SAKATA LA LUKU,SASA SERIKALI KUBULUZWA MAHAKAMANI,KAMPUNI YA SELCOM YALIA NA WAZIRI SIMBACHAWENE,BOFYA HAPO KUJUA

Kampuni ya Selcom
iliyoingia mkataba na Shirika la Umeme nchini (Tanesco) kuuza umeme kwa njia ya
mtandao, imesema Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene, amekurupuka
kuvunja mkataba kati yake na Tanesco na kutishia kuishitaki serikali.
Kampuni hiyo
imesema serikali imepata hasara ya Sh. bilioni 6.0 katika kipindi cha
siku nne, ambacho kampuni hiyo ilisitishwa kutoa huduma ya kuuza umeme. Kampuni
hiyo ilisema huuza umeme kwa asilimia 75.
Aidha, kampuni
hiyo imesema haijapata notisi toka serikalini ya kusitishwa kwa mkataba wake na
Tanesco.
Juzi waziri
Simbachewene alitangaza kusitisha mkataba na kampuni hiyo kwa kushindwa kutoa
huduma bora ya mfumo wa Luku kutokana na mitambo yao kutokukidhi vigezo na
kusababisha usumbufu kwa wateja.
Chanzo changu janaJumamosi
ilifanya mahojiano na Meneja Ukuzaji Biashara na Masoko kutoka Kampuni ya
Selcom, Juma Mgoli, ambaye alisema ameshangazwa na taarifa ya waziri kudai
kampuni yake haina vigezo wakati imekuwa ikiuza umeme wa Tanesco kwa asilimia
75.
Alisema wameshindwa
kuelewa ni vigezo gani vilivyotumiwa na waziri kusitisha mkataba, wakati
kampuni yake imekuwa ikiuza umeme wa Sh. bilioni 1.0 hadi bilioni 2.0 kwa siku.
Aliongeza kuwa
inapokaribia mwisho wa mwezi mauzo hufika hadi Sh. bilioni 4.0 kwa siku.
Alisema kutokana
na mauzo hayo, inaonyesha dhahiri kuwa kampuni yao inafanya vizuri sokoni na
kwamba tatizo la mtandao halipo upande wao bali lipo kwa Tanesco.
Alisema Tanesco
ina mashine za Electronic Vending Getway (EVG) ambazo uwezo wake ni mdogo
katika kuhudumia wateja, hivyo kusababisha ukosefu wa mtandao. “Mfano mzuri
nadhani unaona tangu tumeacha kutoa hiyo huduma kuna foleni kubwa kwenye vituo
vinavyouza umeme sasa, tutaambiwaje hatufanyi vizuri sokoni,” alihoji.
Aliongeza kuwa
Selcom imejiunganisha kwenye benki 34 kwa ajili ya kutoa huduma hiyo.
Alisema toka
kampuni yake ilipozuiwa kuuza umeme katika kipindi cha siku nne, Tanesco
imepata hasara ya Sh. bilioni 6.0 na serikali imepoteza mapato ya kodi ya zaidi
ya Sh. bilioni 1.0.
Hata hivyo, alisema
suala hilo linahusu masuala ya kisheria na kwamba wameshawasiliana na
wanasheria wao kuangalia kama kuna ukiukwaji wowote wa mkataba huo ili sheria
ichukue mkondo wake.
Alisema waziri
hana mamlaka ya kuvunja mkataba kienyeji kwani uvunjaji wa mkataba una
utaratibu wake.
Usitishwaji wa
huduma hiyo, ulianza tangu mwanzo wa wiki hii ambapo juzi baadhi ya wateja
walikuwa wakitumia ujumbe mfupi kwenye simu zao za mkononi unaosema:
"Ndugu mteja huduma ya Luku haipatikani kwa sasa kutokana na shida iliyopo
upande wa washirika wetu, tafadhali tembelea wakala wa Tanesco kununua umeme
wako".
Hata hivyo, jana wakati Chanzo changu kilikielekea mtamboni
ujumbe mwingine kupitia simu za mkononi ulitumwa ukieleza: "Ndugu
mteja sasa unaweza kununua umeme wako wa Tigopesa kwa kupiga namba *150* 01#
Pia Chanzo hicho kilishuhudia vituo vingi vinavyouza umeme wa Luku
vikiwa na foleni ya wateja wanaotaka huduma hiyo.
Baadhi ya wateja walikuwa wakiilalamikia Tanesco kuifungia
kampuni iliyokuwa ikitoa huduma hiyo kwa njia ya mtandao na kusababisha
usumbufu mkubwa.
CHANZO: NIPASHE
No comments
Post a Comment