Zinazobamba

WAZIRI KAPINGA APONGEZA KIWANDA CHA NIDA

Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga ameupongeza uongozi wa kiwanda Cha kutengeneza nguo cha NIDA kwa kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuimarisha sekta ya viwanda na kukuza uchumi wa Nchi.

Pongezi hizo amezitoa Julai 8,2026 wakati alipo tembelea banda la Kiwanda cha NIDA katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) yanayoendelea jijini Dar es Salaam na kueleza kuridhishwa na utendaji wa kiwanda hicho.

"Napenda kuwapongeza kwa juhudi kubwa mlioifanya ya kuunga mkono Serikali katika kuinua sekta ya viwanda,mmekua mkizalisha bidhaa nzuri kwa Watanzania"amesema Waziri Kapinga.

Kwa upande wake Meneja wa Mahusiano wa NIDA,Mohamed Honelo,amesema kuwa kampuni hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa katika kutatua changamoto ya ajira kwa kutoa ajira za moja kwa moja kati ya 1,500 na 2,000, pamoja na ajira za muda kulingana na mahitaji ya uzalishaji.

Honelo amesema kampuni imejenga mnyororo kamili wa uzalishaji unaoanzia kwa kuwawezesha wakulima wa pamba, kununua mazao yao, kuyasindika kuwa nyuzi na vitambaa katika kiwanda chake kilichopo Mbeya, kisha kuvipeleka NIDA Textile Mills kwa ajili ya uchapishaji kabla ya kuviuza kupitia maduka yake.

"Mfumo huu unaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 inayolenga kuongeza viwanda nchini, kuzalisha ajira, kukuza biashara na kuongeza mchango wa sekta ya viwanda katika uchumi wa Taifa."amesema Honelo Nakuongeza kuwa"bidhaa za kampuni yetu, zikiwemo kanga, vitenge, mashuka na bidhaa nyingine zinazotokana na pamba, zinapatikana katika maduka ya NIDA na NIDA Textile Mills,nawakaribisha wananchi kuzinunua na kuunga mkono bidhaa zinazozalishwa hapa nchini."

Hata hivyo ametumia fursa hiyo kuiomba Serikali kuweka utaratibu utakaowezesha sehemu kubwa ya pamba inayozalishwa nchini kubaki kwa matumizi ya viwanda vya ndani badala ya kuuzwa nje kama malighafi.

Amesema kuwa Serikali iweke akiba ya pamba kwa ajili ya viwanda vya ndani,ili iwe rahisi kupatikana kwa malighafi hiyo.Amesema gharama kubwa za uzalishaji zinapunguza uwezo wa viwanda vya ndani kushindana na bidhaa kutoka nje, huku wazalishaji wa nchi nyingine wakinufaika na gharama ndogo za uzalishaji zinazowaruhusu kuuza bidhaa kwa bei nafuu zaidi.

"Naipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kuhamasisha maendeleo ya sekta ya viwanda,akisema hatua hiyo itaongeza ajira, kukuza uchumi na kuifanya Tanzania kuwa taifa lenye msingi imara wa viwanda."amesema Honelo 

No comments