WAZIRI MAGUFULI KUIFIRISI SERIKALI YA KIKWETE,SASA KUITIA HASARA YA MABILIONI YA FEDHA,NI UZEMBE WAKE UMESABABISHA
![]() |
| Pichani ni Waziri John Magufuli |
Na Kulwa Mzee, kutoka gazeti la
Mtanzania
WACHINA wa ‘samaki wa Magufuli’
walioachiwa huru wanadai meli na samaki zilizokuwamo, ambavyo vyote vina
thamani ya Dola za Marekani 3,220,000.
Mbali na kutakiwa kulipa fedha
hizo, pia inatakiwa kulipa Sh trilioni 1.3 ikiwa ni gharama zote, ikiwamo meli,
samaki, mawakili na mabaharia wake.
Hayo yalisemwa Dar es Salaam
jana na Wakili wa Wachina hao, Kapten Ibrahim Bendera na Wakili John Mapinduzi,
walipokuwa wakizungumzia hatima ya madai hayo.
“ Tunadai meli na ikiwezekana na samaki
waliokuwamo, thamani ya meli ya Tawaliq 1 kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya
Uvuvi ni Dola za Marekani milioni 2.5, thamani ya samaki zilizokuwamo ni Dola
za Marekani 720,000.
“Hivi sasa tunasubiri
maelekezo kutoka kwa wenye meli ili tuendelee na mchakato wa madai hayo, wateja
wangu wanaendelea na taratibu za kurudi kwao,” alisema Kapteni Bendera.
Wakili John Mapinduzi alisema
Serikali inatakiwa kulipa gharama zote kuanzia meli, samaki, gharama za
mawakili na mabaharia wake.
“Serikali italipa karibu Sh
trilioni 1.3, ile haikuwa meli ya kawaida, ilikuwa ni kama kiwanda, ilikuwa
inafanya kazi ya kuvua na kusindika,” alisema.
Ijumaa iliyopita Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu iliwaachia huru Wachina wa ‘samaki wa Magufuli’ na kuamuru
Jamhuri iwarejeshee vitu vyao, ikiwamo meli ya Tawaliq 1.
Wachina hao waliachiwa kwa mara ya
pili kwa vile mara ya kwanza waliachiwa na Mahakama ya Rufaa Machi
28 mwaka huu, lakini walikamatwa tena na kushtakiwa upya kwa mashtaka
hayo hayo yaliyofutwa.
Washtakiwa hao ni Nahodha wa
meli, Hsu Chin Tai na Wakala wa Meli ya Tawaliq 1, Zhao Hanquing, waliokuwa
wakikabiliwa na mashataka ya uvuvi haramu katika Ukanda wa Uchumi wa Tanzania.
Wakili wa Serikali Mwandamizi,
Prosper Mwangamila, aliwasilisha maombi ya kuifuta kesi hiyo mbele ya Hakimu
Mkazi Mfawidhi, Isaya Harufani.
“Mheshimiwa Hakimu, Jamhuri
tunaifahamisha mahakama kwamba hatuna haja ya kuendelea na kesi dhidi ya
washtakiwa, maombi yetu tunawasilisha chini ya kifungu cha sheria namba 91(1)
cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) ya mwaka 2002,” alidai
Mwangamila.
Wakili wa washtakiwa, Kapten
Ibrahimu Bendera, alikubaliana na maombi hayo na kuiomba mahakama iwarudishie
hati zao za kusafiria, meli iliyokamatwa
na
samaki waliokuwamo ikiwezekana.
Mahakama ilikubali kuwaachia
huru washtakiwa wote na kuamuru warejeshewe vitu vyao vilivyokuwa
vinashikiliwa.
Mahakama ya Rufaa iliwaachia
Machi 28 mwaka huu na kuwafutia adhabu ya kifungo cha miaka 30 na faini ya Sh
bilioni 22 waliyopewa baada ya kutiwa hatiani na Mahakama Kuu Februari 23 mwaka
2012 kwa uvuvi haramu katika Ukanda wa Uchumi wa Tanzania.
Washtakiwa hao waliachiwa baada ya
Mahakama kubaini sheria zilikiukwa wakati wa uendeshwaji wa kesi hiyo katika
mahakama za chini.
Washtakiwa waliachiwa na
kukamatwa nje ya mahakama kisha kufunguliwa kesi mpya yenye mashtaka
yanayofanana katika Mahakama ya Kisutu. Walidaiwa kwamba wote kati ya
Januari 10, 2009 na Machi 8, 2009 kwa pamoja walivua samaki bila leseni katika
Ukanda wa Bahari wa Uchumi wa Tanzania.
Katika shitaka la
pili, watuhumiwa wote walidaiwa kati ya Januari 10,
2009 na Machi 8, 2009 walichafua bahari na kuathiri viumbe vilivyomo ndani ya
bahari kinyume cha sheria.
Jamhuri ilidai shtaka la tatu
ni kwa ajili ya mshtakiwa Zhao Hanguin ambaye ni wakala wa meli.
Alidaiwa kuwa huku akijua ni
kosa kuvua samaki katika ukanda huo bila leseni, alimsaidia mshtakiwa wa kwanza
kukwepa kuchukuliwa hatua na kupata adhabu kwa kosa alilotenda.
Washtakiwa hao walikamatwa mwaka 2009 na boti ya askari wa doria
wa Tanzania, Afrika Kusini, Botswana. Leseni waliyokuwa nayo
ilikuwa imemaliza muda wake Desemba mosi, mwaka 2008.

No comments
Post a Comment