MAWAZIRI MIZIGO KIKAANGONI DODOMA, WAANZA KUHOJIWA NA KAMATI KUU CHINI YA MWENYEKITI WAKE RAISI JAKAYA MRISHO KIKWETE
Dodoma. Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM chini ya Mwenyekiti wake
Rais Jakaya Kikwete, imeanza kuwahoji mawaziri waliotajwa ni ‘mzigo’ kwa
Serikali.

Rais Kikwete akiendesha kikao cha
baraza la Mawaziri siku za hivi karibuni. Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu
ya CCM chini ya Mwenyekiti wake Rais Jakaya Kikwete, imeanza kuwahoji
mawaziri waliotajwa ni ‘mzigo’ kwa Serikali. Picha na Maktaba
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, jana alilithibitishia gazeti dada la Mwananchi, The Citizen juu ya kuanza kwa kikao cha Kamati Kuu (CC), lakini hakuwa tayari kuingia kwa undani kuhusu ajenda.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, jana alilithibitishia gazeti dada la Mwananchi, The Citizen juu ya kuanza kwa kikao cha Kamati Kuu (CC), lakini hakuwa tayari kuingia kwa undani kuhusu ajenda.
Hata hivyo, habari za ndani zilieleza kwamba miongoni mwa ajenda kuu za
CC ni kuwahoji mawaziri wanaolalamikiwa na wananchi, kwamba wameshindwa
kutekeleza majukumu yao.
Wakiwa Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, Nape aliwatupia lawama mawaziri
wakati akielezea changamoto zinazowakabili wakulima ambao ni asilimia
80 ya Watanzania, huku mawaziri husika wakikaa kimya.
Mawaziri waliotajwa mzigo ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk
Shukuru Kawambwa; Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher
Chiza na Naibu wake, Adam Malima, kwamba wameshindwa kazi na
alipendekeza wang’olewe.
Hata hivyo, gazeti hili jana lilishuhudia mawaziri kadhaa wakifika na
kuingia kwenye mkutano wa CC, taarifa zingine zilisema mawaziri
waliofika kwenye kikao hicho walihojiwa na wajumbe wa CC.
Kuhojiwa na CC
Mawaziri waliohojiwa na CC hadi kufikia saa 8:00 mchana jana walitajwa
kuwa ni Naibu Waziri wa Fedha, Saada Mkuya na Waziri wa Kilimo, Chakula
na Ushirika, Christopher Chiza. Mkuya ndiye ambaye kwa sasa anaisimamia
Wizara Fedha kutokana na Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa kulazwa
nchini Afrika Kusini akisumbuliwa na maradhi ambayo hayajatajwa.
Waandishi wa gazeti hili jana waliwashuhudia takriban mawaziri 10
wakiingia katika ofisi za makao makuu ya CCM, Dodoma, maarufu White
House, huku baadhi wakiwa si wajumbe wa CC.
Habari zilizotufikia jioni ziliwataja wengine kuwa ni Dk David Mathayo
David (Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi), Hawa Ghasia (Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa-Tamisemi), Dk Kawambwa, Celina Kombani (Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma).
Dk Kawambwa wakati akitoka kwenye kikao cha CC aliulizwa na waandishi wa
habari kilichotokea na yeye alijibu kwa kifupi; “Mawaziri mizigo ndiyo
tunatoka.”
Mawaziri ambao si wajumbe wa CC ni Mkuya, Chiza, Dk Kawambwa, Hawa
Ghasia na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais anayeshughulikia Utawala Bora,
George Mkuchika ambaye naye taarifa zilidai alihojiwa.
Azimio la Bunge
Tayari Bunge limepitisha azimio la kumtaka Ghasia pamoja na naibu
mawaziri wake wawili, Aggrey Mwanry na Majaliwa Kassim Majaliwa, kupima
na kutafakari kama bado wanatosha kusimamia wizara hiyo.
Kiini cha Bunge kupitisha azimio hilo ni taarifa ya Kamati ya Bunge ya
Hesabu za Serikali kubainisha kuwapo wizi, ubadhirifu na mtandao wa
ufisadi ndani ya Tamisemi, Halmashauri na Hazina.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ambaye baadhi ya wabunge wamemtaja kama
waziri mzigo namba moja, amesema yuko tayari kuachia ngazi kama Rais
ataamua kumwondoa katika wadhifa huo.
Pinda alitoa kauli hiyo juzi bungeni mjini Dodoma wakati akijibu swali
la papo kwa hapo kutoka kwa Mbunge wa Viti Maalumu, Rukia Ahmed (Cuf)
aliyetaka aeleze anajisikiaje kuitwa mzigo namba moja.
Akijibu swali hilo, Pinda alisema yeye anasimamia wizara 20, hivyo kama
wapo watakaomhukumu kwa sababu ya wizara moja ama mbili kutofanya vizuri
basi watu hao watakuwa hawamtendei haki.
Alisema kama Rais atamwona ameshindwa kuwajibika yuko tayari kuachia
ngazi na endapo Rais hatafanya hivyo na wabunge bado wakaona ipo haja
hiyo, wampigie kura ya kutokuwa na imani naye.
