TANESCO INAENDELEA KUTOA ELIMU YA TEKNOLOJIA YA KUDHIBITI VIFAA VYA UMEME KATIKA MAONESHO YA 50 YA SABASABA

*Wananchi waombwa kutembelea banda la TANESCO kupata elimu hiyo.
Na Mussa Augustine
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) linaendelea kutoa elimu kuhusu teknolojia ya Nyumba Janja (Smart House), inayorahisisha matumizi ya umeme kwa kumwezesha mtumiaji kudhibiti vifaa vya umeme akiwa popote alipo.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Huduma kwa Wateja wa TANESCO, Irine Gowelle, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika banda la TANESCO kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba).
Aidha, Gowelle amesema kuwa kupitia mfumo wa kidijitali wa Smart Life, mtumiaji anaweza kuwasha na kuzima vifaa vya umeme kwa kutumia simu ya mkononi kupitia mtandao, hata akiwa mbali na nyumba yake.
"Teknolojia hii inalenga kuongeza urahisi, usalama na udhibiti katika matumizi ya umeme majumbani na maofisini. Hivyo, ni vyema wananchi wakafika kwenye banda letu ili waweze kujionea na kujifunza teknolojia hii," amesema.
Ameongeza kuwa, mbali na kudhibiti vifaa vya umeme kwa njia ya mtandao, mfumo huo humwezesha mtumiaji kufuatilia matumizi ya umeme ya kila siku na kubaini kifaa kinachotumia umeme mwingi zaidi, hatua inayosaidia kupanga matumizi bora ya nishati na kupunguza matumizi yasiyo ya lazima.
Aidha, amesema mfumo wa Smart Life hutoa taarifa za hitilafu zinazoweza kujitokeza kwenye vifaa vya umeme vilivyounganishwa katika mfumo huo kupitia simu ya mkononi, hivyo kumwezesha mtumiaji kuchukua hatua kwa wakati.
Halikadhalika, amesema mtumiaji anaweza kupanga muda wa kuwasha na kuzima vifaa vya umeme pamoja na kudhibiti matumizi ya soketi na swichi za umeme popote alipo, mradi awe na huduma ya intaneti.Amesema kuwa mfumo wa Smart Life unaweza kufungwa katika nyumba yenye mfumo wa kawaida wa umeme kwa kuunganisha vifaa maalumu vya Smart Socket na Smart Switch, vinavyomwezesha mtumiaji kufurahia urahisi wa kudhibiti matumizi ya umeme kwa njia ya kidijitali.
Aidha,amesema kuwa nyumba janja hutumia mfumo wa kisasa wa waya za umeme (wiring) unaoweza kusaidia kuzuia majanga ya moto, sambamba na kuongeza ufanisi wa matumizi ya nishati.
No comments
Post a Comment