MASIKINI WAZIRI WA KIKWETE,AINGIZWA KWENYE MKENGE MCHAFU NA MBIA WA KAMPUNI YA IPTL,SOMA HAPA KUJUA ZAIDI
PICHANI NI RAIS JAKAYA KIKWETE |
Na
Ezekiel Kamwaga
WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, amesema amepokea kiasi cha dola za Marekani
milioni moja (Shilingi bilioni 1.65) kutoka kwa mmoja wa waliokuwa wamiliki wa
kampuni ya Independent Power (IPTL), James Rugemalira.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, fedha
hizo alipewa na mfanyabiashara huyo kama mchango wa kusaidia Shule ya Sekondari
Babro ya jijini Dar es Salaam, ambayo yeye ni mmoja wa wakurugenzi wake.
Maelezo hayo ya Waziri Tibaijuka
yamekuja katika wakati ambao zimeibuka taarifa kwamba mfanyabiashara huyo
ametoa fedha kwa baadhi ya vigogo wa serikali (sasa na zamani) mara baada ya
kulipwa fedha kutoka katika akaunti ya Tegeta Escrow inayotajwa kugubikwa na
utata.
Katika mazungumzo
yake na Chanzo hicho wiki hii, Profesa Tibaijuka, aliyewahi
kuwa Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Makazi (UN-HABITAT), amesema
alipokea fedha hizo kutoka kwa Rugemalira kwa vile alihakikishiwa ni salama na
si za uovu.
“Ni kweli kaka yangu JR (James
Rugemalira) baada ya kulipwa alitoa mchango wa dola milioni moja kwa Shule ya
Sekondari ya Wasichana ya Babro ili tulipe deni sugu tulilokuwa nalo Bank M.
Tulichukua mkopo kwa kutumia dhamana ya nyumba yangu na kama tusingelipa basi
nyumba yangu ingechukuliwa.
“VIP walitutaka kufungua akaunti
Mkombozi Bank, tukalipwa na kuhamishia fedha Bank M ili kulipa hilo deni.
Malipo haya yote yalifanyika katika benki zilizopo hapa nchini na kwa upande
wangu yanaonyesha nia njema niliyo nayo.
“Sikudhani malipo hayo yaliyosimamiwa
na BoT, Wizara husika na Mahakama yangelikuwa na dosari ambazo sasa zinadaiwa
kuwapo kama nazo ni kweli.
“Kimsingi, mimi bado najiuliza, hivi
tatizo katika suala hili la fedha za IPTL ni VIP kulipwa fedha zake au ni namna
gani ililipwa?
“Hivi watu waliolipwa na VIP wangewezaje
kujua kwamba wanalipwa fedha chafu ikiwa wenyewe hawakuhusika kabisa na
utolewaji wa fedha katika akaunti ya Escrow ya BoT?” alihoji Tibaijuka.
Chanzo hicho halikuweza
kupata maoni ya Rugemalira mwenyewe kuhusu suala hili kwa vile ilielezwa yuko nje
ya nchi kwa sasa lakini sasa limejiridhisha pasi na shaka kwamba malipo hayo
yalifanyika kupitia Benki ya Mkombozi.
Mwaka jana unaonekana pia kuwa mwaka
wa mavuno kwa Rugemalira kwani pia alilipwa kiasi kikubwa cha fedha na
watengenezaji wa bia ya Heineken kama makubaliano ya kuvunja nao mkataba.
Benki ya Mkombozi inamilikiwa na Kanisa
Katoliki nchini kama mwenye hisa kiongozi lakini pia kuna wabia wengine wadogo.
Chanzo hicho kimeambiwa kwamba
imekuwa utaratibu wa kawaida wa Rugemalira kutumia benki hiyo katika malipo
yake mengi anayofanya na kwamba kwa wale wasio na akaunti, huwataka kwanza
wafungue na ndipo afanye uhamishaji wa fedha.
Kampuni ya Rugemalira, VIP
Engineering and Management (VIPEM), ilikuwa inamiliki asilimia 30 ya IPTL huku
kampuni ya Mechmar Bhd ya Malaysia ikiwa na hisa asilimia 70.
Kutokana na kiasi hicho cha hisa,
Rugemalira amelipwa kiasi cha dola milioni 75 (Shilingi Bilioni 123) huku
taarifa mbalimbali zilizopo zikionyesha kwamba alilipwa kiasi cha dola milioni
7.5 ( Shilingi bilioni 12.4) mwaka jana na kiasi kilichosalia alimaliziwa mwaka
huu.
Kiasi hicho cha fedha kililipwa
kwa Rugemalira na kampuni ya PAP inayomilikiwa na Harbinder Singh, ambaye kwa
sasa ndiye mmiliki pekee wa IPTL baada ya kununua hisa za Mechmar na zile za
VIP.
Mgogoro
uliosababisha fedha kuwekwa katika akaunti hiyo ya Tegeta ya BoT ulitokana na
Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kugoma kulipa gharama za uwekaji mitambo (Capacity
Charge) kwa IPTL mwaka 2006 kwa vile ilibainika IPTL ilikuwa ikitoza
gharama kubwa kuliko iliyopaswa.
Akaunti hiyo ya Tegeta ilianzishwa
kwa sababu ya kuhifadhi fedha zote zilizopaswa kulipwa na Tanesco hadi hapo
mgogoro baina ya pande hizo mbili umalizike.
Hata
hivyo, Septemba mwaka jana, serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini, iliagiza
BoT kulipa fedha hizo kwa kampuni ya PAP mara baada ya kuridhishwa na uamuzi wa
Mahakama Kuu uliosema kwamba mgogoro baina ya wamiliki wa IPTL na Tanesco
umemalizika na hivyo Benki Kuu haina sababu ya kuhifadhi fedha hizo.
Uamuzi huo wa kulipwa ulizua upinzani
mkali bungeni ambapo wabunge wawili wa kambi ya upinzani; Mbunge wa Kigoma
Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila na Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA),
Zitto Kabwe, walidai kuwa zoezi hilo limejaa ufisadi.
Hatimaye Bunge la Tanzania liliamua
kwamba suala la kutolewa fedha katika akaunti ya Tegeta lifanyiwe uchunguzi wa
kina na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) pamoja na
ile ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Chanzo hicho kinafahamu
kwamba tayari ripoti ya CAG na Takukuru imekamilika na kinachosubiriwa kwa sasa
ni utekelezaji.
Chanzo ni Gazeti la Raia Mwema
Hakuna maoni
Chapisha Maoni