Zinazobamba

USIPITE BILA KUSOMA KILIO HICHI CHA MWANDISHI HUYU WA HABARI,SOMA HAPO KUJUA

Mwenyekiti wa Umoja wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT), Dk. Reginald Mengi (kushoto), akisalimiana kwa kumbatiana na Mfanyabiashara maarufu nchini, Rostam Azizi ambaye pia ni mmoja wa wamiliki wa vyombo vya habari

Na Malisa GJ.
Kama kuna sekta zenye maslahi duni nchini ni sekta ya habari. Hakuna kada yoyote ambayo watumishi wake wanalipwa hovyo kama kada ya habari. Kwanza mishahara ya wanahabari haina formular. Wanalipwa bila kuzingatia viwango vyao vya elimu na uzoefu.

Ndio maana leo ukienda kwenye "media house" fulani usishangae mwandishi wa "degree" analipwa kidogo kuliko wa "certificate". Yani mwajiri anakulipa tu kwa jinsi anavyokuona. Akiona unafanana na laki mbili anakulipa laki mbili, akiona unafanana na elfu 70 anakulipa elfu 70 na hakuna wa kumuuliza.

Kwa miongo mingi sasa waandishi wamekuwa wakilalamikia maslahi yao ikiwemo mishahara duni wanayolipwa lakini hakuna wa kuwasikiliza. Mwajiri anajiamulia kukulipa laki mbili kwa mwezi kama hutaki ondoka atakuja mwingine.

Kutokana na kulipwa maslahi duni waandishi wengi wamekuwa wakiishi maisha ya "hovyohovyo" hali inayofanya kupoteza heshima yao ktk jamii. Rafiki yangu mmoja mwandishi wa muda mrefu wa gazeti moja kubwa hapa nchini amekuwa akiishi maisha ya "kisanii" sana.

Kwanza haijulikani Dar anaishi sehemu gani. Yupo kama digidigi. Leo analala Mabibo Hostel kwa washkaji wake wa chuo, kesho analala Tandale kwa mshkaji wake mwingine. Kwa miaka mitatu kama Mwandishi wa habari ameshindwa hata kupanga chumba cha kumuwezesha kuishi.

Kutokana na hali mbaya kiuchumi amekua akikopa hela na kushindwa kurudisha. Akikuazima elfu 50 usihangaike kumdai, fanya kama umetoa sadaka maana hata ukimdai hana uwezo wa kukulipa.

Siku moja niliongea nae akaniambia licha ya kuandikia gazeti hilo miaka mitatu bado hajaajiriwa. Hivyo halipwi mshahara bali analipwa kwa story. Anaenda mtaani kutafuta habari na story yake ikitoka analipwa elfu 10. Sasa imagine kwa wiki nzima zinatoka story zake 3 that means analipwa elfu 30 kwa wiki. Huyu mtu anaishije?

Hapo si ajabu ametumia zaidi ya elfu 30 kama nauli ya kusaka hizo habari kwa wiki nzima. Lakini mwajiri hataki kuliona hilo. Na mwandishi akidai maslahi yake, mwajiri atamjibu kwa dharau kama hutaki ondoka watakuja wengine.!

Millard Ayo aliwahi kuelezea namna alivyotumikishwa na mwajiri mmoja nchini wa kituo cha Radio. Alifanya kazi bila kulipwa hata senti moja. Akihangaika mtaani kutafuta habari kwa fedha zake mwenyewe. Kutokana na changamoto ya fedha ilimlazimu kutumia kitambulisho chake cha shule ya "sekondari" ili kwenye daladala alipe nauli ya mwanafunzi maana hakuweza kumudu kulipa nauli ya mtu mzima.

Alisema alipokua kariakoo anatafuta habari huku jua kali linawaka alilazimika kujipoza kwa kunywa maji ya Azam yaliyokua yakiuzwa sh.50 kwenye mifuko ya plastick. Maji hayo yalikuja kupigwa marufuku na baraza la usimamizi wa mazingira (NEMC). Ingekua ni sasa tungesema maji ya "Kandoro". Hayo ndio maisha aliyopitia Millard hadi kufika alipofikia leo.

