MALOTO AONYA WASAIDIZI WA RAIS SAMIA WENYE TAMAA YA URAIS

URAIS 2030 USIMKWAMISHE RAIS SAMIA KATIKA KUWATUMIKIA WANANCHI- MALOTO
MALOTO ATAJA ATHARI, WASAIDIZI WA RAIS SAMIA KUJIPANGA NA URAIS 2030
Mwanahabari Luqman Maloto amewaonya wasaidizi wa Rais Samia Suluhu Hassan wenye tamaa ya Urais kuacha kuutolea macho urais wa 2030 na badala yake wafanye kazi waliyopewa kwa uaminifu kwajiili ya maendeleo ya Tanzania.
Katika makala yake, kwa kuwataja, Maloto amesema Makamu wa Rais Dk. Emmanuel Nchimbi na Waziri Mkuu Dk. Mwigulu Nchemba ni wasaidizi wakuu wa Rais kwa mujibu wa Katiba, hivyo wanapaswa kutumia nafasi zao kumuunga mkono Rais Samia na kuhakikisha Serikali inatimiza wajibu wake. Hata hivyo, amesema mitaani kumekuwa na mazungumzo yanayowahusisha wawili hao na mbio za Urais wa 2030, ingawa hakuna kauli yao ya moja kwa moja inayothibitisha kuwa wanajiandaa kugombea.
Amesema Nchemba anatajwa pia kutokana na historia yake ya kushiriki mchakato wa kuwania tiketi ya CCM mwaka 2015, wakati Nchimbi hakushiriki. Kwa Maloto, jambo la msingi si kama wana ndoto ya Urais, bali kama wana tamaa ya Urais inayoweza kuwafanya washindwe kuitumikia Serikali ya sasa kwa uaminifu.
“Wasaidizi wa Rais wafanye kazi badala ya kuutolea macho Urais. Tamaa ya Urais itawafanya wawe wapinzani wa Rais Samia, sasa watawezaje kufanya kazi kwa maelewano ili kuwaletea watanzania maendeleo? Msaidizi mwenye tamaa ya Urais hutamani Rais afeli ili yeye apate mtaji wa kisiasa. Vema kukaa pembeni ili kutumikia ndoto kuliko kumsaidia Rais kwa ujanjaujanja." amesema Maloto akionya tabia ya kumdhoofisha kiongozi wayemtumikia kama njia ya kujitengenezea mazingira ya kuutaka Urais.
Maloto amesema tamaa ya Urais inaweza kusababisha kujenga makundi, kuvujisha siri, kujitenga na lawama za Serikali na hata kutamani Serikali iliyopo ifeli ili kupata mtaji wa kisiasa, akibainisha kuwa historia ya siasa imeonesha madhara ya makundi yanapojitokeza wakati wa maandalizi ya mabadiliko ya uongozi.
Ameeleza kuwa Urais unaweza kuja kutokana na kazi nzuri na mazingira ambayo mtu hawezi kuyapanga, akitolea mfano Gerald Ford wa Marekani na Fernando Henrique Cardoso wa Brazil, akisisitiza kufanya kazi zao kwa uadilifu na kuacha muda uamue nani atafaa kuwa Rais.
Maloto amesema Rais Samia kwa sasa ana majukumu mazito, yakiwemo kushughulikia masuala ya Oktoba 29, 2025 kupitia tume mbalimbali, pamoja na kuendesha diplomasia na kujenga ushirikiano wa uwekezaji na viongozi mbalimbali wa Afrika na dunia.
Kwa msingi huo, Maloto amewataka wasaidizi wa Rais kuacha siasa za kujitengenezea nafasi na badala yake wamsaidie Rais Samia kuwaletea Watanzania maendeleo, akisisitiza kuwa utendaji wao wa leo unaweza kuwa ndio utakaowabeba kesho, ikiwa Urais umeandaliwa kwao.
No comments
Post a Comment