SERIKALI YATOA MIEZI SITA KWA WAMILIKI WA MIUNDOMBINU MUHIMU YA TEHAMA KUJISAJILI
Serikali imewataka wamiliki na waendeshaji wa miundombinu muhimu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika sekta mbalimbali nchini kuhakikisha miundombinu hiyo inasajiliwa na kulindwa kwa mujibu wa sheria, ikielezwa kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuhakikisha huduma muhimu zinaendelea kupatikana hata wakati wa mashambulizi ya kimtandao, majanga au dharura nyingine.
Akizungumza na waandishi wa habari mapema leo, Agosti 19, 2026, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki, amesema udhibiti wa miundombinu hiyo unalenga kuhakikisha mifumo muhimu inakuwa salama, inapatikana na inaendelea kufanya kazi kwa uhakika wakati wote.
Waziri Kairuki amesema hatua hiyo inatekelezwa kwa kuzingatia matakwa ya Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015, pamoja na maelekezo yaliyotolewa kupitia Tangazo la Serikali linalobainisha miundombinu muhimu ya TEHAMA kutoka sekta mbalimbali inayopaswa kulindwa kwa mujibu wa sheria.
“Zoezi la tathmini na usajili wa miundombinu muhimu ya TEHAMA limepewa muda wa miezi sita, na muda huu unatarajiwa kukamilika Septemba 15, 2026,” amesema Waziri Kairuki.
Ameongeza kuwa hadi sasa zimebaki takribani miezi miwili na nusu kabla ya muda huo kumalizika, hivyo Wizara imeona umuhimu wa kutoa taarifa kwa umma kupitia vyombo vya habari ili kuwafikia wamiliki na waendeshaji wa miundombinu hiyo katika sekta mbalimbali.
Amezitaja sekta zinazohusika kuwa ni pamoja na mawasiliano, fedha na benki, maji, afya, viwanda, madini, usafirishaji, chakula na kilimo, ujenzi, usafiri wa maji, uvuvi, mafuta, elimu, nishati, pamoja na sekta nyingine zenye miundombinu muhimu ya TEHAMA.
Amesema wamiliki au waendeshaji wa miundombinu muhimu ya TEHAMA wanatakiwa kuingia katika mfumo maalumu wa usajili wa CII na kuwasilisha taarifa zinazohitajika kabla ya kuanza kutangaza au kutumia taarifa zinazohusu miundombinu yao.
Waziri Kairuki amesema miongozo mbalimbali iliyoandaliwa itasaidia wamiliki na waendeshaji kupata uelewa wa namna ya kutekeleza matakwa ya usajili, ulinzi na usimamizi wa miundombinu muhimu ya TEHAMA.
“Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imeandaa mpango wa kutoa elimu kwa umma kwa makundi na sekta mbalimbali kuhusu usajili, ulinzi na ujenzi wa miundombinu hiyo,” amesema Waziri Kairuki.
Amesisitiza kuwa wamiliki na waendeshaji wa miundombinu muhimu wamehimizwa kushirikiana kwa karibu na timu za wataalamu kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari katika masuala ya usajili, uzingatiaji wa matakwa ya usalama na kupata msaada wa kitaalamu.
Amesema msaada unaweza kupatikana kupitia namba za simu na njia nyingine rasmi za mawasiliano zilizotolewa na Wizara, pamoja na barua pepe maalumu ya usajili na fomu ya maombi inayopatikana kwa ajili ya matumizi ya usajili wa CII.
Halikadhalika, Serikali imeonya kuwa kutotangaza au kutosajili miundombinu muhimu ya TEHAMA kwa mujibu wa sheria ni kosa linaloweza kuchukuliwa hatua za kisheria.
Waziri huyo amefafanua kuwa sheria inaweka adhabu kwa mtu anayehusika na ukiukaji wa matakwa yanayohusu miundombinu muhimu ya TEHAMA, ikiwa ni pamoja na faini ya fedha, kifungo au adhabu zote kwa pamoja, kutegemea kosa lililofanyika.
Serikali imesisitiza kuwa usajili wa miundombinu hiyo si suala la kuongeza taratibu kwa taasisi, bali ni hatua muhimu ya kutambua miundombinu inayohitaji ulinzi maalumu na kuweka mazingira ya kuhakikisha huduma muhimu zinaendelea kutolewa kwa ufanisi.
Aidha, hatua hiyo itasaidia Serikali kutambua mapema vitisho vinavyoweza kuathiri miundombinu muhimu, kuweka teknolojia na mifumo ya ulinzi, pamoja na kushirikiana na mamlaka husika katika kuzuia vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama wa taifa na uchumi.
Wizara imewahimiza wamiliki na waendeshaji wa miundombinu muhimu kutoa taarifa kwa mamlaka pale wanapobaini vitisho au matukio yanayoweza kuhatarisha usalama wa mifumo yao, kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa kisheria.

No comments
Post a Comment