Baraza la mawazi laiva....Mawaziri, wabunge waitwa Dar, Dk. Nchimbi, Kagasheki wamo

RAIS
Jakaya Kikwete anatarajia kuipanga upya safu ya Baraza lake la Mawaziri
wakati wowote, huku baadhi ya wabunge na mawaziri wakitakiwa kusitisha
mapumziko yao ya mwisho wa mwaka na kurejea jijini Dar es Salaam haraka.
Miongoni
mwa wabunge waliositisha mapumziko yao na kurejea nchini ni aliyekuwa
Waziri wa Mambo ya Ndani, Emmanuel Nchimbi, aliyekuwa nchini Afrika
Kusini na aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis
Kagasheki, aliyekuwa Uswisi.
Wabunge
hao walipoteza nafasi zao za uwaziri baada ya ripoti ya Kamati ndogo ya
Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, kuwagusa mawaziri hao kwamba
walishindwa kuwajibika katika utekelezaji wa Operesheni Tokomeza
Ujangili.
Dk.
Nchimbi anapewa nafasi ya kurejea kwenye Baraza la Mawaziri kutokana na
kushiriki kwake kuipinga operesheni hiyo, ambayo kwa kiwango kikubwa
ilikuwa chini ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, na kwamba
alishawahi kumuandikia barua Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, akiipinga.
Kwa
upande wake Kagasheki, anatajwa kurudi kwenye Baraza la Mawaziri
kutokana na kubainika kwamba hakuwa na kosa na kwamba operesheni hiyo
ilitekelezwa zaidi kijeshi na haikuwa chini ya wizara yake moja kwa
moja.
Aidha
Kagasheki anatajwa kuwa mmoja wa waliokuwa mawaziri hodari kutokana na
uwezo wake wa kufuatilia mambo, ambapo akiwa ndani ya Wizara ya
Maliasili na Utalii, alianza harakati za kukomesha biashara haramu ya
pembe za ndovu.
Wakati
Kagasheki na Dk. Nchimbi wakipewa nafasi ya kurejea kwenye Baraza la
Mawaziri, pia zipo taarifa kwamba wapo baadhi ya wabunge wataingia kwa
mara ya kwanza kwenye baraza hilo, huku wengine wakirudishwa kwa mara ya
pili.
Taarifa
za uhakika kutoka kwa watu wa karibu wa baadhi ya wabunge, zimebainisha
kwamba jana Rais Kikwete aliwaita Ikulu wabunge wawili vijana, hata
hivyo haikujulikana waliitwa kwa sababu gani.
Baadhi
ya wabunge wanaotajwa kujumuishwa kwa mara ya kwanza kwenye baraza hilo
ni Mbunge wa Nzega, Dk. Hamis Kigwangala, Mbunge wa Iramba Magharibi,
Mwigulu Nchemba na Mbunge wa Kahama, James Lembeli, sambamba na mmoja wa
wabunge vijana kutoka mikoa ya Iringa na Njombe.
Wakati
wabunge hao wakiitwa Ikulu, zipo taarifa za uhakika kwamba mawaziri
wote wametakiwa kusitisha mapumziko yao ya mwisho wa mwaka na kurejea
Dar es Salaam.
Hatua
hiyo ya kutajwa kwa baadhi ya wabunge kuingia kwenye Baraza la Mawaziri
imewatia hofu baadhi ya mawaziri, hasa wale walionyooshewa vidole na
chama chao kwamba ni mawaziri mizigo.
Mawaziri
waliotajwa na CCM kuwa ni mizigo wamekuwa hawana matumaini ya kurejea
kwenye baraza hilo na kwamba wanaamini wao ndio watakuwa wa kwanza
kutemwa.
Wakati
baadhi ya mawaziri wakiwa na hofu, zipo taarifa kwamba mmoja wa wabunge
wanaotoka Mkoa wa Mbeya ameshaanza kufanya sherehe, akiamini kwamba
amejumuishwa kwenye Baraza la Mawaziri.
