HABARI KUBWA LEO-KAMATI KUU YA CCM KUPASUKA,NI MPANGO WA WASAKA URAIS,NAPE ABAINI NJAMA SOMA HAPA KUUA

Mbio za urais ndani ya CCM sasa zimefikia pabaya
baada ya kuibuka hofu ya kuwapo kwa mpango wa kuivuruga Kamati Kuu kabla ya
haijakutana kuchuja majina ya makada watakaotakiwa kupigiwa kura na Halmashuri
Kuu ili kumpata mgombea atakayepeperusha bendera ya chama hicho kwenye Uchaguzi
Mkuu.
Hadi sasa CCM
haijatangaza ratiba yake kwa ajili ya kuongoza wanachama wanaotaka kuwania
uongozi wa ngazi mbalimbali kwa tiketi ya chama hicho.
Hata hivyo,
Chanzo changu kilitaarifiwa wiki hii kuwa Kamati Kuu ya CCM itakutana Mei 20 na
kufuatiwa na vikao vya siku mbili vya Halmashauri Kuu Mei 21 na 22 kwa ajili ya
kupitisha ratiba, ilani na taratibu nyingine za uchaguzi, ikiwa ni kuashiria
kuanza rasmi kwa mchakato wa uchaguzi ndani ya chama hicho kikongwe.
Wakati chama
kikitafakari kuanzisha rasmi mchakato wa uchaguzi, tayari kuna habari kuwa moja
ya makundi ya makada wanaowania urais limeonyesha kutokuwa na imani na mwenendo
wa Kamati Kuu ambayo ina jukumu la kuchuja wanaowania urais na kupeleka majina
Halmashauri Kuu kwa ajili ya kupigiwa kura.
Taarifa ambazo Chanzo changu imezipata
zinaeleza kuwa kundi hilo linashawishi wanachama ili wakubali kuomba kupiga
kura ya kutokuwa na imani na Kamati Kuu kwa madai kuwa inaonekana kupendelea
baadhi ya waliojitokeza na kubana wagombea wengine.
Chanzo chetu cha
habari kimeeleza kuwa kundi hilo limekuwa likifanya vikao mbalimbali vya kuweka
mkakati wa jinsi gani ya kuivuruga Kamati Kuu kabla ya kuchuja majina ya wagombea
urais kwa tiketi ya CCM.
“Kuna mkakati wa
kuweka CC itakayowasaidia kwa kuwa ukishapita hapo, umeshakuwa Rais wa nchi
hii. Uzuri ukishinda ndani ya chama na kutangazwa kuwa mgombea wao, basi
makundi yote hurudi kukipigania chama na wengine kujipendekeza ili wapewe
nafasi katika serikali ijayo,” alisema mpashaji habari wetu ambaye ni mmoja wa
viongozi wa juu wa CCM.
Taarifa zaidi
zinaeleza kuwa mpango huo unafanyika kwa umakini mkubwa ili kuweza kuhakikisha
Kamati Kuu haikati jina la mgombea wa kundi hilo kama ambavyo imewahi kufanyika
kwa makada wengine ambao majina yao hayakupelekwa kwenye Halmashauri Kuu kwa
ajili ya kupigiwa kura kutokana na nguvu yao kwenye chama.
Kama hilo
litafanikiwa itakuwa ni kwa mara ya pili kutokea baada ya mwaka 1995, Jakaya
Kikwete kumlalamikia aliyekuwa katibu mkuu wa CCM, Lawrance Gama kuwa hawezi
kumtendea haki baada ya kuonekana akiwa amevaa nguo yenye nembo ya mmoja wa
waliokuwa wakiwania kuteuliwa na chama hicho kugombea urais.
Alipoulizwa kuhusu
mkakati huo, katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema kuwa
wamesikia na kuelezwa kuwa kundi hilo linagawa fedha kufanikisha jambo hilo kwa
kuwa wanadhani sekretarieti ya chama haiwapendelei wao.
“Wanadhani kuna
watu wanapendelewa, kama suala hilo lipo bila shaka chama hakiwezi kukaa kimya
kwani huo ni uasi na usaliti kwa chama,” alisema Nape.
