Zinazobamba

TABOA WAITAKA SERIKALI KUIMARISHA ULINZI NA USALAMA WA KUTOSHA BARABARANI KABLA YA KUONDOA ZUIO LA MABASI YA ABIRIA KUTEMBEA USIKU


Chama cha wenye Mabasi yaendayo Mkoani (TABOA) kimeitaka serikali imarishe usalama barabarani kabla ya kuondoa Zuio lililopo sasa hivi la mabasi ya abiria kusafiri usiku.

Msimamo huo umetolewa na Katibu Taboa, Enea Mrutu kufuatia kauli iliyotolewa Bungeni wiki iliyopita na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuwa Serikali inaangalia uwezekano wa kuondoa zuio hilo katika usafiri huo wa mabasi ya abiria.
TABOA
Waziri Pinda alitoa kauli wakati akijibu swali la Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Murtaza Mangungu (CCM), aliyetaka kujua serikali ina mpango gani wa kurejesha utaratibu wa mabasi ya abiria kusafiri kwa saa 24 kama ilivyokuwa awali.
“Ni kweli kulikuwa na zuio hilo lakini lilitokana na kuongezeka kwa ajali na hasa wakati wa usiku, lakini kwa sasa kuna uboreshaji wa miundombinu tunaweza kuangalia jinsi gani ibadilishwe,” alisema Pinda
Mrutu alisema licha ya malengo mazuri ya Serikali katika kuboresha sekta ya usafiri hapa nchini, lakini kwa suala la kutembea usiku linapaswa kufanyiwa utafiti kwa kuwa lina changamoto nyingi zinazohatarisha usalama wa mabasi na abiria kwa ujumla.
Alisema ukiacha madhara ya ajali za barabarani yanayowezwa kusababishwa kutokana na uwingi wa Malori nyakati hizo,pia bado maeneo mengi hapa nchini yamekubikwa na vitendo vya utekeji wa mabasi.

“Sasa hivi pamoja na kwamba mabasi yanasafiri mchana, bado yanatekwa je itakuwaje kama yataruhusiwa kutembea usiku, hiisawa na kumpeleka swala mbele ya kinywa cha Simba mwenye njaa” aliongeza.

Alisema suala la kuruhusu mabasi hayo kutembea usiku, pia kunaweza kuongeza idadi ya ajali za barabarani zitakazohusisha malori na gari ndogo kwa kuwa mengi yanatumia muda huo kusafiri.

Aliomba chama hicho kushirikishwa katika masula mengi yanayohusu sekta hiyo kwa madai kuwa watasaidia kutoa michango inayoweza kuleta ufanisi kwa maendeleo ya nchi.

Aidha aliipongeza Serikali kwa kuboresa miundombinu ya barabara kwa kiasi kikubwa nchini suala lililorahisisha usafiri wa mabasi huku changamoto ya ubora wa mabasi ikibaki kuwa kwao.

No comments