RIPOTI.WAZIRI NYALANDU AZIDI KUFANYA UASI KWA WATANZANIA SOMA KWA MAKINI UONE ALIVYOWADANGANYA WATANZANIA
Waziri wa Maliasili na Utalii,Lazaro Nyalandu akikabidhiwa Mfano wa Hundi Yenye Utata na Mkurugenzi wa Friedkin Conservation Fund, Mitchel
Allard.
BAADA ya Kuishinda
Nguvu Ikulu ya Rais Jakaya Kikwete, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro
Nyalandu, baada Ikulu hiyo kusalimu amri
kwa Waziri huyo kutokana na Kitendo cha ikulu kuwaondoa kwenye Nyadhifa zao
Wakurugenzi wa Wanyama Poli,Profesa Alex Songorwa na Japhari Kidegesho
Hivi leo Usanii wa
kisiasa unaofanywa na Waziri huyo wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu,
unazidi kubainika baada ya rafiki zake kumkabidhi hundi hewa ya dola milioni
2.25 za Marekani.
Kiasi hichocha fedha kwa
mwaka jana kilikuwa sawa na Sh bilioni 3.668.
Waziri huyo, kwa
kushirikiana na rafiki zake wa Kampuni ya Friedkin Conservation Fund
inayojihusisha na masuala ya uwindaji wa kitalii, na wanaojitangaza kama wadau
wanaopinga ujangili walikabidhiana mfano wa hundi hiyo feki wakati wa kilele
cha matembezi yaliyopewa jina la “Walk for Elephant” yaliyoshirikisha watu 18
kutoka Arusha hadi Dar es Salaam (umbali wa kilometa zaidi ya 600).
Nyalandu alipokea mfano
huo wa hundi kutoka kwa Mkurugenzi wa Friedkin Conservation Fund, Mitchel
Allard. Matembezi yaliratibiwa na asasi ya African Wildlife Trust, inayoongozwa
na Pratik Patel. Huyu ni mmoja wa watu wanaozunguka huku na huko ulimwenguni
kukusanya fedha kwa madai ya kuzitumia kuwahami tembo dhidi ya majangili.
Patel anatajwa kuwa
mmoja wa marafiki wa karibu mno wa Nyalandu, na ambaye wakati mwanasiasa huyo
akitangazwa kuwa Waziri kamili, hakusita kuonesha furaha yake kwa kuwakusanya
“Friends of Nyalandu” mjini Arusha kusherehekea uteuzi huo uliofanywa na Rais Jakaya
Kikwete.
Pamoja nao, wengine
walioshuhudia kituko hicho ni Meneja Maendeleo ya Jamii kutoka Friedkin Group
of Companies, Aurelia Mtui; Faraja Nyalandu; Nancy Sumari na Mkurugenzi wa
Idara ya Wanyamapori, Profesa Alexander Songorwa.
Pamoja naye, alikuwapo
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James
Lembeli. Kwa siku za karibuni Lembeli na Nyalandu wamekuwa marafiki wakubwa,
kiasi cha kujipanga kuyashitaki magazeti wanayoyatuhumu kuhoji urafiki wao.
Miongoni kwa mambo yaliyowaudhi
ni kutibuliwa kwa mpango wa kukodishwa kwa Hifadhi ya Taifa ya Katavi kwa
kampuni ya African Parks Network (APN) ya Afrika Kusini ambayo Nyalandu ni
mjumbe wa Bodi. Hasira zao sasa wanataka kuzihamishia mahakamani kwa kile
kinachoelezwa kuwa ni mkakati wa kuwafunga mikono wanahabari wanaofukua tuhuma
mbalimbali ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii.
Akiwa Naibu Waziri
wakati huo, alipokea matembezi hayo kuanzia Ubungo na kuyahitimisha katika
Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini humo. Watembezi hao walitumia siku 19.
Uchunguzi uliofanywa na
Gazeti hilo linalotoka mala
moja kwa wiki umebaini kuwa baada ya hafla kubwa iliyotangazwa kwa
mbwembwe katika vyombo vingi vya habari, Wizara ya Maliasili na Utalii
ilijaribu kupata fedha hizo, ndipo ilipobainika kuwa kilichofanywa na hao
waliojiita ‘wafadhili’ kilikuwa kiini macho tu!
Baadaye ikabainika kuwa
hundi hiyo ilitolewa na kampuni hiyo ya Friedkin na kupelekwa kwa kampuni yake
nyingine, huku Nyalandu akitumika kujipatia umaarufu kwa “kufanikisha” kupata fedha
za kuiwezesha Serikali kwenye mapambano dhidi ya ujangili!
