walala hoi nao kunufaika mradi wa mabasi yaendayo kasi, Jk mwenyewe kuongoza kikao hicho
Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete
anatarajia kuongoza mkutano wa mashauriano ya awamu ya kwanza ya
uwekezaji katika mradi wa mabasi yaendayo kasi (DART) utakaowakutanisha
wawekezaji wa ndani na nje Dar es Salaam.
Mtendaji Mkuu wa DART, Asteria Mlambo
alisema mwishoni mwa wiki kuwa mkutano huo utakaofanyika mapema mwezi
ujao utatoa nafasi kwa wawekezaji kuzijua fursa za uwekezaji
zitakazopatika kwenye mradi huo.
Washiriki wa mkutano huo wanatarajiwa
kutoka katika benki na taasisi mbalimbali za kifedha, kampuni za
kutengeneza mabasi, kampuni za mawasiliano, mifuko ya kijamii na
wengine.
Mada kuhusu mradi wenyewe wa DART itatolewa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Jumanne Sagini.
Kabla ya mkutano huo, DART imeandaa
mkutano wa wamiliki wa daladala Dar es Salaam, Kampuni ya Usafirishaji
Dar es Salaam (UDA) na wadau wengine ili kuwafahamisha jinsi gani
wanaweza kunufaika na mfumo huo mpya.
"Tutawaelezea faida na fursa zitakazopatikana kwenye mfumo mpya wa usafirishaji jijini," alisema Mlambo.
Mwezi uliopita Dart ilikamilisha
shughuli ya kusajili mabasi ya daladala yanayopita katika Barabara ya
Morogoro au kukatiza katika njia hiyo ikiwa ni moja ya matayarisho ya
kupisha mradi huo.
Kulingana na mpango huo wa Dart
barabara hizo za Morogoro, Kawawa na Msimbazi zitatumiwa na mabasi ya
mfumo huo pekee kwa njia 64 Dar es Salaam zitakoma kutumika kutokana na
mradi huo.(E.L)

No comments
Post a Comment