WADAU WAKUTANA KUJADILI UTEKELEZAJI WA MKAKATI WA NISHATI SAFI YA KUPIKIA
📌*Lengo ni kuharakisha utekelezaji wake*
Katika kuendeleza jitihada za kuimarisha utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia wa mwaka 2024–2034, Jumuiya ya Wadau wa Nishati Jadidifu Tanzania (TAREA) na African Enterprise Challenge Fund (AECF), kwa kushirikiana na Wizara ya Nishati, wameendesha mdahalo maalumu uliowakutanisha wadau wa maendeleo, Asasi za kiraia, Taasisi za Kiserikali pamoja na wazalishaji na wasambazaji wa teknolojia za nishati safi ya kupikia.
Lengo la mdahalo huo ni kujadili sera na masuala ya kiudhibiti yanayoweza kuathiri utekelezaji wa mkakati huo na kuandaa mapendekezo yatakayosaidia kuharakisha utekelezaji wake.
Mdahalo huo umefanyika leo, Agosti 6, 2026, jijini Dar es Salaam, ukitoa fursa kwa washiriki kujadili maendeleo yaliyofikiwa katika utekelezaji wa mkakati huo pamoja na masuala mtambuka yanayohusu uhifadhi wa misitu, uendelezaji wa nishati endelevu ya tungamotaka, nafasi ya Serikali za Mitaa katika uzalishaji endelevu wa nishati, na mfumo wa sera na kanuni zinazoweza kuwezesha au kukwamisha maendeleo ya suluhisho za nishati safi ya kupikia.
Washiriki pia wamejadili changamoto zinazokabili sekta hiyo, ikiwemo kodi, upatikanaji wa mitaji, uzalishaji wa ndani wa teknolojia za nishati safi ya kupikia na ushiriki wa sekta binafsi.
Mdahalo huo una lengo la kuhakikisha majadiliano hayo yanazaa mapendekezo yanayotekelezeka, yanayobainisha taasisi zitakazowajibika pamoja na muda wa utekelezaji wake.
Akifungua mdahalo huo, Mkuu wa Kitengo cha Nishati Safi ya Kupikia kutoka Wizara ya Nishati, Bw. Nolasco Mlay, amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ni Kinara wa Nishati Safi ya Kupikia barani Afrika, ameifanya Tanzania kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ndani na nje ya nchi.
Amesema majadiliano hayo ni sehemu ya jitihada za kuunga mkono maono ya Mheshimiwa Rais kwa kuhakikisha uongozi wa Tanzania katika agenda ya nishati safi ya kupikia unaambatana na utekelezaji wenye matokeo chanya kwa wananchi kupitia sera, mipango na ushirikiano wa wadau mbalimbali.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wadau wa Nishati Jadidifu Tanzania (TAREA), Dkt. Prosper Magali, amesema bado zipo changamoto zinazohitaji kufanyiwa kazi, ikiwemo ubora wa vifaa na teknolojia za nishati safi ya kupikia pamoja na upatikanaji wa rasilimali za kifedha.
Amesisitiza kuwa wadau wanaendelea kujadili namna mkakati wa nishati safi ya kupikia unaweza kuboreshwa ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wake na kufikia malengo ya Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia.



No comments
Post a Comment