KAMANDA WA BAVICHA AJITOSA RASMI SHINYANGA,SOMA HAPO KUJUA
![]() |
Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Taifa la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bavicha), Pastrobas Katambi |
KADIRI uchaguzi mkuu wa Oktoba unavyokaribia,
ndivyo sura mpya kwenye siasa zinachomoza na hivyo kuwatia hofu wawakilishi
wanaoshikilia kata, majimbo na hata kiti cha urais kitakachokuwa wazi baada ya
Rais Jakaya Kikwete kumaliza muda wake.
Pastrobas Katambi, ni Mwenyekiti wa
Baraza la Vijana Taifa la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bavicha). Ni
Mwasheria kitaaluma na mmoja wa wanasiasa vijana anayejitokeza kwa mara ya
kwanza kusaka ubunge katika Jimbo la Shinyanga Mjini.
Kwa sasa jimbo hilo,
linashikiliwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Steven
Masele (CCM), ambaye alimshinda kimiujiza mpinzani wake wa mwaka 2010, hayati
Magadula Shellembi wa Chadema.
Chanzo changu kimepata nafasi ya kufanya
mahojiano na Katambi ili kujua sababu zinazomsukuma kujitosa kwenye ubunge
katika jimbo hilo.
SWALI: Unaweza kutueleza historia yako kiufupi?
JIBU: Mimi naitwa Pastrobas Katambi, nimezaliwa mwaka 1985 katika
familia ya mzee Katambi nikiwa mtoto wa nne kati ya watano.
Elimu yangu ya Msingi
nimehitimu Mwenge mwaka 1999 na baadaye nikachaguliwa kwenda Nsumba
Sekondari ya jijini Mwanza lakini nilijiunga na Kahama Sekondari na baadaye
nilihamia Seminari ya Mtakatifu Mary’s iliyopo Nyegezi Mwanza na kuhitimu mwaka
2004.
Baadaye nikachaguliwa
kujiunga na shule ya Serikali ya wavulana Malangali iliyopo mkoani Iringa,
nikasoma kidato cha tano na sita na kuhitimu mwaka 2007.
Mwaka 2007 nilichaguliwa katika vyuo vikuu vitatu vya Makerere
nchini Uganda, Mtakatifu Augustino (SAUT) Mwanza na Chuo cha Uongozi wa
Mahakama Lushoto (IJA), lakini nikajiunga SAUT kusoma shahada ya sheria
kwa miaka mine.
Nikiwa mwaka wa
tatu, nilianza kufanya kazi na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu cha jijini
Dar es Salaam.
Baada ya kuhitimu
masomo, uongozi wa SAUT kwa ushawishi wa Makamu Mkuu wa Chuo mstaafu Dk.
Charles Kitima ulitoa Scholarship kwa wanafunzi waliofanya vizuri katika
shahada ya sheria, hivyo nikapata fursa ya kusoma shahada ya pili ya
uzamilihapo hapo mwaka 2012.
Mwaka huo pia
nikaanza kufanya kazi na ofisi za sheria za mawakili na baadaye nikaajiriwa
katika kampuni ya Sahara Media Group.
Nikiwa katika kampuni
hiyo kama Mwanasheria, nilifanya kazi kwa bidii na kupata mafanikio makubwa kwa
muda mfupi na badaye nikaongezewa majukumu kuwa Meneja Utawala na
Raslimali Watu msaidizi na baada ya kufanya kazi hiyo kwa kipindi kirefu
nilijiuzulu nilipochaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Vijana Taifa.
Awali, bado nikiwa
mwanachama wa kawaida wa Chadema pia nilifanikiwa kuongoza Tawi la SAUT kama
mwenyekiti na baadaye nikawa mwanasheria wa kanda ya Ziwa Mashariki
(Serengeti) na Magharibi Victoria wakati huo bado nikiwa nafanyakazi
Sahara.
SWALI:
Una muda gani tangu uingie kwenye siasa?
JIBU: Nimeanza siasa
muda mrefu tangu mwaka 2003 na mwishoni mwa 2004 nilishiriki vyema uchaguzi
mkuu 2005 nikiwa kidato cha tano kuipigia debe Chadema kwa sababu ya kuona nchi
yetu imejaliwa rasilimali nyingi lakini viongozi wetu wengi ni wala rushwa.
SWALI: Kwanini umechagua jimbo la Shinyanga?
