Zinazobamba

TENDWA AMSHUKIA WALIOBA KAMA MWEWE, AMTAKA AACHE TABIA YA KUTETEA RASMU YAKE YA KATIBA

 
Aliyekuwa Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa amemtaka aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba kuacha
kuitetea Rasimu ya Katiba kwa maelezo kuwa kazi yake ilikuwa ni kuiandaa na siyo kushawishi kila mtu akubaliane nayo.
 
Amesema kazi sasa imebaki kwa Bunge Maalumu la Katiba, ambalo linaijadili rasimu hiyo na kutoa mapendekezo yatakayofaa na kuyapitisha, baadaye wananchi kupiga kura ya ndiyo au hapana kupitisha Katiba Mpya.
 Isingefaa Jaji Warioba kuingia katika Bunge la Katiba na kutoa ufafanuzi kuhusu suala lolote lile. Hivi sasa hayupo katika Bunge hilo, lakini matamko anayoyatoa ni ya kuitetea,” alisema Tendwa katika mahojiano maalumu na gazeti hili.
 
Tangu Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilipotoa rasimu ya pili ya Katiba Desemba 30 mwaka jana, Jaji Warioba amenukuliwa na vyombo mbalimbali vya
habari akitoa ufafanuzi wa sababu za tume hiyo kupendekeza masuala mbalimbali, likiwemo la muundo wa serikali tatu.
 
Jaji Warioba alianza kushambuliwa kwa kasi kuanzia Machi 21 mwaka huu, baada ya kuwasilisha rasimu ya Katiba katika Bunge la Katiba.
 
Watu wa kada mbalimbali, akiwemo Rais Jakaya Kikwete walipingana na kilichopendekezwa na tume yake kwa maelezo kuwa kuna mambo yanatakiwa
kuangaliwa kwa kina, kauli ambayo kila uchwao inapingwa na Jaji Warioba, huku akisisitiza kuwa kilichomo katika rasimu hiyo kimetokana na maoni
ya wananchi.
 
Jaji Warioba ameshamaliza kazi yake ya kuandaa rasimu ya Katiba.
Anatakiwa kukaa kando na kuacha kutetea rasimu ya Katiba kwa sababu muda
wake umekwisha na sasa ni zamu ya Bunge la Katiba,”alisema Tendwa na
kuongeza;
 “Awaache wajumbe wa Bunge hilo kuichambua rasimu na siyo kuwashawishi wakubaliane na rasimu yake,” alisema msajili huyo wa zamani.
 
Tendwa pia aligusia suala la maadili ya viongozi nchini, kwamba kwa muda mrefu wameshindwa kufuata maadili na kuchukulia suala hilo kama
utamaduni wa kuheshimika wakiwa katika nafasi zao.
 
Amesema sheria ya maadili ya viongozi nayo inatakiwa kufanyiwa maboresho ili iweze kuwabana viongozi wafuate maadili.
 “Hata katika uhakiki wa mali za viongozi, wanafanya shughuli hiyo bila
utaratibu maalumu, unaweza kudhani ni maofisa za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru),” alisema Tendwa.
 
Akitolea mfano jinsi alivyosumbuliwa wakati wa ukaguzi wa mali zake, alisema sheria hiyo inatakiwa kueleza mbinu za kufanya uchunguzi wa viongozi kuliko ilivyo sasa, ambapo hata ukijua mali za kiongozi huwezikuziweka wazi.

Hakuna maoni