mara moja, kamati inahoji kuna maslahi gani waziri kutetea mfumo ambao unaipotezea serikali mapato.
      Amefafanua kuwa kamati pamoja na Bunge walishauri waziri atekeleze hukumu ya Mahakama kuu kanda ya Arusha iliyomtaka kutangaza katika gazeti la Serikali tozo mpya zitakazotumika katika mahoteli yaliyo ndani ya hifadhi ya Ngorongoro ili zianze kutumika mara moja.
Kwamba, kutokana na ucheleweshwaji wa kutumika kwa tozo mpya kama ilivyoamriwa na mahakama, Serikali imepoteza Sh. 3 bilioni hadi kufikia 15 Machi mwaka huu.
         “Kutokana na hali hiyo, kamati inamtaka waziri kulieleza Bunge ni nini kilimfanya akaidi kutekeleza hukumu iliyokuwa na maslahi kwa taifa. Kamati inashangazwa na hali ya serikali kulalamika kuwa makusanyo yake ya ndani ni madogo wakati serikali hiyo hiyo inafanya vitendo vya kujikosesha mapato,” amehoji.     
Ujangili wa tembo
        Lembeli ameliambia Bunge kuwa, kwa sasa ujangili wa tembo umekuwa janga la kitaifa.
Amesema ni ukweli usiofichika kwamba tembo sio kwamba wanauwawa bali kwa sasa tembo hao wanateketezwa.
       Amesema kwa mujibu wa tafiti zilizofanywa na taasisi ya utafiti wa wanyamapori nchini (Tawiri 2011), zinazoshabihiana na utafiti wa kimataifa, zinaonesha kwamba tembo wasiopungua 30 wanauwawa kwa siku moja na kwa mwezi wanauwawa 850 ambapo kwa mwaka tembo 10,000 wanauwawa.
          Lembeli amefafanua kuwa, kutokana na kasi kubwa ya kuuwawa kwa tembo, taarifa za kitaalam kutoka Tawiri zinadhibitisha kwamba idadi ya tembo imepungua kutoka 109,000 mwaka 2009 na kufikia chini ya 70,000 mwaka 2012.

Chanzo ni mwanahalisi oline

Hakuna maoni