Zinazobamba

CCM DAR YAUNGA MKONO MCHAKATO WA KUMPATA MAKAMU WA RAIS, YAMPONGEZA SAMIA


Na Mussa Augustine.Dar es Salaam

Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam imeunga mkono mchakato wa kumpata Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Deogratius Ndejembi, ikisema uamuzi huo umezingatia maslahi mapana ya Taifa na matakwa ya Katiba.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Abbas Mtemvu, amesema hayo leo, Septemba 7, 2026, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu maazimio ya kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa kilichofanyika Septemba 6, mwaka huu.

Amesema kikao hicho kimeunga mkono maamuzi ya Kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kilichofanyika Agosti 26, 2026, kuhusu mchakato huo.

Mtemvu amesema maamuzi hayo yamezingatia maslahi mapana ya Taifa pamoja na matakwa ya Katiba ya CCM na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa mujibu wa Mtemvu, mchakato huo ulizingatia Ibara ya 103(8) ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977, kama ilivyorekebishwa, pamoja na Ibara ya 50(2)(c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aidha, amesema Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Dar es Salaam imempongeza Makamu wa Rais aliyeteuliwa baada ya kutangazwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuthibitishwa na Bunge na kuapishwa kwa mujibu wa Katiba.“CCM Mkoa wa Dar es Salaam imemtakia Makamu wa Rais huyo kazi njema na mafanikio katika kutekeleza majukumu aliyoaminiwa na Rais na Mwenyekiti wa CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan,” amesema Mtemvu.

Katika hatua nyingine, Mtemvu amesema Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa huo inaunga mkono uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, huku ikimpongeza kwa kazi anayoifanya katika kukiongoza chama na kuendesha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Amesema CCM Mkoa wa Dar es Salaam itaendelea kuunga mkono juhudi za uongozi wa Dk. Samia, huku ikimtakiwa afya njema na mafanikio katika kuendelea kulitumikia Taifa.

No comments