WAJASIRIAMALI WA CHAKULA KUULA,TFDA YAPANGA KUWAENDELEZA KIUCHUMI


PICHA NA HASSAN SILAYO> MAELEZO
MAMLAKA YA CHAKULA NA DAWA
MAELEZO
KWA WAANDISHI WA HABARI KUHUSU MPANGO WA MAFUNZO NA UFUATILIAJI KWA
WAZALISHAJI WADOGO WA BIDHAA ZA CHAKULA , UKUMBI WA IDARA YA HABARI
MAELEZO, TAREHE 16 SEPTEMBA 2013
Napenda
kwa heshima na taadhima kutumia fursa hii kwa niaba ya Menejimenti ya
TFDA na wafanyakazi wote kwa ujumla kuwakaribisha katika mkutano huu.
TFDA ni taasisi ya Serikali iliyopo chini ya Wizara ya Afya na Ustawi
wa Jamii iliyoundwa chini ya sheria namba 1 ya Chakula, Dawa na Vipodozi Sura 219 kwa lengo la kudhibiti ubora na usalama wa chakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba ili kulinda afya za wananchi. Hii inamaanisha kuwa wanaolindwa ni sisi sote ikiwa ni pamoja na jamaa zetu na wananchi kwa ujumla.
Ndugu wanahabari,
Leo
tumekutana hapa kwa lengo la kupeana taarifa kuhusu mkakati wa TFDA
katika kuwaendeleza wajasiriamali wa chakula kwa lengo la kulinda
afya ya walaji, lakini pia kufanya vyakula hivyo kuweza kumudu
ushindani wa soko la ndani na nje na kuleta matokeo makubwa sasa.
Ndugu wanahabari,
Suala la usalama wa vyakula ni la msingi kwa sababu lina athari kubwa kiafya, kiuchumi na kijamii. Hata
hivyo, kama hazikudhibitiwa ipasavyo matumizi ya bidhaa hizi yanaweza
kuleta madhara makubwa ikiwa ni pamoja na kusababisha ulemavu, kupoteza
maisha na hata kudhoofisha uchumi wa nchi. Kwa sababu hiyo TFDA
kama taasisi iliyopewa dhamana ya usimamizi wa bidhaa hizo inahakikisha
kwamba vyakula vinavyouzwa katika soko la Tanzania vinakidhi viwango
vya usalama, ubora na ufanisi.
TFDA
ina majukumu mengi kwa mujibu wa Sheria. Miongoni mwa majukumu hayo ni
pamoja na udhibiti wa uhifadhi, usafirishaji, usindikaji, uagizaji na
usambazaji vyakula. Katika kutekeleza jukumu lake, TFDA inasajili
majengo yote yanayotumika katika usindikaji wa vyakula ikiwa ni pamoja
na utoaji wa vibali vya usindikaji, uingizaji na usafirishaji nje
vyakula. Majukumu mengine yanayofanywa na TFDA ni pamoja na ufuatiliaji
usalama wa vyakula kwenye soko na utoaji wa elimu kwa wadau mbalimbali.
Ufanisi
wa utekelezaji wa majukumu haya unawezekana kutokana na mifumo mizuri
ya utendaji kazi iliyojiwekea ikiwa ni pamoja na kufanya kazi kulingana
na viwango vya kimataifa vya ISO 9001: 2008.
Ndugu wanahabari,
TFDA
kama taasisi ya udhibiti wa vyakula, tunatambua kuwa tuna wajibu wa
kuwasaidia wasindikaji wadogo wa vyakula ili waweze kukua na kuzalisha
vyakula kwa mujibu wa Kanuni bora za uzalishaji ili viweze kumudu
ushindani wa soko la ndani na nje kutokana na biashara huria na
kuzalisha chakula salama.