Alisema kuwa
ndani ya chama viko vyombo vingi ambavyo kama mtu ana shida anaingia kwenye
mikutano sahihi ya chama.
“Mtu huwezi
kutengeneza vikao nje ya vikao halali halafu urudi kuongoza chama hicho hicho,”
alisema Nape.
“Labda watu wana
mpango wa kukivuruga chama hiki halafu wagombee kwa chama kingine sawa, lakini
kama wanataka kugombea humuhumu CCM, haitawezekana,” alisema Nape.
Mmoja wa wajumbe
wa CC ambaye pia ni Meya wa Ilala, Jerry Silaa alipoulizwa kuhusu mkakati huo
kama amesikia, hakuwa tayari kusema chochote kwa kuwa yeye yupo ndani ya Kamati
Kuu.
Hadi sasa makada
sita wa CCM wamefungiwa kwa zaidi ya miezi 12 kujishirikisha na harakati za
uchaguzi ndani ya chama. Makada hao ni mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa
na Frederick Sumaye. Pia, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Bernard Membe, Waziri wa Kilimo na Chakula, Stephen Wasira, Naibu Waziri wa
Sayansi na Teknolojia, January Makamba na waziri wa zamani wa Nishati na
Madini, William Ngeleja.
Baadhi ya makada
wanaotajwa kutaka urais kwa tiketi ya chama hicho ni pamoja na Waziri Mkuu
Mizengo Pinda, waziri wa zamani wa Ulinzi, Emmanuel Nchimbi, waziri wa zamani
wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha na Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta na
Waziri wa Ujenzi, John Pombe Magufuli.
Alipoulizwa kama
kuna watu wanapita kushawishi wanachama kujiunga na mkakati huo, mwenyekiti wa
CCM wa Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja alisema hofu hiyo inatokana na chama
kuchelewa kuruhusu wanachama wake kuingia kwenye mchakato.
“Kama chama
kingeruhusu mapema, kingedhibiti mapema mambo haya,” alisema Mgeja.
Muda mfupi baada
ya kumaliza mazungumzo, Mgeja, ambaye anaingia kwenye vikao vya Halmashauri Kuu
ya CCM kutokana na nafasi yake kwenye mkoa, alipiga simu na kumweleza mwandishi
kuwa anataka kuwatoa hofu wanachama wa CCM kuwa chama kiko imara na hakuna
ajenda ya mpasuko ndani ya chama.
Akizungumza na Chanzo changu kwa simu,
Makamba, ambaye ni mbunge wa Bumburi, alisema amesikia kuwapo kwa mpango huo
lakini hajathibitisha.
“Hata mimi
nimezisikia habari hizo ingawa hazijathibitishwa. Kwa kuwa hazijathibitishwa,
siwezi kuzungumzia kiundani,” alisema Makamba, ambaye ni Naibu Waziri wa
Sayansi na Teknolojia.
“Nachoweza kusema
ni kwamba chama chetu kina utaratibu, kinatabirika na kinaeleweka. Hakuna haja
ya kuwa na papara katika hili na mimi sina hofu na hili kwa kuwa najua kila
kitu kitakwenda kama ilivyopangwa.”
Alisema anajua kuwa
uteuzi utafanyika miezi miwili kabla ya uchaguzi ili utakapofika mwezi Agosti
chama kipeleke majina kwenye Tume ya Uchaguzi yakiwa yamechujwa kwa umakini
bila ya kuwa na papara ya aina yoyote.
Waziri Mkuu wa
zamani, Frederick Sumaye na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Bernard Membe, ambao wote wanatajwa kuwamo kwenye mbio za urais, hawakutaka
kuzungumzia suala hilo, Membe akisema yuko safarini kikazi na Sumaye akisema
hajasikia habari hizo.
Juhudi za kumpata
Waziri Mkuu Mizengo Pinda na mbunge wa Monduli, Edward Lowassa hazikufanikiwa.
Chanzo ni Gazeti la Mwananchi
No comments
Post a Comment