HUYU NDIYE WAZIRI WA JK JANGILI,VITENDO VYAKE VYA VYALIMALIZA TAIFA,SOMA HAPA KUMJUA WAZIRI HUYO
WAZIRI aliyeukwaa wadhifa huo katika
mabadiliko ya mwisho ya Baraza la Mawaziri yaliyofanyika mapema mwaka huu,
akiongoza wizara nyeti, amebainika kuratibu mtandao wa ujangili wenye mizizi
yake wilayani Manyoni na maeneo mengine mkoani Singida,
Waziri huyo (jina linahifadhiwa kwa
sasa) amekuwa na mawakala maalumu katika maeneo ya karibu na mapori
kunakoendeshwa ujangili na mara kwa mara, hufika wilayani Manyoni kuhakiki
ufanisi wa mtandao wake huo wa ujangili, huku gazeti hili likielezwa kwamba,
taarifa zake ziko ‘mikononi’ mwa vyombo muhimu vya dola nchini.
Kutoka wilayani Manyoni, mkoani
Singida, taarifa za ‘kiintelijensia’ zinafichua kwamba mtandao wa waziri huyo
unaongozwa na mfanyabiashara (jina linahifadhiwa) wa maduka ya vifaa.
Mfanyabiashara huyo ni mkazi wa kitongoji cha Mnyang’ombe mjini Manyoni na kazi
zake hizo ndani ya mtandao wa ujangili huzifanya hadi mkoani Tabora.
Inadaiwa kwamba ukaribu kati ya
mfanyabiashara huyo na waziri husika umejijengea nguvu zaidi kutokana na
umakini wake katika kufanikisha matukio ya ujangili.
Taarifa zinabainisha kwamba
mfanyabiashara huyo amekuwa na vijana maalumu ambao kazi yao ni kukusanya pembe
za ndovu kutoka katika maeneo ya Itigi, Ilangali lakini katika kituo cha
Manyoni, mfanyabiashara huyo hufanya kazi hiyo yeye binafsi.
Vijana hao (majina yanahifadhiwa
pamoja namba zao za simu), mmoja anaishi Manyoni akimiliki namba tatu za
mtandao wa aina mmoja wa simu za mkononi, mwenzake mwingine ni mwenyeji katika
vijiji vinavyopakana na Pori la Akiba Rungwa, maeneo ya Kizigo. Kijana huyo wa
Kizigo ndiye mnunuzi wa meno yote ya tembo yanayopatikana maeneo hayo kwa niaba
ya mtandao huo.
Mbali na vijana hao wawili, yupo kijana
mwingine (jina linahifadhiwa kwa sasa), huyu ni mkazi wa kijiji cha Ilangali,
naye akiwa anamiliki namba tatu tofauti za simu za mtandao mmoja wa mawasiliano
ya simu za mkononi. Kazi kubwa ya kijana huyu katika mgawanyo wa majukumu ya
kijangili ni kuhifadhi silaha sambamba na kununua meno ya tembo kwa ‘wadau’
hapo kijiji cha Ilangali na baada ya kununua meno hayo, mfanyabiashara wa
Manyoni hufika kuyachukua.
Mbinu za usafirishaji
Baada ya kazi ya ununuzi na ukusanyaji
kukamilika, meno ya tembo yaliyopatikana, husafirishwa kwa njia ya reli ya kati
chini ya usimamizi wa mfanyakazi mmoja wa Shirika la Reli Tanzania (jina
linahifadhiwa) mwenye makazi yake mjini Morogoro.
Mfanyakazi huyo husimamia usafirishaji
wa meno hayo kutoka Tabora hadi Itigi ambako hapo hupokelewa na mfanyabiashara
(wa Manyoni) ambaye huyahifadhi hapo Manyoni.
Yakiwa hapo Manyoni, meno hayo
huhifadhiwa kwa mmiliki wa mojawapo ya hoteli kubwa na maarufu mjini Manyoni,
mwenye asili ya mikoa ya kanda ya kaskazini, ambaye yeye huwasiliana na waziri
kwa ajili ya maelekezo zaidi juu ya namna ya kusafirisha meno hayo.
Taarifa za kiuchunguzi zinazidi
kubainisha kwamba mara nyingi, waziri husika hufika hapo Manyoni kwa ajili ya
kuchukua “mzigo” na kila anapokwenda huongozana na mwanamke mmoja, mwenye
lafudhi ya watu kutoka mikoa ya kanda ya kaskazini (jina linahifadhiwa).
Mwanamke huyo ndiye hutumiwa
kusafirisha meno hayo yaliyokusanywa yakiwamo ya kutoka ‘kituo’ chao cha Puma,
mkoani Singida, ili hatimaye kuyafikisha wanakokubaliana yafike.
Waziri huyo anapokuwa Manyoni amekuwa na
kawaida ya kuwakusanya washirika wake katika mtandao huo na wote hupata malazi
yao katika moja ya hoteli kubwa na maarufu hapo Manyoni.
