Zinazobamba

ABOOD YAGONGA IST BUNJU, WATU WANNE WAFARIKI


Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Watu wanne wamefariki dunia baada ya basi la kampuni ya Abood kugongana na gari dogo aina ya Toyota IST katika eneo la Bunju Sokoni, Kinondoni, jijini Dar es Salaam.

Ajali hiyo ilitokea Septemba 7, 2026, majira ya saa 1:40 usiku katika Barabara ya Bagamoyo, ambapo basi lenye namba za usajili T 235 EMJ, aina ya Yutong, lililokuwa likitokea Tegeta kuelekea Bunju kwa safari ya mkoani Tanga, liligongana na gari lenye namba T 274 ERU, aina ya Toyota IST.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, SACP Jumanne Muliro, chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa basi hilo, ambaye alifanya kitendo cha kulipita gari lingine bila kuchukua tahadhari kwa watumiaji wengine wa barabara.

Miongoni mwa waliofariki katika ajali hiyo ni dereva wa Toyota IST, Hamad Mohamed Juma, maarufu kama Majid, mwenye umri wa miaka 37, mkazi wa Mtoni Mtongani, Dar es Salaam.

Wengine ni Edward Kimanyara, mstaafu na mkazi wa Yombo Dovya, Temeke; Magdalena Manyenga (45), mkazi wa Temeke; pamoja na Melina Emmanuel Kayoka (42), mkazi wa Yombo Kisiwani, Temeke.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Mwananyamala, Kinondoni, Dar es Salaam.

Wakati huo huo, dereva wa basi hilo, Christivian Steven Shemuhilu (38), anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa hatua zaidi za kisheria.

Jeshi la Polisi limewataka watumiaji wote wa barabara, wakiwemo waendeshaji wa vyombo vya moto, kuendelea kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za usalama barabarani ili kuzuia na kuepusha ajali.

No comments