Zinazobamba

COASCO KUHAKIKISHA SEKTA YA USHIRIKA INAKUA IMARA

Na Mwandishi wetu 

Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO) limesema limejipanga kuhakikisha sekta ya ushirika inakuwa imara kupitia ukaguzi wa uhakika unaolenga kuongeza uwajibikaji, uwazi na kuimarisha utendaji wa vyama vya ushirika nchini.

Hayo yamebainishwa leo Julai 8,2026 na Kaimu Mkurungezi Mkuu (COASCO),CPA, Jeremiah Mugeta mara baada ya kutembelea Taasisi zilizopo chini ya wizara ya Kilimo zinazoshiriki katika  maonesho ya 50 ya kimataifa ya biashara sabasaba yanayoendelea katika viwanja vya mwalimu julias Nyerere Jijini Dar es salaam.

Amesema malengo ya Taasisi hiyo ni kuhakikisha wanaushirika wanapata elimu bora pamoja na kufahamu misingi, kanuni na taratibu za uendeshaji wa vyama vya ushirika ili viweze kufanya kazi kwa ufanisi.

"COASCO  ni jicho la Serikali katika sekta ya ushirika, COASCO hufanya ukaguzi wa kila mwaka na kuandaa taarifa ya jumla inayoonesha matokeo ya utendaji wa vyama vya ushirika pamoja na kutoa maoni ya kitaalamu kuhusu ukaguzi uliofanyika"amesemaAmesema ifikapo mwezi Septemba mwaka huu itatoa ripoti maalumu ya ukaguzi kwa mwaka wa fedha 2025/26, ambayo itaeleza hali ya usimamizi na matumizi ya fedha katika vyama vya ushirika.

"COASCO  ina mchango mkubwa katika kuimarisha sekta ya kilimo kutokana na wakulima wengi kujiunga na vyama vya ushirika, jambo hili limeongeza umuhimu wa kuhakikisha ukaguzi unafanyika kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vya kitaalamu.

Amesema ukaguzi unaofanywa unalenga kubaini na kutoa taarifa sahihi kuhusu matumizi ya fedha zinazopitia katika vyama vya ushirika, hatua inayosaidia kuimarisha uwajibikaji na kuongeza imani ya wanaushirika.Ameongez kuwa Taasisi hiyo imeendelea kutoa huduma za ushauri kwa vyama vya ushirika katika maeneo mbalimbali ikiwemo uzingatiaji wa sheria za kodi, uandaaji wa miongozo na taratibu za uendeshaji, hatua inayochangia kuongeza tija na kuimarisha utawala bora katika vyama vya ushirika nchini.



No comments