Kauli ya CCM
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, mbele ya Katibu Mkuu wa
chama hicho, Abdulrahman Kinana, alisema kuwa mawaziri hao wameshindwa
kutimiza wajibu wao wa kuwatumikia Watanzania.
Alisema kuwa Waziri Chiza na Malima wamebaki wakifunga tai na kuvaa suti
mjini wakati wakulima wa Ruvuma na mikoa mingine ya Tanzania
wakiteseka.
Nape alisema Waziri Kawambwa naye anatakiwa kuchukuliwa hatua kwa
kuingia mkataba na kampuni ya ujenzi ya Progressive iliyopewa zabuni ya
kutengeneza barabara ya Namtumbo hadi Tunduru wakati mkandarasi huyo
hana uwezo wa kuijenga na matokeo yake amefukuzwa kazi.
Dk Kawambwa ametupiwa lawama hizo kutokana na kuipa kazi kampuni hiyo
wakati akiwa Waziri wa Miundombinu pamoja na kushindwa kusimamia elimu.
“Katibu Mkuu (Kinana), nilimuuliza Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Chiza na
Malima wamefika lini kusikiliza matatizo ya wakulima wa tumbaku, korosho
na mahindi, alinijibu hakumbuki kama wamefika mkoani hapa. Nikafuatilia
na kubaini si yeye tu hata Waziri aliyetangulia Profesa Jumanne
Maghembe naye hakuwahi kufika. Najiuliza sababu nini, hakuna majibu,”
alisema Nape.
Alisema anasikitishwa na kitendo cha mawaziri hao waliopewa dhamana
kushindwa kutambua wajibu wao na kwamba umefika wakati wa kuhojiwa na
Kamati Kuu (CC) ya CCM, ili wachukuliwe hatua kwani bila kufanya hivyo
aibu itarudi kwa chama chake.
Wabunge wajitosa
Kikao hicho cha CC kinafanyika huku kikiwa na taarifa kwamba wabunge wa
chama hicho tawala wameanza kukusanya saini za wabunge, ili kushinikiza
kuitishwa kwa kikao cha wabunge hao au Party Cocas.
Uchunguzi wa gazeti hili, uliofanywa kwa siku kadhaa mjini hapa,
umebaini kuwa wabunge wa CCM zaidi ya 160 wametia saini katika fomu hiyo
wakiwamo mawaziri zaidi ya 10.
Chanzo kimoja cha kuaminika kilisema kuwa fomu hiyo iliwasilishwa katika
ofisi ya katibu wa wabunge wa CCM, ikiambatana na barua inayotaka
kuitishwa kwa kikao kitakachowakutanisha.
“Tuliwaomba waitishe kikao cha wabunge wa CCM ili mawaziri ambao
tunawaona hawatimizi majukumu yao kikamilifu waweze kuhojiwa lakini
wakawa wanasuasua,”kilisema chanzo hicho.
“Lakini mmoja wetu akasema kwa kuwa wamepiga chenga ya kukiitisha basi
kuna nafasi ya kikanuni ya kukusanya saini za wabunge zaidi ya nusu
kushinikiza kuitishwa kwa kikao,”alisema mbunge huyo.
Taarifa ya ziada na Habel Chidawali
Mbunge mwingine wa CCM alisema katika kikao hicho wabunge walitaka
kukutanishwa kwa pamoja kati yao, mawaziri wanaoonekana kuwa mzigo na
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana.
“Kikao hicho tulitaka kiwe Desemba 12 mwaka huu ili tuanze kuwahoji
mawaziri kabla ya CC lakini Mwenyekiti (Mizengo Pinda), amekuwa akipiga
danadana hadi leo (jana) inapokutana”alisema.
Habari zaidi zilisema baadhi ya wabunge wa CCM walikutana faragha na
Kinana juzi jioni na kumtahadharisha kama mawaziri hao wasipowajibishwa,
CCM kitakuwa na wakati mgumu.
Vuguvugu linaloendelea hivi sasa ndani ya wabunge wa CCM, liliwahi
kujitokeza Bunge la Aprili mwaka jana na kumlazimisha Rais Kikwete
kupangua Baraza lake Mawaziri Mei 4,2012.
Kung’olewa kwa mawaziri sita waliokuwa wakishinikizwa na wabunge
wajiuzulu kulitokana na taarifa za kamati za kudumu za bunge na za
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Katika baraza lake hilo jipya, Rais aliwatosa mawaziri waliokuwa
wakishinikizwa kujiuzulu akiwemo Waziri wa Fedha, Mustafa Mkullo na
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Cyril Chami.
Wengine waliotoswa kwa shinikizo hilo lililoungwa mkono na kambi ya
upinzani ni wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige, wa Nishati na Madini,
William Ngeleja na wa Uchukuzi, Omar Nundu.
Pia Naibu Waziri wa Uchukuzi wa wakati huo, Dk Athuman Mfutakamba naye
alitoswa sambamba na Waziri wa Afya, Dk Haji Hussein Mponda na Naibu
wake, Dk Lucy Nkya.
No comments
Post a Comment