JIBU: Nimeamua kuomba kugombea jimbo hilo kutona na jimbo
hilo kukosa maendeleo kwa muda mrefu na viongozi wa leo wanaopata nafasi
wametanguliza mbele rushwa na kusababisha wananchi kukosa maendeleo.
SWALI: Mapungufu yapi umeyaona?
JIBU: Ndani ya chama changu sijaona mapungufu, hiki ndicho chama
pekee ambacho hata Baba wa Taifa hayati Mwalimu Nyerere katika maoni yake
aliwahi kusifu sera zake za utu, uadilifu, kupinga na kuchukia rushwa.
SWALI: Endapo utachaguliwa nini kipaumbele
chako?
JIBU: Nikichaguliwa kuwa mbunge katika jimbo la Shinyanga mjini,
kwa kuwa matatizo ni mengi sana na jimbo linahitaji mbunge muadilifu
na mwajibikaji anaejua kero na shida sugu na umaskini wa watu wake,
nitapambana ili watu wafahamu haki na usawa kwa wote, pamoja na kuboresha
huduma za jamii kwa kukuza na kuimalisha uchumi wa Shinyanga.
SWALI: Hali ya jimbo ikoje kielimu na
miundombinu?
JIBU: Kwa kweli ni miaka 53 sasa tangu uhuru wa nchi hii na
jimbo hili limeongozwa na wabunge wa CCM lakini bado katika maeneo mengi
hayajaunganishwa na barabara kwa kiwango cha lami.
Mkoa wenye dhahabu kila kona lakini unapambwa na barabara za
mashimo hadi mjini pia huduma za maji na umeme kwa watu wengi hazipatikani,
shule hazina vitabu na vifaa vya kufundishia pamoja na upungufu wa maabara.
SWALI: Unadhani tatizo ni nini?
JIBU: Tatizo ni uhaba wa walimu na vifaa na hilo linasababisha
wanafunzi wengi kutokufaulu vizuri pia walimu hawana nyumba za kuishi,
mishahara midogo na bado wanaidai Serikali na wanachereweshewa kupanda
madaraja. Haya yote ni matatizo na kero zinazopaswa kutatuliwa.
SWALI: Umejipanga vipi kuwasaidia wananchi?
JIBU: Nikipitishwa na Chadema na kuchaguliwa mbunge wa Shinyanga,
nitaweka mipango imara na sera makini zinazotekelezeka, ushirikishwaji na
uwajibikaji wa kila mtu kwa uadilifu na upendo kwa manufaa ya wananchi.
Nitahakikisha nyota ya matumaini inarejea na kutoa nuru kupitia
utetezi na usimamiaji makini wa kodi za wananchi katika halmashauri na bungeni.
SWALI: Vijana wanamchango gani katika uchaguzi?
JIBU: Vijana wana mchango mkubwa sana wa kushiriki moja kwa moja
kwa kugombea ama kupitia uwakilishi kumchagua kijana katika nafasi ya uongozi
ikiwa ni pamoja na kunadi sera, kampeni, kusimamia kituo kama mawakala,
kuhesabu na kulinda kura kwani wizi wa kura huvuruga amani kwa kulazimishwa
kuongozwa na mtu ambaye hawakumchagua.
SWALI: Kwanini vijana wengihawapigi kura?
JIBU: Vijana wengi hawashiriki katika uchaguzi kwa sababu zamani
walikuwa hawaelewi umhimu wa kuchagua viongozi bora, matatizo ya vijana
yanasababishwa na kukithiri kwa rushwa, ubaguzi na upendeleo kwa watoto wa
viongozi na matajiri na kuweka tabaka la wasiokuwa nacho na kusababisha vijana
kukosa fursa za ajira.
Wito wangu sasa kwa vijana waliokuwa wakilalamikia kero hizo,
kutumia vizuri fursa ya kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika daftari jipya
la kudumu la wapiga kura mara tu uandikishaji huo utakapotangazwa katika maeneo
yao.
Hii ndiyo itakuwa fursa pekee kwao, kuendelea kulalamika
hakutawasaidia kama hawatachukua hatua kwa vitendo ili kupata haki ya
kuwachagua viongozi bora na makini wawatakao.
Makala
haya yameandikwa na Mwandishi Wetu mkoani Mwanza
No comments
Post a Comment