Aidha imebainika kwamba wapo baadhi
ya manaibu waziri wameshaanza kujipigia debe ili kupandishwa na kuwa
mawaziri kamili.
Mchakato
huo wa kujipigia debe unachagizwa na utaratibu wa Rais Kikwete wa
kuwapandisha hadhi manaibu waziri kuwa mawaziri kamili.
Tayari
baadhi ya Manaibu Waziri kama Amos Makala, Lazaro Nyalandu na January
Makamba, Aggrey Mwanri na Angela Kairuki, wameshaanza kutajwa kuwa
wanastahili kuwa mawaziri kamili.
Naibu
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, anatajwa kuwa
miongoni mwa Manaibu Waziri wanaoweza kusalia kwenye Baraza la Mawaziri,
kutokana na utendaji wake, lakini hawezi kupandishwa hadhi kutokana na
makosa madogo aliyowahi kuyafanya, kama vile kushindwa kutofautisha nchi
ya Zambia na kisiwa cha Zanzibar, hali iliyoonesha kuishushia hadhi
Serikali ya Rais Kikwete, kwa kuwa na kiongozi asiyejua historia na
jiografia ya nchi yake.
Utamaduni wa kupandisha manaibu
waziri
Dhana
ya manaibu waziri hao kupandishwa inatokana na hatua ya Rais Kikwete
kuwahi kuwapandisha Dk. Nchimbi, aliyekuwa Naibu Waziri wa Wizara ya
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo na Naibu Waziri wa Wizara ya Ulinzi
na Jeshi la Kujenga Taifa.
Aidha
Ezekiel Maige kabla ya kupandishwa kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii,
alikuwa naibu waziri wa wizara hiyo, wakati huo ikiwa chini ya Shamsa
Mwangunga.
Balozi
Kagasheki kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii,
alikuwa naibu waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Mara
baada ya Rais Kikwete kuingia madarakani, mwaka 2006 alimpandisha
aliyekuwa Naibu Waziri wa Maji na Mifugo wakati wa Serikali ya Awamu ya
Tatu, Anthony Diallo, kuwa Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Mifugo.
William
Ngeleja, aliyekuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, alipandishwa
hadhi na kuwa waziri kamili wa wizara hiyo, kabla ya kutemwa kwenye
mabadiliko ya mawaziri yaliyofanyika Mei, mwaka 2013.
Aidha Waziri wa sasa wa Uchukuzi, Dk
Harrison Mwakyembe, awali alikuwa Naibu Waziri wa Ujenzi.
Dk.
Cyril Chami, ambaye ameanza kupigiwa chapuo la kurejea kwenye baraza
jipya, kabla ya kupandishwa hadi kuwa Waziri wa Wizara ya Viwanda na
Biashara na kutemwa mwaka 2012, alianzia kwenye unaibu waziri kwenye
wizara hiyo.
Mawaziri
wengine ambao walianzia kwenye nafasi ya unaibu waziri ni Celina
Kombani, ambaye kabla ya kuwa waziri kamili wa Wizara ya Nchi, Ofisi ya
Rais (Utumishi), alikuwa Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (Tamisemi).
Kwa
upande wake, aliyekuwa Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Mifugo, Dk
Mathayo, kabla ya kupewa nafasi hiyo alianzia kwenye nafasi ya Naibu
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika.
Historia
hiyo ya Rais kuwapa hadhi manaibu waziri kuwa mawaziri inatoa nafasi
kwa manaibu wengi kuamini kuwa huenda wakapandishwa, hata hivyo hali ni
tofauti kwa Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Makongoro Mahanga, ambaye
amekosa bahati ya kupandishwa kuwa waziri kamili, ingawa ni mmoja wa
manaibu waziri wa muda mrefu waliozunguka kwenye wizara mbalimbali.