Takwimu
zinaonesha asilimia 75 ya viwanda vya vyakula nchini ni viwanda vidogo
(Kwa mujibu wa upembuzi yakinifu uliofanyika 2004/5) ambapo kukua kwa
viwanda hivi kutakuwa na mchango mkubwa katika; kuongeza ajira na kipato
katika ngazi ya kaya, kukuza kilimo cha mazao ya chakula kutokana na
kuwepo na soko la mazao ya vyakula na kuchangia katika pato la taifa.
TFDA
inatambua kuwa viwanda vidogo vina nafasi kubwa ya kuchangia katika
pato la Taifa kutokana na uwingi wake lakini pia vinaweza kutoa mchango
mkubwa katika kuleta athari za kiafya ikiwa bidhaa zake hazitakidhi
viwango vya usalama na ubora.
Ndugu wanahabari,
Kwa kuzingatia mambo hayo niliyotaja, TFDA imeamua kuja na mkakati wa kuwafundisha wajasiriamali wadogo wa vyakula ili kuwawezesha
wasindikaji hawa kujua sheria, kanuni na miongozo inayohusu usindikaji
wa chakula salama pamoja na kuongeza kiwango cha uzingatiaji wa kanuni
bora za uzalishaji wa vyakula.
Hadi
sasa mafunzo hayo yametolewa kwa wajasiriamali 417 kutoka katika Kanda
zote katika mikoa ya Dar es Salaam (90), Singida (44), Mbeya (76),
Arusha (54), Dodoma (98) na Mwanza (55).
Ndugu wanahabari,
Aidha,
kutoka mwaka 2012/13, TFDA imekuwa inaendesha mpango wa majaribio kwa
wasindikaji wadogo wa mafuta ya alizeti mkoani Singida ili kuelekeza
namna ya kuboresha uzingatiaji wa matakwa ya Sheria kuhusu misingi ya
usafi na uzalishaji bora.
Mpango huu umehusisha hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na;
i. Kufanya tathmini ya kiwango cha uzingatiaji wa sheria
ii.Kuainisha maeneo yenye mapungufu
iii. Kuandaa mafunzo yanayozingatia mapungufu yaliyojionesha
iv. Kuwasilisha taarifa ya tathmini kwa wadau pamoja na wasimamizi wa sheria katika eneo husika
v. Kukubaliana namna ya kutatua upungufu na kuwa na ratiba ya utekelezaji kwa mambo ya muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu
vi. Ufuatiliaji wa makubaliano
vii.Tathmini ya jumla kwa makubaliano ya muda mfupi na wa kati ili kujua kiwango cha utekelezaji.
Lengo
la mpango huu ni kusambazwa nchi nzima ikiwa utaleta matokeo mazuri kwa
mkoa huu wa Singida ambao ni wa majaribio ifikapo mwaka 2016/17.
Ndugu wanahabari,
Kwa
kuhitimisha, TFDA inatoa shukurani kwa ushirikiano ambao mmekuwa
mkiuonesha katika kutoa taarifa za kiudhibiti pale inapotokea pamoja na
kuelimisha jamii.
Rai
yetu kwenu ni kuendelea kutumia kalamu zenu katika kuwaondolea hofu
wananchi kuhusu usalama na ubora wa bidhaa za chakula, dawa, vipodozi na
Vifaa tiba vilivyopo katika soko kutokana na mifumo thabiti iliyowekwa
na TFDA.
Aidha,
tunatoa wito kwa wananchi kwamba ikiwa mtu atabaini au kuwa na mashaka
juu ya usalama na ubora wa bidhaa hizo basi asisite kuwasiliana nasi
kupitia ofisi zetu za Makao Makuu na za Kanda zilizopo Extenal Mabibo,
Mwanza, Arusha, Mbeya, Dodoma na Ofisi za Waganga wakuu wa Mikoa na
Wilaya au kutoa taarifa katika kituo chochote cha polisi kilicho jirani
naye.
Asanteni kwa kunisikiliza!
No comments
Post a Comment