Dharau, na kejeli za wamiliki wa vyombo vya habari ndizo zimetufikisha hapa. Mmmiliki anataka kuona akipata faida tu lakini hataki kujua mwandishi unaishije.

Kifo cha Sophia Yamola (pichani) mwandishi wa gazeti la DIRA YA MTANZANIA ni mwiba mwingine kwenye taaluma yetu. Taarifa zilizochapishwa kwenye gazeti la JAMHURI zinadai Sophia amefariki akiwa anadai mishahara ya miezi mitatu kwa mwajiri wake.

Sophia alipoanza kuugua alimwandikia mwajiri wake amlipe limbikizo la mishahara yake ili aweze kugharamia matibabu. Maskini Sophia hakuwa hata na Bima ya Afya. Lakini Mwajiri wake alimjibu kwa dharau kuwa "kampuni haina hela kwa wakati huo na ikipata itamlipa".

Hivi unaweza kumwambia mtumishi wako kuwa utamlipa ukipata? Na usipopata je? Kwa hiyo usipopata ndio jasho lake limeenda bure? Mbona wamiliki wa media mna dharau kiasi hiki? Mbona sijawahi kusikia waajiri wengine kama TRA, Benki, NGOs, wakiwaambia watumishi wao kuwa watawalipa wakipata?

Gazeti la Jamhuri linasema kuwa Sophia alifikia hatua ya kukosa hata hela ya kununua matunda. Nesi mmoja wa Hospitali alipokua amelazwa Sophia alisema kuwa Sophia alimuomba amnunulie machungwa siku moja kabla ya kifo chake. Bahati mbaya nesi huyo nae hakua na hela. Hivyo Sophia alikufa bila kupata haja ya nafsi yake kutokana na ugumu wa maisha.

Ikumbukwe Sophia aliyekosa hata hela ya machungwa ni mwandishi mkongwe nchini. Rafiki yangu Cassian Mbunda anasema Sophia Yamola na Jenerali Ulimwengu ndio walikua "role models" wake kwny tasnia ya habari. Sasa jiulize ikiwa mwandishi mkongwe kama huyu alifikia hatua ya kukosa hela ya kununua machungwa vipi kwa waandishi chipukizi?

Waandishi wengi Tanzania hawana mikataba. Waajiri wanawalipa wanavyojisikia. Inaumiza, inakera, inaudhi.

Marehemu Rehema Mwakangale ni mmoja wa waandishi walionyanyasika katika utumishi wao. Licha ya kufanya kazi ITV kwa miaka 8 hakuwahi kuajiriwa. Hadi anakufa alikuwa kibarua. This is totally unfair.

Halafu mwajiri wake anapita makanisani na misikitini akitoa misaada ya mamilioni ya fedha kumbe watumishi wake wanakufa njaa. Hakika kama Mungu yupo malipo ni hapahapa duniani.!

Kuna chombo kimoja kikubwa cha habari hapa nchini chenye Radio na Television, waandishi wake hawajalipwa mishahara tangu mwezi August mwaka jana. Lakini mmiliki ambaye amewahi kuwa mbunge na waziri, saivi yupo "busy" kwenye mbio za kugombea ubunge hana story na watumishi wake.

Mbunge ni mtetezi wa wananchi na anayelinda maslahi yao., hivi huyu jamaa anawezaje kutetea wananchi na kulinda maslahi yao kama ameshindwa kulinda maslahi ya watumishi wake? Huyu dawa ni kumnyima kura ili azimie tena kama alivyozimia baada ya kushindwa uchaguzi wa 2010.

Waajiri wanadharau taaluma hii na kuiona si taaluma kwa sababu hakuna sheria inayowalazimisha kufanya hivyo. Mwajiri anakujibu hovyo "degree holder" kwa sababu anajua ukiondoka atamwajiri kijana wa form four aliyefeli akaweza kufanya kazi yako.

Comrade Dotto Bulendu jana alieleza kisa cha kigogo mmoja anayemiliki kituo cha radio, hajawalipa mishahara watumishi wake kwa miezi kadhaa na walipomuuliza aliwajibu kuwa hata wakiondoka ataajiri "waimba kwaya" waje kutangaza, kwa sababu waimba kwaya wana sauti nzuri kuliko watangazaji wake. Hii ni dharau ya kiwango cha PhD.!

