Zinazobamba

IGP WAMBURA: AMANI IPO, WANANCHI WAJIKITE KWENYE MAENDELEO


Na Mwandishi Wetu

DAR ES SALAAM: Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Camillus Wambura, amewataka wananchi kuendelea na shughuli zao za kiuchumi na kijamii bila hofu, akisisitiza kuwa hali ya usalama nchini ni shwari na imara.

IGP Wambura alitoa kauli hiyo jana, Septemba 4, 2026, alipokutana na kuzungumza na baadhi ya viongozi wa Kijiji cha Jaribu Mpakani, Kata ya Mjawa, Mkoa wa Kipolisi Rufiji.

Katika mazungumzo hayo, alisisitiza umuhimu wa wananchi kutumia fursa ya amani na utulivu uliopo kuendelea kufanya shughuli za uzalishaji na kujiletea maendeleo.

Alisema pamoja na jukumu la Serikali na vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha amani inalindwa, jamii nayo ina wajibu wa kushiriki katika kulinda utulivu uliopo nchini.

IGP Wambura pia alizitaka familia kuimarisha malezi ya watoto na kusimamia maadili, akisema hatua hiyo ni muhimu katika kujenga kizazi kinachoheshimu sheria, amani na uzalendo.

“Jamii inapaswa kuendelea kuimarisha malezi ya watoto na kusimamia suala la maadili ili kuwa na jamii yenye kuipenda na kuithamini amani iliyopo,” alisema.Katika hatua nyingine, IGP Wambura alifanya ziara ya ukaguzi wa miundombinu ya ujenzi wa vituo vya Polisi pamoja na Ofisi ya Kamanda wa Polisi katika Mkoa wa Kipolisi Rufiji.

Alisema Jeshi la Polisi linaendelea kuthamini juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita katika kulipatia rasilimali mbalimbali kwa ajili ya kuboresha mazingira ya utendaji kazi na kuongeza ufanisi wa jeshi hilo.

Kwa mujibu wa IGP Wambura, uboreshaji wa miundombinu ya Jeshi la Polisi ni sehemu muhimu ya kuwezesha askari kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, hususan katika kulinda usalama wa raia na mali zao.

Katika ziara hiyo, IGP Wambura aliambatana na Kamishna wa Fedha na Lojistiki, CP Liberatus Sabas; Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, DCI Ramadhani Kingai; Kamishna wa Utawala na Menejimenti ya Rasilimaliwatu, CP Tatu Jumbe, pamoja na maafisa wengine wa Jeshi la Polisi.IGP Wambura alisema Jeshi la Polisi litaendelea kutumia rasilimali zinazotolewa na Serikali kwa ufanisi ili kuboresha huduma za kiusalama na kuhakikisha wananchi wanaendelea kuishi katika mazingira ya amani, utulivu na usalama.



No comments