UFISADI WA BILIONI 200 ZA IPTL--MAPYA YAZIDI KUFICHUKA ,WAMILIKI WAKE WAANZA KUGEUKANA,RUGEMALIRA ALIA NA YAKE,SOMA HAA KUJUA ZAIDI
MMOJA
wa waliokuwa wamiliki wa Kampuni ya Independent Power (IPTL) amedai hana
ushahidi na hakuhusishwa katika uuzaji wa hisa za mbia mwenzake wa kampuni
hiyo, uuzaji ambao hatimaye umesababisha kuchotwa kwa mabilioni ya shilingi
katika akaunti ya Tegeta Escrow, imefahamika.
Mmiliki huyo ni Mkurugenzi wa
Kampuni ya VIP Engineering (VIPEM), James Rugemalira na alitoa maelezo hayo
kwenye ofisi za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ambayo
inachunguza tukio la kuchotwa kwa fedha hizo zilizokuwa zimehifadhiwa na Benki
Kuu ya Tanzania (BoT).
Katika maelezo aliyoyatoa kwa CAG na
ambayo Chanzo hicho imefanikiwa kupata nakala yake, Rugemalira alieleza kwamba
hakushirikishwa wakati mbia mwenzake wa zamani katika IPTL, Kampuni ya Mechmar
ya Malaysia, ilipofanya uamuzi wa kuuza hisa zake (asilimia 70) kwa Kampuni ya
Pan African Power Solution (PAP) ambayo sasa ndiyo inamiliki IPTL.
“Bwana Rugemalira hakuwa na ushahidi wa
kuuzwa kwa hisa za Mechmar kwa PAP ingawa alikwishaona baadhi ya barua za
Mechmar kwenda Wizara ya Nishati na Madini.
“Rugemalira hakuhusishwa katika
uuzwaji wa Mechmar kwa Piper Link. Wakati wa kusaini transfer tarehe 24/1/2014,
kuna document (nyaraka) Bwana Rugemalira aliiona ambayo inaonyesha kununuliwa
kwa share (hisa) za Mechmar,” inasema sehemu ya maelezo hayo ya Rugemalira
ambayo yamesainiwa naye Septemba 10, mwaka huu.
Rugemalira naye aliuza hisa zake kwa
kampuni hiyo ya PAP inayomilikiwa na Harbinder Seth Singh kwa thamani ya dola
za Marekani milioni 75 (sawa na shilingi bilioni 123 za Tanzania).
Uuzwaji wa hisa za Mechmar kwa Piper
Link na hatimaye PAP, ndiyo uliosababisha Rugemalira auze hisa zake kwa kampuni
hiyo; tukio ambalo mwisho wake umewezesha kutolewa kwa fedha katika akaunti ya
Tegeta.
Katika maelezo yake kwa CAG, Rugemalira
ameeleza kwamba kwa kadri anavyofahamu, alilipwa fedha hizo kwa taratibu halali
za kibiashara na kisheria.
Ofisi ya CAG inafanya uchunguzi
kutafuta ni kwa vipi kiasi cha shilingi bilioni 200 zilitolewa katika akaunti
hiyo ya Tegeta iliyokuwa ikishikiliwa na BoT na kulipwa kwa PAP.
Pia alisisitiza katika maelezo yake
hayo kwamba uamuzi wa serikali, akimtaja Waziri wa Nishati na Madini, Profesa
Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu wake, Eliakim Maswi, kuruhusu fedha hizo zitoke
BoT na kumaliza mgogoro zimeiokoa serikali na hasara nyingi ikiwamo kununua
umeme wa bei ghali zaidi kutoka sehemu nyingine.
Hata hivyo, maelezo hayo ya Rugemalira
yamefunua mapya taarifa kuhusu uhalali hasa wa Singh kupewa hisa za Mechmar na
hatimaye kuruhusiwa kuchukua fedha hizo zilizokuwa zimehifadhiwa BoT.
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali
(PAC) ambayo ndiyo iliyomwagiza CAG kufanya uchunguzi huo, ilikuwa na wasiwasi
kwamba Singh atajipatia kiasi cha shilingi bilioni 200 kwa kununua hisa za
Rugemalira.
Kwa
mujibu wa Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe, Piperlink ilinunua asilimia 70 ya
hisa hizo za Mechmar kwa thamani sawa na shilingi milioni sita za Tanzania
lakini nayo ikaziuza kwa PAP kwa thamani ya dola 300,000 (shilingi milioni 500
za Tanzania).
Hata hivyo, wakati Mechmar ikidaiwa kuuza
hisa zake hizo mwaka 2010, taarifa zilizopo zinaonyesha kwamba ilikuwa
imefilisiwa nchini Malaysia na kwa mujibu wa sheria za nchi za Jumuiya ya
Madola, isingewezekana kuruhusiwa kuuza hisa zake.
“Ni kwa njia gani ambako PAP ilichukua
hisa za Mechmar katika IPTL mwaka 2010 wakati Mechmar ikiwa inafilisiwa? Sheria
za nchi zote ulimwenguni haziruhusu jambo hilo kutokea kwani ni marufuku hisa
za kampuni iliyo chini ya muflisi kuuzwa au kufanyiwa biashara yeyote.
“Au, kama wengine wanavyoamini,
wakurugenzi wa Mechmar waliwazidi akili wasimamizi wa Malaysia, ikiwa ni pamoja
na Mahakama Kuu na kufaulu kuuza hisa zao? Anachoeleza Harbinder ni kuwa
Mechmar kwanza iliuza hisa zake katika IPTL kwa kampuni kificho inayoitwa Piper
Link, ambayo ilizihifadhi, kwa sababu moja au nyingine, huko British Virgin
Islands vya Uingereza,” ilisema taarifa ya Kabwe iliyopelekwa kwa CAG, Machi
mwaka huu.
Mmoja wa wabunge waliosimama kidete
kutaka fedha zilizotolewa BoT zirudishwe, David Kafulila, alisema haingii
akilini kwamba hisa ambazo zimenunuliwa kwa shilingi milioni sita na baadaye
milioni 500, zipande thamani ghafla na kufikia mabilioni ya shilingi.
Mbunge
huyo wa Kigoma Kaskazini (NCCR-Mageuzi), alisema suala la PAP kununua hisa za
IPTL na hatimaye kupewa mabilioni hayo limegubikwa na rushwa.
Wakati hayo yakiendelea, zimeibuka
tuhuma kwamba baadhi ya viongozi wa serikali wamepokea fedha kutoka kwa mmoja
wa waliokuwa wamiliki wa IPTL katika mazingira ya kutia shaka.
Taarifa hizo zimeenea katika mitandao
mbalimbali ya kijamii huku majina kadhaa ya viongozi wa serikali na wabunge
yakitajwa.
Mmoja wa wabunge ambao majina yao
yametajwa sana ni Mbunge wa Bariadi Mashariki, Andrew Chenge, ambaye katika
mazungumzo yake na Chanzo hicho amekataa kuzungumzia suala hilo.
“Mimi kwa sasa nashughulika na masuala ya
Katiba. Nafanya kazi hadi usiku. Sipendi kujadili mambo yangu binafsi au ya
kikazi na vyombo vya habari. Naomba kwenye suala hilo la IPTL mniache,” alisema
Chenge.
Chenge ni Mwenyekiti wa Kamati ya
Uandishi wa Katiba ya Bunge la Maalumu la Katiba linaloendelea na vikao vyake
mkoani Dodoma.
Chanzo ni Gazeti la Raia Mwema
Hakuna maoni
Chapisha Maoni