Mr. Bean Mchekeshaji mwenye elimu kubwa kichwani

KWENYE safari yake ya kwenda mapumziko
nchini Kenya mwaka 2001, rubani wa ndege yake binafsi alizimia wakiwa
angani na hapo akalazimika kuongoza ndege hiyo kwa dakika kadhaa kabla
ya rubani huyo kuzinduka na kuendelea na safari.
Hii si kama ilikuwa sehemu ya vipande
vya filamu zake za vichekesho, bali lilikuwa tukio halisi. Hapa
anazungumziwa Mr. Bean, mchekeshaji mashuhuri duniani katika filamu za
komedi.
Mr. Bean ambaye jina lake halisi ni
Rowan Sebastian Atkinson, ni mwigizaji mashuhuri Mwingereza ambaye
amepata umaarufu mkubwa duniani kutokana na kuigiza filamu za komedi.
Akiwa amezaliwa Januari 6, 1955 na
kushiriki kwenye filamu mbalimbali ikiwamo za ucheshi za Mr. Bean na
Blackadder, Atkinson amekuwa tajiri mkubwa miongoni mwa waigizaji wa
komedi na kuwa na pato linalokadiriwa kuwa la Dola 130 milioni. Umahiri
wa filamu zake za komedi ndizo zinazofanya ziendelee kupendwa hadi sasa
na hivyo kumwingizia pesa.(P.T)
Jinsi alivyopiga pesa
Atkinson kwanza amepata sifa moja,
kuwa mwigizaji maarufu zaidi Uingereza kutokana na kuigiza komedi.
Alianza kuigiza kwenye redio kabla ya kuhamia kwenye televisheni na
kisha kutengeneza mfululizo wa filamu za vichekesho zinazofahamika kama
Mr. Bean.
Kufanikiwa kwa mfululizo huo na ile
filamu yake ya Johnny English kulimfanya kuwa maarufu zaidi na kupanua
wigo wa kipato chake cha pesa ambapo hadi kufika sasa, Atkinson anatajwa
kuwa moja ya waigizaji wa komedi matajiri zaidi duniani.
Ameingiza pesa nyingi kutokana na
kuigiza kwake kuanzia kwenye redio, televisheni hadi kwenye filamu.
Alivuna Pauni 11 milioni kama ada ya ushiriki kwenye mfululizo wa filamu
za Mr. Bean.
Dola 2 milioni nyingine aliziingiza
baada ya kushiriki kwenye 'Blackadder' na kiasi kama hicho tena
alikiingiza kwa kutokea kwenye matangazo mbalimbali ya benki.
Amewekeza pia kwenye kampuni ya
upangaji wa vipindi vya televisheni na hivyo kumwongezea zaidi utajiri
wake na kumfanya afikie kadirio hilo la kuwa na kipato cha Dola 130
milioni.
Umahiri wake kwenye kuigiza unaendelea
kumwingizia kipato hadi sasa kutokana na kupata dili mbalimbali za
matangazo licha ya kwamba mfululizo wa filamu zake za Mr. Bean
umeripotiwa kufikia kikomo mwaka 2012.
Maisha ya starehe
Kutokana na kuwa na pesa za maana,
Atkinson hataki kujibanabana na amekuwa akiishi maisha ya starehe nyingi
ili kufurahia matunda yanayotokana na sanaa yake.
Anamiliki majumba ya kifahari sehemu
mbalimbali ikiwamo Chelsea, London na Oxford zote zikiwa England.
Ukiweka kando majumba yenye hadhi kubwa, Atkinson anamiliki pia magari
mengi ya kifahari na yenye thamani kubwa.
Kwenye orodha ya magari hayo, kuna
Audi R8, Honda NSX, Honda Civic Hybrid na McLaren F1 yenye uwezo wa
kukimbia kwa kilomita 350 kwa saa.
Mr. Bean ni kichaa wa magari na mara
kadhaa alipata ajali, lakini hakuwa amepata majeraha makubwa. Mwigizaji
huyo
pia anamiliki ndege yake binafsi Cessna 202. Pesa zake pia amekuwa
akizitumia katika huduma mbalimbali za kijamii akijitolea kuchangia
miradi ya UNICEF, Comic Relief, CAFOD & Save the Children.
Maisha binafsi na ndoa
Maisha ya Mr. Bean yamekuwa safi
kabisa na hana shida. Alizaliwa na wazazi Waingereza akiwa mtoto wa
mwisho kwenye familia ya watoto wanne. Ni mwigizaji ambaye elimu imelala
kichwani kutokana na kuwa na Shahada ya Pili ya masuala ya umeme
aliyoisomea kwenye Chuo Kikuu cha Oxford.
Kwenye maisha ya ndoa, alianza
kujihusisha kimahusiano na mrembo mwenye asili ya India, Sunetra Sastry
mwishoni mwa miaka ya themanini na mwaka 1990 alifunga naye pingu za
maisha.
Wanandoa hao ambao wanatajwa kuwa kwenye mapenzi motomoto wamefanikiwa kupata watoto wawili.
No comments
Post a Comment