Zinazobamba

TAFITI ZA USAFIRI ZIGEUKE SULUHISHO LA CHANGAMOTO NA KICHOCHEO CHA UCHUMI” – PROF. MBARAWA

Na Mwandishi wetu: Dar es salaam 

Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amewataka watafiti nchini kuhakikisha tafiti wanazofanya katika sekta ya usafiri na usafirishaji zinatoa suluhisho la changamoto halisi na kuchangia maendeleo ya kiuchumi, badala ya kuishia kwenye makabrasha na mikutano

Akifungua Mkutano wa Nne wa Kimataifa kuhusu Usafiri, Lojistiki na Usimamizi leo Agosti 20, 2026, katika Ukumbi wa Mikutano Mlimani City, Dar es Salaam, Prof. Mbarawa amesema Serikali inahitaji tafiti zitakazosaidia kupunguza gharama za usafirishaji, kuongeza ufanisi wa bandari na reli, kuboresha usalama na kuimarisha miundombinu inayokabiliana na mabadiliko ya tabianchiAmesema Serikali inaendelea kuwekeza katika SGR, bandari, ATCL, BRT, barabara na usafiri kwa  njia ya maji na kusisitiza umuhimu wa kuunganisha mifumo hiyo ili kujenga mfumo mmoja wa usafiri wenye ufanisi, unaopunguza gharama na muda wa kusafirisha abiria na mizigo

“Haipaswi uchumi ukue halafu usafiri ufuate , usafiri wenyewe lazima uwe kichocheo cha ukuaji wa uchumi nchini na miundombinu ya usafiri inapaswa kuzalisha fursa za biashara, ajira na uwekezaji" amesisitiza Mbarawa

Prof. Mbarawa amewataka washiriki wa mkutano huo kuwasilisha mapendekezo yanayotekelezeka na yenye matokeo yanayopimika na kusisitiza kuwa mafanikio ya tafiti yanapaswa kuonekana katika kupunguza gharama, kuongeza ufanisi, kuboresha usalama na kuchochea ushindani wa Tanzania katika masoko ya kikanda na kimataifaKwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Prof. Ulingeta Mbamba, amesisitiza umuhimu wa tafiti na ubunifu katika kutatua changamoto za sekta ya usafiri, huku Mkuu wa Chuo cha NIT, Dkt. Prosper Mgaya, akieleza kuwa chuo hicho kitaendelea kuimarisha tafiti, ubunifu na ushirikiano na wadau wa ndani na nje ya nchi

Mkutano huo utakaofanyika kwa siku mbili, Agosti 20 na 21, 2026, ukiwa na kaulimbiu inayolenga "Kuwa na mifumo ya usafiri iliyo janja, rafiki kwa mazingira, inayounganisha na kuhimili changamoto”, unawakutanisha watafiti, wataalamu, watunga sera, Serikali na wadau wa kisekta kutoka ndani na nje ya nchi.



No comments