Hadi wiki iliyopita,
Wizara ilikuwa haijapata hata dola moja kutokana na hundi hiyo. Mmoja wa
watumishi amesema misaada kadhaa kati ya mingi inayotangazwa na kuoneshwa kwa
mbwembwe kwenye vyombo vya habari ni usanii tu.
“Wengi wanatumia njia
hii kujipatia umaarufu na kunyoosha masuala yao. Nyalandu ni rafiki mkubwa wa
kampuni hii. Alishiriki kuafiki wazo la matembezi hayo kama njia ya kuonesha
ana uwezo wa kushawishi na kufanikisha kupata fedha kwa ajili ya kupambana na
ujangili. Lengo lake lilikuwa kujiandalia mazingira ya kuwa Waziri,” amesema
mmoja wa watumishi kwa masharti ya kuhifadhiwa jina lake.
Msemaji wa Wizara ya
Maliasili na Utalii, Nurdin Chamuya, alipoulizwa kwa simu alisema, “Nitakupigia,
nipo benki kidogo.” Hata hivyo, hakupiga simu. Alipotafutwa, simu iliita bila
kupokewa.
Kwa upande wake,
aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, alipoulizwa,
alisema, “Jamani naomba mniache kwa sababu mimi si Waziri tena…Waulizeni
waliopo.”
Alipoulizwa zaidi
alisema, “Sina kumbukumbu sawa sawa za suala hilo, lakini nadhani hizo fedha
hatukuziona, pengine zililetwa nikiwa nimeshaondoka wizarani.”
Urafiki wa Nyalandu na kampuni
za Friedkin Conservation Fund ni wa wazi, na sasa Waziri anajitahidi
kushinikiza mmoja wa Watanzania wenye asili ya Kiarabu anyang’anywe kitalu ili
zipewe kampuni hizo za Kimarekani.
Limekuwa jambo la
kawaida kwa kampuni hiyo na nyingine zenye uhusiano nayo, kushinikiza mambo
yafanyike bila kufuata sheria na taratibu mradi tu jambo wanaloshinikiza lina
maslahi kwao.
Pale wanapokataliwa
wamekuwa na tabia ya kusingizia Idara ya Wanyamapori au watumishi kuwa
wanawanyanyasa na kwamba wanapokea rushwa.
Wanapata kiburi kutoka
kwa Nyalandu na wanasiasa wengine wanaohaha usiku na mchana kuhakikisha wazawa
wananyang’nywa vitalu ili wao wapewe.
Baadhi ya watumishi
wamekuwa waoga wanapokabiliana na madai ya kampuni hizo, hasa wanapotakiwa
watekeleze maagizo bila kufuata misingi ya Sheria ya Wanyamapori Namba 5 ya
mwaka 2009 na kanuni zake za mwaka 2010.
Mifano michache juu ya
tabia hii ni pamoja na mgogoro wa Lake Natron Game Controlled Area ambako
Kampuni ya Wengert Windrose Safaris (WWS) imekuwa ikilazimisha Idara ya
Wanyamapori kuipa kitalu ambacho kiligawiwa kwa kampuni ya Green Miles Safaris
(GMS).
Msimamo wa Wizara na
baadaye hukumu ya Mahakama ni kwamba madai ya marafiki hao wa Nyalandu hayana
msingi.
Hata hivyo, WWS ambao
ndiyo hao hao Friedkin Conservation Fund, waliandika barua kwenda Baraza la
Congress la Marekani kulalamika kwamba watumishi wa Idara wamekula rushwa na
kutoa kitalu chao kwa Kampuni ya GMS ambayo ni ya Kitanzania. Wabunge karibu 20
walitia saini barua kwenda kwa Rais Barack Obama, wakitaka aingilie kati ili
WWS wapewe vitalu wanavyovitaka.
Uchunguzi unaonesha
kuwa baada ya madai hayo kuchunguzwa na Serikali ya Marekani, ilibainika kuwa
ni ya kipuuzi, na hivyo kampuni hiyo ikatakiwa iombe radhi Idara ya Wanyamapori
na Serikali ya Tanzania. Serikali ya Marekani ikasema wazi kuwa kampuni hiyo,
na nyingine zinapaswa kufuata sheria na kanuni za Tanzania. Hadi sasa maswahiba
hao wa Nyalandu hawajaomba radhi kama walivyotakiwa na Serikali ya Marekani.
