HIVI NDIVYO TIBAIJUKA ALIVYOAIBIKA MBELE YA WANANCHI WA MBARALI, AZOMEWA MCHANA KWEUPE

Mkurugenzi Mtendaji wa Kapunga Rice Project Limited, Justin Vermaak
akizungumza na Waziri wa Ardhi , Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Prof
Anna Tibaijuka, alipotembelea shamba hilililopo Wilayani Mbarali,
Mkoani Mbeya juzi.Picha na Mpiga Picha Wetu
Na Lauden Mwambona, Mwananchi
Mbeya.Waziri wa Ardhi, Nyumba
na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka alipata wakati mgumu juzi
jioni baada ya kuzomewa na wananchi waliokerwa na kitendo chake cha
kubadilika na kumruhusu mwekezaji kuendelea kumiliki eneo la ardhi
katika Shamba la Kapunga, Wilaya ya Mbarali, Mbeya.
Ilibidi Mkuu wa Wilaya hiyo, Gulam Hussein Kifu
aingilie kati kuwatuliza wananchi hao waliokuwa wakipiga kelele na kutoa
maneno makali kwa waziri huyo.
Profesa Tibaijuka alikwenda huko kwa nia ya
kusuluhisha mgogoro wa ardhi wa muda mrefu baina ya wananchi wa Kapunga
na mwekezaji wa Kampuni ya Kapunga Rice Project. Awali, shamba hilo
lilikuwa mali ya Kampuni ya Taifa ya Kilimo (Nafco).
Wananchi hao walikasirishwa na hatua yake ya
kuamua kuwa eneo hilo ni halali kwa mwekezaji huyo tofauti na msimamo
wake wa awali wa kutaka ardhi hiyo irudishwe kwa wananchi.
Profesa Tibaijuka alibadili mawazo yake baada ya kufanya mazungumzo na mwekezaji huyo ndani ya gari akiwa na Mkuu wa Wilaya.
Msimamo awali
Profesa Tibaijuka alifika Kijiji cha Kapunga saa
6.45 mchana na kuanza kikao cha ndani na viongozi wa kijiji kwenye ofisi
yao hadi saa 8.14 mchana. Alielezwa alielezwa kwamba mgogoro huo
unatokana na kitendo vya mwekezaji huyo kutaka kupora ardhi yote ya
kijiji chenye wakazi wapatao 4,400.
Mwenyekiti wa Kijiji, John Nyoni alisema mwaka
1995, wanakijiji walitoa hekta 5,500 za ardhi kwa Nafco ambazo ziko
kwenye mradi maalumu wa kuendelea kilimo cha mpunga, lakini
wanachoshangaa ni kuona aliyerithi eneo hilo (mwekezaji) anadai hekta
nyingine 1,870 kutoka kwenye mashamba ya wananchi pamoja na kijiji
chote.
Nyoni alidai kuwa katika harakati hizo, mwekezaji
huyo alipokonya shule, zahanati ya kijiji na sasa anataka kuwaondoa
wananchi wote. Akizungumza katika kikao hicho, Profesa Tibaijuka alisema
alifika hapo kutoa jawabu la suluhisho na kwamba atakachotoa ni cha
mwisho wala hakutakuwa na mgogoro mwingine tena.
“Serikali imetambua chanzo cha makosa ni Nafco
kusajili na kupata hati moja kwa eneo lote likiwamo la kijiji pamoja,
hivyo mwekezaji huyo alikabidhiwa hati hiyo ikionyesha eneo la hekta
7,370 badala ya hekta 5,500,’’ alisema Profesa Tibaijuka.
Aliwahakikishia viongozi wa kijiji hicho chenye
vitongoji saba kwamba alifika hapo ili kumtaka mwekezaji akabidhi hati
hiyo serikalini ili ofisi yake ikaibadilishe na kwamba kama atakataa
atamwandikia Rais Jakaya Kikwete kumtaka aifute hati yote.
No comments
Post a Comment