Ugumu wa maisha kwa waandishi wengi ndio unasababisha kuwa ombaomba kila wanapoitwa kukusanya habari. Unamuita mwandishi kwenye tukio lako amekuja kwa bodaboda, hajala, hata vocha kwenye simu hana. Alipofika amekubeep ili ujue kafika. Sasa unategemea huyu mwandishi akimaliza kucover story ataondoka hivihivi wakati hata nauli ya kurudi hana?

Lazima adai chochote.. na ukimpa chochote unampangia na jinsi ya kuandika hiyo story. The one who control ur economy, control your mind. Kwa hiyo waandishi wengi wanakiuka maadili ya kazi yao kwa sababu ya kupewa bahasha za kaki na "sources" wao. Kwenye taaluma inaitwa "Payola".

Lakini mwajiri anamjibu mwandishi kwa dharau kwa kuwa anajua hakuna sheria inayombana na kulinda taaluma. Hata akiajiri "house girl" wake akatangaze "nobody cares"...

Ndio maana muswada wa sheria ya huduma za habari unaowalazimisha kuajiri waandishi wenye "degree" tu, wameupinga haraka sana maana wanajua utawacost.

Mimi nasema licha ya kasoro kadhaa za muswada huo ikiwa ni pamoja na kujiunga na TBC kwa ajili ya taarifa ya habari, lakini kipengele cha kulinda professionalism ya waandishi kwa kuajiri degree holders nakiunga mkono.

Waajiri wakilazimishwa kuajiri degree holders watalazimika kuboresha maskahi yao. Na sisi sio wa kwanza kufanya hivyo. Kenya wameweza, kwanini sisi tushindwe?

Sheria ikiset standards za professionalism itaweka kiwango cha chini cha mshahara wa mwandishi. Kwamba mwandishi asilipwe chini ya milioni moja au laki tisa au kiwango kingine chochote kinachokubalika.

Na hakuna mwajiri atakayethubutu kukulipa chini ya hapo. Pia sheria itamlazimisha mwajiri akupatie bima ya afya, mkataba wa ajira na kuchangia kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii.

Waajiri kwa kulitambua hilo wamejitokeza haraka na kupinga kipengele hicho na kudai eti wakilazimishwa kuajiri "degree holders" watakosa watumishi maana wenye degree ni wachache. What a weak argument? Wanaojua kama wenye degree ni wachache au ni wengi ni TCU. Waajiri waakubali then waone kama wenye degree ni wachache kama wanavyodhani.

Kusema wenye degree ni wachache hivyo tuajiri mtu yoyote ni sawa na kusema tuajiri waganga wa kienyeji kwenye hospitali zetu kwa kuwa madaktari ni wachache. Huu ni utetezi wa kijinga sana. Lazima tuheshimu taaluma za watu.

Cha ajabu ni kuwa wapo waandishi wameanza kujitokeza kuwaunga mkono wamiliki wa media juu ya kupinga kuajiri degree holders. Ukimuona mwandishi anapinga kipengele hiki ujue kuna mawili. Mosi ni kuwa yeye mwenyewe ni "kanjanja" hivyo anaogopa wakiajiriwa degree yeye atakosa kibarua. Au yeye ni vuvuzela la waajiri.

Tumeanza kuzozana wenyewe kwa wenyewe kwa kutetea maslahi ya waajiri. Huu ni ulimbukeni. Waandishi tuungane pamoja kudai maslahi yetu. Tukianza kupingana wenyewe kwa wenyewe tutaendelea kukandamizwa kwa sababu vita vya panzi ni furaha kwa kunguru.

Tusipopigania maslahi yetu wenyewe tusitegemee kuna atakayetupigania. Tusimame, tuungane, tupigsnie maslahi yetu. Tumechoka kuishi maisha ya aibu huko mitaani, tumechoka kunyanyaswa, tumechoka kufa tukiwa vibarua, tumechoka kufa vifo vya aibu vya kukosa hata hela ya machungwa kama marehemu Sophia Yamola. Tuungane sasa wakati ndio huu.!


JIPU LIMEPASUKA, SIWEZI KUWA ADUI KWA KUSEMA UKWELI.!
Malisa GJ || Your Partner In Critical Thinking.!

Hakuna maoni