Kampuni ya WWS imekuwa
ikiendelea kufanya fujo kwa wageni wa GMS, hivyo kusababisha wageni hao
kuondoka na wengine kufuta safari zao. Hali hii imesababisha Serikali kukosa
mapato kwa kuwa shughuli za uwindaji hazikufanyika kabisa katika kitalu hiki.
Baada ya Nyalandu kuona
mbinu za kuwaondoa wazawa hao ni ngumu, na hasa baada ya wakurugenzi
aliowafitini kumwekea ngumu, sasa ameibuka kwa njia nyingine ya Bunge.
Msemaji wa Kambi Rasmi
ya Upinzani Bungeni wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Peter Msigwa, anatajwa
kama mmoja wa wanasiasa walioanza kupiga zengwe ili kampuni ya GMS iweze
kuondolewa kwa madai kwamba inaua wanyama bila kufuata sheria.
Hii ni habari njema kwa
Nyalandu ambaye kwa kutumia maneno ya Msigwa, anaweza kuhalalisha kufutwa kwa
leseni ya GMS, hivyo kufungua njia kwa rafiki zake Wamarekani wa kampuni za WWS
na nyingine kulitwaa eneo hilo lenye utajiri mkubwa wa wanyamapori.
Msigwa
ahoji Sarakikya kuendelea kupeta
Kuna habari kwamba Paul
Sarakikya ambaye ameonekana kufeli kwenye vita dhidi ya ujangili, ndiye
aliyeandaliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Wanyamapori.
Hata hivyo, Msigwa
amehoji weledi na uadilifu wa Sarakikya hata Nyalandu aweze kumpa nafasi ya
kukaimu nafasi ya Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, kabla ya kuondolewa na
mamlaka ya uteuzi.
Katika hotuba yake
bungeni, Msigwa alisema, “Mheshimiwa Spika, Waziri Nyalandu alitoa taarifa za
kuwavua nyadhifa zao Mkurugenzi Mkuu wa Wanyamapori na Mkurugenzi Msaidizi,
Idara ya Matumizi Endelevu ya Wanyamapori nyadhifa zao. Nyalandu anadai kuwa
moja ya sababu za kuwaondoa ni kutekeleza maazimio ya Kamati ya Lembeli
kutokana na kutowajibika wakati wa Operesheni Tokomeza.
“Jambo la kujiuliza,
kama aliwahi kusema kuwa taarifa ya kamati ni uongo mtupu, je, ni lini
amethibitisha kuwa kile alichodai kwamba ni uongo, ulikuwa ukweli?
“Cha ajabu,
aliyeteuliwa kukaimu nafasi ya ukurugenzi, Paul Sarakikya aliyekuwa kiongozi wa
utekelezaji wa Operesheni Tokomeza na aliyehusika moja kwa moja na kinachodaiwa
kuwa uvunjifu wa haki za binadamu, ndiye amepewa nafasi ya kukaimu ukurugenzi!
Wote tunafahamu ukiukwaji mkubwa wa haki za binaadamu na ukatili uliofanywa
katika Operesheni Tokomeza kiasi cha kusababisha mawaziri wanne kuwajibishwa
kwa kutenguliwa nafasi zao.
“Mheshimiwa Spika,
aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kueleza ilitumia vigezo gani
kumteua Sarakikya kukaimu nafasi ya Ukurugenzi wa Wanyamapori huku ikijua
alivyoshindwa kutokomeza ujangili hapa nchini na jinsi alivyoendesha Operesheni
Tokomeza iliyokuwa imejaa dhuluma, uporaji, utesaji na udhalilishaji dhini ya
wananchi. Jambo ambalo liliishangaza zaidi Kambi Rasmi ya Upinzani ni kitendo
cha Waziri Nyalandu kumteua Ndugu Sarakikya kukaimu nafasi ya Mkurugenzi wa
Wanyamapori huku akijua kuwa Sarakikya alifanya makosa mengi katika utendaji
wake wa kazi katika Idara hiyo ya Wanyamapori.
“Mheshimiwa Spika,
ikumbukwe pia kuwa Ndugu Sarakikya ndiye aliyeongoza Kikosi cha Kuzuia Ujangili
hata kabla ya Operesheni Tokomeza. Katika kipindi hicho, Tanzania ilishika
nafasi ya kwanza kati ya nchi nane duniani zilizoongoza kwa matukio ya ujangili.
Aidha, ili kuonyesha kwamba Serikali hii haizingatii weledi katika utendaji,
alietuliwa tena kusimamia Operesheni Tokomeza.”
Habari hii Imeandikwa na Mwandishi wa Mtandao huu Karoli Vinsent na Kusaidiwa
kwa Kiwango kikubwa na Gazeti la Jamhuri
No comments
Post a Comment