Dk. Migiro na uwaziri
Kwa
upande wake, Dk. Asha-Rose Migiro anapewa nafasi kubwa ya kuwemo kwenye
Baraza la Mawaziri, kutokana na historia ya Rais Kikwete ya kutoa
nafasi ya uwaziri kwa watu anaowateua kuwa wabunge, ambapo kwenye idadi
ya wateule wake nane, tayari watano amewapa nafasi ya uwaziri.
Wabunge
hao ni Shamsi Vuai Nahodha, aliyekuwa akiongoza Wizara ya Ulinzi na
Jeshi la Kujenga Taifa, Profesa Makame Mbarawa, anayeshikilia Wizara ya
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia.
Wateule
wengine wa Rais kwenye ubunge ambao wameteuliwa kuwa mawaziri ni
Profesa Sospeter Muhongo, anayeshikilia Wizara ya Nishati na Madini,
Saada Mkuya na Janet Mbene, ambao ni manaibu waziri wa Wizara ya Fedha.
Wakati
Dk. Migiro na wabunge wengine wakipewa nafasi ya kuwemo kwenye Baraza
la Mawaziri, joto linabaki kwenye nani atakwenda wizara gani.
Wizara
zinazoonekana kuwa ni mtihani kwa Rais Kikwete kumpa mtu sahihi ni
Wizara ya Fedha, ambayo inashikiliwa na Dk. William Mgimwa, ambaye kwa
sasa ni mgonjwa.
Hata
hivyo, Dk. Abdallah Kigoda, anayeshikilia Wizara ya Viwanda na Biashara
kwa sasa, anatajwa kuweza kuimudu wizara hiyo, huku Zakia Meghji
akitajwa kuwa na nafasi kubwa ya kurudi kwenye Baraza la Mawaziri, ili
kuiongoza Wizara ya Maliasili na Utalii.
Dk.
Migoro anapewa nafasi ya kurejea kwenye wizara yake ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, huku Bernad Membe, anayeshikilia wizara hiyo,
akipewa nafasi ya kurudishwa Wizara ya Mambo ya Ndani, aliyoihudumia kwa
kipindi kifupi akiwa naibu waziri wa wizara hiyo.
Uteuzi wa nafasi ya uwaziri kimikoa
Kama
Rais Kikwete ataendeleza utaratibu wake wa kuchagua mawaziri kulingana
na mikoa yao na kuamua kutomrejesha Nchimbi kwenye Baraza la Mawaziri,
anaweza kuteua mmoja kati ya wabunge hawa, Mbunge wa Viti Maalumu,
Mhandisi Stella Manyanya, Jenister Mhagama (Peramiho), Vita Kawawa
(Namtumbo) au Mhandisi Ramo Makani (Tunduru Kaskazini) ili kujaza nafasi
ya Nchimbi.
Endapo
Kagasheki hatarejea, ni wazi turufu ya kuwemo kwenye Baraza la Mawaziri
inaweza kumuangukia Jason Rweikiza (Bukoba Vijijini), Charles Mwijage
(Muleba Kaskazini), Deogratius Ntukamazina (Ngara) au Asumpta Mshama
(Nkenge).
Nafasi
ya Dk. David Mathayo, huenda ikawa kaa la moto kwa Rais Kikwete kufanya
maamuzi ya kumpata mtu sahihi, kwani idadi ya wabunge wa Mkoa wa
Kilimanjaro ni ndogo na kwamba wengi wao wameshashikilia wizara,
ukimuondoa Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela, ambaye
wachambuzi wa masuala ya siasa hawampi nafasi sana ya kuingia kwenye
Baraza la Mawaziri.
Kauli ya Ikulu
MTANZANIA
Jumatano lilimtafuta Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi, Premi
Kibanga, ili kujua ukweli wa habari hizo, lakini alisema hajui chochote.
“Mimi niko Tanga, sijui
kinachoendelea,” alisema Kibanga kwa kifupi, alipozungumza kwa simu na
Mtanzania.
No comments
Post a Comment