Wakiwa hapo Manyoni na bosi (waziri)
genge hilo la kijangili hujiimarisha kiulinzi kwa kuweka watu wa kulinda hoteli
husika na hata kudadisi wageni wengine wanaofika hotelini hapo.
Katika maeneo ya Singinda, mjini Puma,
yupo kijana maalumu anayetumiwa na waziri huyo ambaye anatajwa kuwa na undugu
wa namna fulani na mteule huyo wa Rais Kikwete. Kijana huyu hutumia namba za
mitandao miwili tofauti ya simu za mkononi.
Huyu kazi yake kubwa ni kuwaunganisha
wawindaji (wenyewe majangili huita wapigaji) na wakati mwingine hutokea waziri
ndiye anayekusanya mzigo. Wakati uchunguzi huu ulipokuwa ukifanyika, kijana
huyo alikuwa na meno ya tembo yaliyokuwa yamehifadhiwa eneo la Tinde, mkoani
Shinyanga. Hata hivyo, uaminifu wa kijana huyo si mkubwa kwa sababu uchunguzi
wetu umebaini wakati mwingine ‘huchota’ mzigo kiasi fulani na kuuza kinyemela bila
mtandao kujua.
Kijana huyo, kati ya kazi
alizowahi kufanya ni kuwaunganisha baadhi ya vijana na mwindaji kutoka Wilaya
ya Igunga (jina na mawasiliano yake yanahifadhiwa). Mwindaji huyo wa Igunga
anamiliki bunduki aina ya Rifle (namba inahifadhiwa) na wakati uchunguzi wa
gazeti hili ukifanyika, alikuwa na vipande sita vya meno ya tembo ambavyo ni
sawa na meno matatu.
Kwa wakati huo tukifanya uchunguzi,
waziri husika alitoa maelekezo vijana wake wasimamishe shughuli zao kwa muda.
Huko wilayani Kahama, mkoani Shinyanga,
Waziri husika anashirikiana na mtu (jina linahifadhiwa) ambaye anafanya
biashara ya ng’ombe kama kinga ya kuficha shughuli zake za ujangili. Mtu huyu
ni mnunuzi wa meno ya tembo na hukusanya meno yanayotoka katika mapori ya
Moyowosi, Kigosi, Burigi, Biharamulo na Kimisi.
Hivi karibuni, mtu huyo amekuwa
akikusanya meno ya tembo yanayotoka Moyowosi na amekuwa na wadau wake ambao ni
watumishi wa serikali katika mapori ya Burigi na Biharamulo. Mtu huyo
amenunuliwa na waziri husika gari aina ya Rav4, kwa ajili ya kukusanya meno ya
tembo maeneo ya vijiji vinavyozunguka mapori hayo.
Katika maeneo ya Ilongelo na Ngamo,
mkoani Singida, huko waziri husika anaendesha mtandao wake wa ujangili kwa
kushirikiana na tajiri mmoja, mwenye asili ya Mkoa wa Simiyu ambaye naye anao
mtandao mkubwa unaowahusisha vigogo kadhaa, akiwamo mmoja wa wabunge aliyepata
kupigia kelele kuhusu ufisadi bungeni, zikiwamo fedha za akaunti za Uswisi,
mbunge huyu ni mwenyeji wa kanda ya ziwa na ni kijana kwa umri.
Taarifa za kiuchunguzi zinabainisha
kwamba meno ya tembo yanayokusanywa maeneo ya Singida, Kahama na Meatu
hufikishwa katika kijiji cha Ngamo ambako waziri husika akiwa na mwanamke mmoja
mkazi wa moja ya mikoa ya kaskazini ambaye ndiye mwenye jukumu la kusafirisha
meno hayo.
Mtandao wa waziri huyo umejipanua zaidi
katika operesheni za kijangili, ukihusisha Wilaya ya Babati, mkoani Manyara.
Huko Babati, katika kijiji cha Mayoka, kuna tawi la ujangili la waziri huyo.
Msimamizi wa shughuli za kijangili
eneo hilo ni mtu (jina linahifadhiwa) ambaye mara kwa mara huwapo Dodoma kila
waziri husika anapokuwa huko kwa shughuli za Bunge. Huyu mtu ndiye husimamia
ukusanyaji meno ya tembo kutoka maeneo ya Magugu na Mayoka, wakipata meno hayo
kutoka katika Hifadhi ya Taifa Tarangire na ushoroba wa Tarangire – Manyara.
Kutokana na umahiri wa kuunganisha
mitandao wa kijangili nchi nzima, waziri huyo kwa baadhi ya watu analinganishwa
na pweza au buibui kutokana na kunasa na kuunda mtandao mpana.
Chanzo ni Gazeti la Raia Mwema
Hakuna maoni
Chapisha Maoni