HUU NDIO MPANGO MKAKATI WA OFISI YA TAKWIMU ULIOWASILISHWA KWA WADAU,
Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS)
inakamilisha Mpango mkakati wa Takwimu za Kilimo wa mwaka 2014/15
mpaka 2018/19 utakaoiwezesha Ofisi hiyo kuendesha zoezi la ukusanyaji
wa takwimu za kilimo nchini kila baada ya miaka 5.
Akizungumza wakati wa mkutano
uliohusisha wadau mbalimbali wa kupitia na kujadili rasimu ya mwisho ya
mpango huo leo jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi wa
Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bw. Morrice Oyuke amesema kuwa mpango huo
utaiwezesha Ofisi ya Taifa ya Takwimu kukusanya takwimu sahihi
zinazokidhi viwango vya ndani na vile vya kimataifa.
Amesema mpango mkakati huo
unalenga kuboresha shughuli za ukusanyaji wa takwimu za kilimo hapa
nchini kwa kujenga mfumo mmoja wa utoaji wa takwimu za Kilimo kupitia
Ofisi ya Taifa ya Takwimu kuliko ilivyo sasa na kubainisha kuwa taarifa
zote za shughuli za kilimo nchini zitaingizwa kwenye mfumo wa serikali.
“Hapa tumekutana wadau
mbalimbali kutoka serikalini kwa maana ya wizara husika na
wawakilishi kutoka mashirika ya maendeleo, lengo letu ni kupitia na
kujadili rasimu hii ya mwisho itakayotuwezesha kujenga uwezo wa ndani wa
ukusanyaji wa takwimu za kilimo kuanzia ngazi ya kijiji mpaka taifa’’
Amesema
Amefafanua kuwa mpango huo
utaiwezesha Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bara na ile ya Mtakwimu Mkuu
Zanzibar kupata takwimu za shughuli zote za kilimo kuanzia wazalishaji
wenyewe, hali ya kilimo, mazao, masoko pia kutoa mwelekeo wa nini
kifanyike kuboresha sekta hizo kupitia takwimu zitakazokusanywa.
Aidha, amesema kuwa vipaumbele
vya mpango huo vimeshaainishwa na kuwekwa mbele ya wadau ili kuwezesha
upatikanaji wa nyenzo na uwezo wa kutekeleza mpango huo.
Mwakilishi wa Shirika la Chakula Duniani (FAO) nchini Tanzania Bi. Diana Tampelman akizungumza na waandishi wa habari kupongeza hatua iliyofikiwa katika kukamilisha Mpango mkakati wa Takwimu za Kilimo nchini Tanzania na kueleza kuwa hatua hiyo inaendana na Mpango wa Dunia ulioanzishwa mwaka 2010 kwa lengo la kuboresha takwimu za kilimo maeneo ya vijijini.
Baadhi ya washiriki wa mkutano wa Kijadili Mpango Mkakati wa Takwimu za Kilimo wakifuatilia masuala mbalimbali wakati wa mkutano huo leo jijini Dar es salaam.
Kuhusu kufanikisha mpango huo
Bw. Oyuke amesema kuwa jopo la taifa la wataalam limeundwa likihusisha
wataalam kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu na ile ya Mtakwimu Mkuu
Zanzibar, Wizara husika za Kilimo, Chakula na Ushirika,Mifugo na Uvuvi,
TAMISEMI, Maliasili na Utalii pamoja na wataam kutoka mashirika ya
maendeleo.
Kwa upande wake Mwakilishi wa
Shirika la Chakula Duniani(FAO) nchini Tanzania Bi. Diana Tampelman
amepongeza hatua iliyofikiwa katika kukamilisha Mpango mkakati huo
nchini Tanzania na kueleza kuwa hatua hiyo inaendana na Mpango wa
Dunia ulioanzishwa mwaka 2010 kwa lengo la kuboresha takwimu za kilimo
maeneo ya vijijini.
“Tunapongeza hatua hizi na
tutaongeza nguvu zetu katika mpango huu ili kupata uhalisia wa shughuli
za kilimo Tanzania kuhusu nani kazalisha nini na kwa kiwango gani ingawa
watu wanaweza kushindwa kuona umuhimu wake lakini tunajua kuwa taarifa
hizi ni muhimu sana kwa uchumi wa nchi” Amesema Diana.
Naye mtaalam kutoka Wizara ya
Kilimo na Maliasili Zanzibar Bw. Mzee Mohammed Mzee akiwasilisha mada
kuhusu Hali ya Takwimu za kilimo nchini amesema kuwa kwa kipindi kirefu
takwimu za kilimo zimekuwa zikipatikana kupitia Wizara na Taasisi zenye
dhamana ya usimamizi wa sekta ya kilimo na kusababisha upatikanaji wa
takwimu zinazotofautiana kutokana na njia zilizotumika wakati wa
ukusanyaji wa takwimu hizo.
“Kisheria Ofisi ya Taifa ya
Takwimu hapa nchini ndio yenye dhamana ya kukusanya na kusambaza
takwimu, suala la ukusanyaji wa takwimu lina njia zake, kumekuwa na
shida ya ya njia za ukusanyaji wa takwimu hizi na wakati mwingine
takwimu kutofautiana ,kukamilika kwa mpango mkakati huu kutaliondoa
tatizo hili” Amesema.
SOURCE FULLSHANGWE
Hakuna maoni
Chapisha Maoni